Monday, June 8, 2015

mchungaji Kakobe amwambia  mheshimiwa  Nyalandu na Mwigulu


Katika hali isiyo ya kawaida Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, Zachary Kakobe amefunguka na Injili nzito kwa kuwataja baadhi ya wagombea urais kwamba waingie katika wokovu kamili badala ya kuwa na wokovu aliodai ni wa kuigiza.

Katika moja ya mahubiri yake kanisani kwake Mwenge, Sam Nujoma Road, Askofu Kakobe  aliwataja wagombea urais Mwingulu Nchemba na Lazaro Nyalandu pamoja na mmoja wa mawaziri maarufu, Dk. Harisson Mwakyembe kwamba wanapaswa kuokoka ili mambo yao yawanyokee.
 
“Leo sikwepeshi maneno. Kila mtu anajifanya ameokoka lakini huo ni wokovu ule. Nyalandu (Lazaro), ameokoka kweli? Mwigulu (Nchemba), ameokoka kweli, Mwakyembe (Dk. Harisson) ameokoka? Angalia sasa kwa viwango hivi ndiyo utajua umeokoka au namna gani.

“Mimi hapa sitafuti mtu, waziri ukija hapa, rais ukija hapa utanisaidia nini, rais huwezi kunipa hela mimi….mimi ndiyo naweza kumpa hela…sihitaji hela ya mwanasiasa, ninachohitaji watu waingie katika wokovu wa kweli,” alisema Askofu Kakobe.
 
Nyalandu aliwahi kuonekana katika kanisa linaloongozwa na Nabii Josephat Mwingira Kibaha ambako aliwaomba waumini kumuunga mkono katika harakati zake za urais na Dk. Mwakyembe aliwahi kuonekana katika Kanisa la Askofu Josephat Ngwajima.
 
Hata hivyo, Mwigulu naye kwa mujibu wa Askofu Kakobe, amekuwa akijitangaza kwamba ameokoka, wokovu ambao kiongozi huyo haridhiki nao.Hakuna kiongozi yeyote kati yao  aliyepatikana juzi kuzungumzia wito huo wa Askofu Kakobe.

WAGOMBEA URAIS VIKUMBO KILA KONA YA NCHI


 mangula press

NA WAANDISHI WETU
MAKADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliotangaza nia ya kugombea urais, sasa ni wazi wanapigana vikumbo kila kona ya nchi.
Hatua hiyo inatokana na kila mtangaza nia kwa nyakati tofauti kutoa kauli nzito.
Wapo makada ambao kauli zao zinaonyesha wazi kuwa kuna mgongano ndani ya CCM, huku wengine wakitangaza nini watakifanya endapo watateuliwa kuongoza nchi.

MEMBE: SINA UNDUGU NA JK

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, amesema hana undugu na Rais Jakaya Kikwete.
Membe ambaye pia ni Mbunge wa Mtama, alikanusha undugu wake na Rais Kikwete mjini Dodoma jana wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuchukua fomu ya kuomba kuwania urais kupitia CCM.
Akijibu maswali ya waandishi wa habari, alisema hana undugu na Rais Kikwete, ingawa baadhi ya nchi ambazo amekuwa anatembelea wamekuwa wakimfananisha naye.
Alisema baadhi ya sehemu hushindwa kumtofautisha kiasi cha kumpa hadhi ya urais ikiwamo kumwomba wapige naye picha.
“Mimi siyo ndugu wa damu wa Rais Kikwete, nimechukua sura, rangi na ufupi kutoka kwa mama yangu. Kwa bahati mbaya na Rais Kikwete pia kachukua sura kutoka kwa mama yake, bado mama zetu siyo ndugu.
“Hata hivyo, kungekuwa na aibu gani kiasi cha mimi kuficha kwamba Rais Kikwete siyo ndugu yangu, ningepata hasara gani kukubali ni ndugu yangu kwa sababu kama ni madaraka tayari nilishajipatia vyeo,” alisema.
Alisema wakati mwingine huwa anaenda katika kaburi la wazazi wake kuwaomba awasamehe wale wote ambao wanazusha maneno kuhusu undugu wake na Rais Kikwete.
“Wazazi wangu walishafariki dunia, wawaache wapumzike kwa amani na waniache niendelee na njia yangu,” alisema.
Katika hatua nyingine, Membe aliahidi kutoa ushirikiano kwa waandishi wa habari pindi akiingia madarakani.
Alisema ataangalia sheria zote zinazohusu vyombo vya habari.
Membe alikuwa akijibu swali jinsi atakavyohakikisha vyombo vya habari vinafanya kazi kwa uhuru kutokana na kauli yake kwamba endapo atapata nafasi ya kuongoza nchi, atavitaka kuhakikisha vinafichua rushwa.
“Ili waandishi wa habari wafanye kazi kwa uhuru, lazima waandaliwe mazingira ya kufanya kazi vizuri, tutaziangalia sheria zote zinazoendesha vyombo vya habari.
“Lengo ni kujenga mazingira mazuri ya kuwaweka waandishi wa habari kuwa na uhuru wa kuandika chochote bila kuogopa kufungwa au kunyanyaswa,” alisema Membe.
Alirejea kauli ya Rais Barack Obama wa Marekani walipokutana katika mazungumzo ambapo alisema ‘kabla ya kufikiria kuvishitaki vyombo vya habari kwa kumshambulia, lazima kwanza ashauriane na mwanasheria wake’.
Alisema hadi sasa Rais Obama hajawahi kushitaki chombo cha habari chochote kutokana na mwanasheria huyo kukataa.
“Rais Obama aliniambia nchi inapumua kupitia waandishi wa habari, nchi inatoa dukuduku lake kupitia vyombo vya habari na mimi nitapita huko,” alisema.
Akizungumzia baadhi ya vipaumbele vyake kama akifanikiwa kuwa rais, alisema atahakikisha nchi inakuwa na uchumi wa viwanda.
Alisema jambo hilo litawezekana kutokana na ugunduzi wa gesi asilia, hivyo nchi itakuwa na nishati ya kutosha.
“Nitahakikisha Serikali yangu inazingatia utawala bora, utawala wenye nidhamu, isiyo na ufisadi na inayopiga vita rushwa na harufu yake,” alisema.

LOWASA APATA MAPOKEZI MAKUBWA GEITA, AZOA WADHAMINI 3,000

WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa jana aliingia wilayani Geita na kupokewa na umati wa wananchi ambako alidhaminiwa na zaidi ya wana CCM 3,000.
Kaimu Katibu wa Wilaya ya Geita, Killian Balindo alisema waliotakiwa kumdhamini Lowassa katika wilaya hiyo ni wanachama 45, lakini waliojitokeza wamefikia zaidi ya 3,000.
Akizungumza na wananchi waliokusanyika mbele ya ofisi ya CCM Mkoa wa Geita, Lowassa alisema japo haruhusiwi kufanya kampeni ameahidi kushughulikia matatizo ya maji, wachimbaji wadogo na mawe yaliyoisha dhahabu (magwangala).
“Hayo ya bodaboda, mamantilie kushughulikia. Nikiingia ikulu ni kuweka tu kalamu nyekundu. Kazi yangu ikikamilika nitashughulikia magwangala,” alisema Lowassa.
Kuhusu wachimbaji wadogo, alisema atawapa kipaumbele kwa kuwamilikisha maeneo ya uchimbaji na mitaji.
“Nilipokuwa mbunge miaka ya 80, niliondoa shilingi bungeni kupinga wachimbaji wadogo kunyanyasika. Nitahakikisha kila mchimbaji anapata eneo lake. Serikali inajua maeneo yote yenye madini. Halafu tutawapa fedha ili wawekezaji wakubwa wakija waweze kushindana,” alisema Lowassa.
Msafara wa Lowassa ulikuwa na magari, pikipiki na baiskeli huku ikisindikizwa na helikopta ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita, Joseph Msukuma.
Awali Lowassa jana aliingia katika Jimbo la Chato linaloshikiliwa na Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli na kupata mapokezi makubwa ya wanachama waliojitokeza kumdhamini.
Dk. Magufuli ambaye pia amechukua fomu za kugombea urais bado hajafika jimboni humo kutafuta wadhamini.
Lowassa aliingia Chato saa 8:30 mchana na kuelekea kwenye ukumbi wa ofisi ya CCM wilaya walikokuwa wamekusanyika wana CCM.
Akizungumzia udhamini huo, mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM wilayani humo, Deusdedith Katwale, alisema wanachama waliojitokeza kumdhamini wamefikia 430.
“Tunashukuru kwa kuipa kipaumbele Chato, hiyo ina maana sana siku zijazo,” alisema Katwale.
Naye Lowassa aliwashukuru wanachama hao na kurudia wito wake wa kuchagua rais aliyebobea katika chama.
“Tunakwenda kuchagua rais, tutafute mtu anayekijua chama. Angalieni historia yake na rekodi ya mambo aliyofanya,” alisema Lowassa.

AWAPONGEZA WANA CCM PEMBA

Awali akiwa kisiwani Pemba jana asubuhi, Lowassa amewasifu wanachama wa CCM kisiwani Pemba kwa kujiimarisha dhidi ya upinzani mkali wa Chama cha Wananchi (CUF).
Tangu kuanza kwa siasa za upinzani mwaka 1995, CCM imekuwa katika wakati mgumu visiwani Zanzibar, na hasa Pemba.
Akizungumza na wana CCM wilayani Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba alikokwenda kutafuta udhamini kwa ajili ya kupitishwa kugombea urais kupitia chama hicho, Lowassa alisema wana CCM kisiwani humo wanastahili pongezi.
Alisema alifika kisiwani humo mara ya mwisho mwaka 1984 na kwamba akifanikiwa kupata urais atafanya ziara ya muda mrefu kisiwani humo.
“Nilifika hapa mwaka 1984 na sijawahi kurudi tena. Lakini endapo nitafanikiwa safari yangu, nitakuja siku mbili tatu tuzungumze.
“Nawapongeza kwa jitihada zenu, licha ya upinzani mkali wa CUF bado mmeendelea kujiimarisha. Nitakuja Pemba siku mbili tatu nitakapofanikiwa ili tuzungumze,” alisema.
Lowassa pia alizungumza na wana CCM wa Wilaya ya Chakechake, Mkoa wa Kusini Pemba na kuwapongeza kwa jitihada zao za kukilinda chama chao licha ya upinzani mkali.
Lowassa alifanikiwa kupata udhamini wa wana CCM 90 katika wilaya za Wete na Micheweni Mkoa wa Kaskazini.
Akizungumzia hali ya chama hicho wilayani Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba, mmoja wa makada wa CCM, Juma Amir Juma alisema wanachokitegemea ni rehema za Mwenyezi Mungu.
“Hatusemi tutaendelea kushindwa, Mungu ni mkubwa ipo siku tutashinda. Lakini hali ni mbaya sana, kwani kama Mbunge wa CUF anapata kura zaidi ya 5,000 wa CCM anapata kura 500, wapi na wapi? Lakini hatukati tamaa,” alisema Juma.
Katibu wa CCM mkoa wa Kaskazini Pemba, Ali Haji Makame, alisema kuna wana CCM wengi walitamani kumdhamini Lowassa, lakini wameshindwa kutokana na idadi maalumu kuwekwa na kanuni za chama hicho ambayo ni wanachama 45 kwa kila wilaya.
Lowassa aliwasili Zanzibar juzi na kupokewa na umati mkubwa wa wanachama wa CCM walioandamana naye hadi katikati ya mji wa Unguja.
Kwa ujumla Lowassa amepata wadhamini 450 katika visiwa vya Unguja na Pemba.

NYALANDU ATANGAZA MAGEUZI YA KISERA

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, amesema endapo atafanikiwa kuwa Rais wa Tanzania, atahakikisha anafanya mageuzi makubwa ya kisera kwa kuweka vipaumbele vya uchumi ili kuwanufaisha wananchi wa kipato cha chini.
Alisema mageuzi hayo yataendana na mabadiliko ya mifumo ya kiutawala kwa kutengeneza uwiano wa mgawanyo wa rasilimali sawa kwa wananchi wa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wale wa Zanzibar.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumaliza ziara ya kutafuta wadhamini mjini Unguja, Zanzibar jana, Nyalandu alisema haitoshi kusikia pato la taifa linakua na uchumi wa nchi unaimarika katika ngazi ya Serikali Kuu pekee, bila ya kuwanufaisha wananchi wa kipato cha chini.
Nyalandu, alieleza kwamba endapo atapata ridhaa ya wananchi na kumchagua kuwa rais, anatarajia kuleta mabadiliko makubwa ya kimaendeleo katika nyanja za kiuchumi, kijamii na kisiasa kwa kuzingatia utu na haki ili kujenga jamii moja ya Watanzania watakaonufaika na matunda ya nchi yao.
Alisema jambo la kwanza atakapopata nafasi ya urais, atahakikisha anaondosha dhana ya watunga sera ambao ni wabunge na wawakilishi kuhakikisha wanatunga sera imara zisizokuwa na chembe ya kulinda masilahi yao, bali ziwe na upana wa kulinda masilahi ya wananchi.
Nyalandu alisema ataweka mifumo imara ya kisheria inayodhibiti viongozi wa ngazi za juu ambao ni watumishi wa umma kufanya biashara na uwekezaji pindi wanapokuwa madarakani, bali mtu afanye kazi moja ya kuwatumikia wananchi ama kufanya biashara.
“Tanzania kwa awamu hii inahitaji kuwa na rais anayefahamu tafsiri halisi ya umasikini na anayechukia jinamizi la ubaguzi na utengano baina ya wananchi wa nchi moja na kuondosha nyufa zilizopo katika Muungano, nami nimejipima nikaona uwezo huo ninao na sababu za kuiongoza nchi kwa uadilifu pia ninazo hivyo wananchi nakuombeni mfanye maamuzi ya kunichagua ili niwatumikieni,” alisema.

LUHAGA MPINA ACHUKUA FOMU, AAHIDI KUONGEZA MAPATO YA SERIKALI

MBUNGE wa Kisesa, Luhaga Mpina, naye ameungana na makada wengine wa CCM kuchukua fomu za kuwania kuteuliwa kugombea urais.
Mpina alichukua fomu hiyo mjini Dodoma jana, huku akijinasibu kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani na kudhibiti mapato yanayokusanywa.
“Nitakuja na njia mbadala ya kuhakikisha mapato ya ziada yanapatikana ili kupata fedha kwa ajili ya huduma za jamii katika sekta mbalimbali kama vile elimu na afya.
“Kwa sasa watu hawalipi kodi, mikataba mibovu inatafuna taifa, mikataba ya gesi ina kasoro kubwa, makampuni makubwa ya madini yanakwepa kodi kwa kiwango kikubwa, haya mambo ninayafahamu na nitayasimamia,” alisema.
Mpina aliahidi kuongeza mapato ya Serikali mara tatu zaidi.
“Wale waliozoea kufuja mali za umma, kuiba na kufanya ubadhirifu, nitakuja na mbadala wa kumwajibisha mwenye jukumu la kuchukua hatua.
“Watanzania wanipe dhamana, wizi huu, utoroshaji wa fedha za umma utafika mwisho, kama kuna watendaji wanaona hawawezi kuacha basi siku wakisikia naapishwa wajiondoe kabisa mana watakiona cha mtema kuni,” alisema.
Mpina aliahidi kuboresha hospitali na shule nchini ili viongozi wakiwamo wabunge waache kuzinyanyapaa hospitali zao kwa kwenda kutibiwa nje ya nchi pamoja na kutowasomesha watoto wao katika shule za Serikali.

CHIFU WA RUNGWE AMPIGIA DEBE MAKONGORO

CHIFU wa Wilaya ya Rungwe, Prince Mwaihojo amesema Makongoro Nyerere ni kiongozi mzuri ambaye ameonekana kuwa na uwezo mkubwa wa kuwaunganisha watu.
Aliyasema hayo jana wilayani Rungwe, Mbeya wakati Makongoro – mtoto wa tano wa Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alipokwenda kutafuta wadhamini watakaomdhamini kwenye nafasi ya urais.
“Nchi ilivyo sasa imekosa kiunganishi, ukiangalia wagombea wote wanajinadi kwa kufuata sera za Baba wa Taifa na hiyo inatokana na chama kupoteza dhana nzima ya kuwa chama cha wafanyakazi na wakulima, na badala yake kugeuka na kuwa chama cha walanguzi,” alisema.
Alisema Makongoro anaweza kuifanya kazi ya kurudisha amani na upendo kwa asilimia 60 kutokana na mtaji wa baba yake, huku asilimia 40 ni kutokana na uadilifu na uzoefu katika siasa.
Naye Makongoro ambaye ni Mbunge wa Afrika Mashariki, akizungumza na umati mkubwa wa wafuasi wa CCM, aliwataka wakazi wa Mkoa wa Mbeya kuhakikisha wanamuunga mkono na kumchagua kuwa rais wa Tanzania.

MANGULA : MATENDO YA WATANGAZA NIA YANAREKODIWA

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Philip Mangula, amesema vitendo vyote vinavyofanywa na wagombea wa urais ndani ya chama hicho wakati huu wanapotafuta wadhamini vinaingia katika rekodi ya chama.
Mbali na hilo, aliwataka wanachama wa chama hicho kutambua mchakato wa kugombea au kuwapata wagombea kwa nafasi ya udiwani, ubunge na uwakilishi bado haujaanza.
Mangula, alitoa kauli hiyo mjini Dodoma jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mchakato unaoendelea sasa ndani ya CCM wa kumpata mwanachama atakayegombea urais wa Jamuhuri ya Muungano na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Alisema rekodi hizo zitatumika katika mchakato wa uteuzi wa wagombea hao ambapo majina matano ndiyo yatateuliwa kwa ajili ya kwenda kupigiwa kura katika kikao cha Halmashauri Kuu (NEC).
“Vikao vya uteuzi vitafanyika kwa kutumia kanuni za uteuzi wa wagombea wa CCM katika vyombo vya dola na kanuni za viongozi na maadili za chama chetu,” alisema.
Kanuni hizo pamoja na mambo mengine zinaeleza mambo ya kuzingatia kwa wagombea na pia zinaeleza sifa za mgombea wa urais.
“Kwa mujibu wa Kanuni ya Uteuzi kifungu cha 20(5) kutangaza nia kunaruhusiwa ila ni marufuku kwa mgombea au wakala wake kufanya vitendo vinavyoonekana ni kufanya kampeni kabla ya muda,” alisema.
Alisema kifungu za 20 cha Kanuni za Uteuzi, kinasema kwamba maadili na nidhamu ya chama katika kusimamia na kutekeleza shughuli za uteuzi wa wagombea wa CCM katika vyombo vya dola lazima vizingatiwe na wale wote wanaohusika.
Mangula alisema kanuni hiyo pia inapiga marufuku wagombea kutumia ukabila, dini, rushwa, rangi, hila na eneo analotoka katika shughuli ya uchaguzi.
“Ni mwiko pia kwa mgombea kufanya kampeni za kupakana matope na ya aina nyingine yoyote dhidi ya mgombea mwingine, ni mwiko kwa mgombea aliyekabidhiwa dhamana ya usimamizi, uchujaji na uteuzi kufanya vitendo vya ukiukwaji wa kanuni,” alisema Mangula.
Alisema kanuni hizo zinaeleza sifa 13 za mgombea wa urais ambazo vikao vya uteuzi vitazingatia sifa hizo wakati wa mchujo wa wagombea.
“Baadhi ya sifa hizo, ni pamoja na awe na elimu kuanzia chuo kikuu, awe na upeo wa kudumisha na kuendeleza muungano na asiwe mwenye hulka ya udikteta,” alisema.
Alizitaja sifa nyingine kwamba awe mtetezi wa wanyonge, asiwe na tamaa ya kujitafutia umaarufu, mpenda haki, asitumie nafasi yake kujilimbikia mali, awe na uwezo wa kuilinda katiba, sheria za nchi na utawala bora, atambulike na wananchi na awe na uwezo wa kusimamia majukumu ya utendaji na uwajibikaji.
Alisema wagombea wote watapimwa kwa sifa hizo katika vikao vya mchujo.
Kwa upande wa nafasi za udiwani, ubunge na uwakilishi, Mangula alisema mchakato wa kuwapata wagombea wa nafasi hizo ndani ya chama bado haujaanza.
“Hivyo napenda kuwaambia wenye nia ya kugombea nafasi hiyo wajiepushe na vitendo vitakavyoonekana ni kufanya kampeni.
Taarifa hizi zimeandaliwa na Pendo Fundisha (Mbeya), Debora Sanja (Dodoma), Is-haka Omar (Zanzibar) na Elias Msuya (Pemba)

CHANZO: MTANZANIA

Membe Akanusha kuwa na Undugu wa Damu na Kikwete


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe. Bernard Membe amekanusha uvumi ambao umekuwa ukienezwa kuwa yeye na  Rais Jakaya Kikwete ni ndugu wa damu.
 
Membe amesema kuwa japo wanafanana kwa sura lakini hawana uhusiano wowote wa kibaiolojia.

Mhe. Membe alikanusha uvumi huo  jana Mjini Dodoma wakati akichukua fomu za kuwania urais kwa tiketi ya CCM, ambapo pamoja na mambo mengine alisema ataimarisha viwanda vidogo na vya kati.

Kada mwingine wa CCM aliyechukua fomu za kuwania urais hii jana ni Mbunge wa Kisesa Luhaga Mpina ambaye amesema vipaumbele vyake vitakuwa ni kuboresha ukusanyaji wa kodi pamoja na usimamizi thabiti wa mapato ya kodi ili taifa liondokane na utegemezi

Video ya Mwigizaji Lulu Michael Akicheza Wimbo wa Diamond yazua Gumzo Mitandaoni..Lulu Adai Diamond Ampe Kazi



Video ya muigizaji maarufu nchini, Elizabeth michael , aka lulu, imezua gumzo kwenye mitandao ya kijamii ambapo msanii huyo aliipost kwenye ukurusa wake wa instagram.
 
Video hiyo inamuonyesha msanii huyo akicheza wimbo wa mwanamuziki maarufu nchini, diamond platnums, unaojulikana kama nana /sankoro

Mwangalie  hapo  chini  anavyokata  kiuno  usafishe  macho.

Mangula Ataja Vigezo 13 Vya Mgombea Urais wa CCM


MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Philip Mangula amesema vigezo 13, vitatumika kuwachuja wanachama wa chama hicho ambao wameomba kugombea urais CCM.
 
Alisema hayo jana mjini hapa wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya CCM mjini Dodoma.
 
Aliwakumbusha watangaza nia kuwa hawaruhusiwi kutoa rushwa, kushawishi au kushawishika kuwapa rushwa wale wanaowadhamini.
 
Vigezo vyenyewe
Alitaja vigezo 13 vitakavyotumika kuwachuja wagombea kuwa ni uwezo mkubwa na uzoefu katika uongozi, uadilifu, unyenyekevu na busara.
 
Pia, kuwa na elimu ya chuo kikuu au inayolingana na hiyo, mtu mwenye upeo mkubwa wa kuimarisha na kuendeleza Muungano, umoja na amani.
 
Anatakiwa kuwa na upeo mkubwa usiotiliwa mashaka kuhusu masuala ya kimataifa, asiye na hulka ya kidikteta au mfashisti, awe tayari kulinda kanuni, sheria na utawala bora,” alisema Mangula.
 
Alitaja vigezo vingine ni kuwa mtetezi wa wanyonge na haki za binadamu na asiwe na tamaa ya kujipatia umaarufu, kuzifahamu, kuzitetea, kutekeleza sera na Ilani ya CCM, mpenda haki na ajue kupambana na dhuluma, asiwe mtu anayetumia nafasi ya uongozi kujilimbikizia mali.
 
“Awe ni mtu makini anayezingatia masuala ya uongozi,” alisema.
 
Alisema katika kipindi hiki cha mchakato wa uteuzi, kanuni zitakazotumika ni zile Kanuni za Uteuzi wa Wagombea katika Vyombo vya Dola, zilizotolewa na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM ya mwaka 2010.
 
Pia, katika kipindi hiki cha mchakato wa uteuzi wa wagombea wa CCM katika vyombo vya dola, ni sehemu ya kazi za chama ndani ya chama. Alisema vikao vya uchujaji, vitazingatia pia Kanuni za Uongozi na Maadili Toleo la mwaka 2012.
 
Alisema kipindi ambacho CCM hudhihirisha dhana ya kazi ya msingi na muhimu katika kujenga uongozi mmoja katika chama, kazi ya kutekeleza kwa dhati kanuni na demokrasia na nidhamu ndani ya chama.
 
Alisema kanuni hiyo, ndiyo inakiwezesha chama hicho kuwa cha demokrasia na papo hapo kuwa chombo cha kuongoza mapinduzi kutokana na nidhamu yake inayokipa uongozi moja katika vitendo.
 
Alisema miiko ya shughuli za uchujaji na uteuzi wa wagombea, itazingatiwa. maadili na nidhamu ya chama katika kusimamia na kutekeleza shughuli za uteuzi wa wagombea wa CCM katika vyombo vya dola, lazima vizingate na wale wote wanaohusika.
 
“Ni mwiko kwa kiongozi yeyote kwa maneno au vitendo kumpendelea au kumsaidia kupata kura nyingi mwombaji mmoja dhidi ya mwingine.”
 
Alisema Chama kinakataza mgombea kutumia au kuhusisha ukabila, dini, rushwa, rangi, hila na eneo analotoka katika shughuli yoyote ya uchaguzi.
 
Alisema ni mwiko kwa mgombea kufanya kampeni ya kupakana matope na ya aina nyingine yoyote ile dhidi ya mgombea mwingine.
 
Aidha, alisema ni mwiko kwa kiongozi yeyote au mwombaji yeyote wa nafasi ya uongozi, aliyekabidhiwa dhamana ya usimamizi, uangalizi, uchujaji na uteuzi, kufanya vitendo vya ukiukaji wa kanuni ambazo ni Katiba ya CCM, sheria, ratiba na taratibu za uteuzi.
 
Mangula alisema kwa mujibu wa kanuni za uteuzi wa wagombea wa CCM katika vyombo vya dola, kutangaza nia kunaruhusiwa kwa masharti, ikiwemo bila kuathiri haki ya mwanachama ya kutangaza nia wakati wowote nia yake ya kutaka kugombea nafasi fulani ya uongozi katika vyombo vya dola, lakini kwa kuwa nafasi hizo zimewekwa muda maalumu wa miaka mitano.
 
Alisema wakati wa kutafuta wadhamini 450, kila anachokifanya mwana CCM anayetafuta wadhamini, kitaingia katika kumbukumbu za tathmini ya mgombea mtarajiwa.
 
Pia, alisema kamati za maadili za wilaya, zikutane mara baada ya wagombea watarajiwa kujaza majina ya wadhamini wilayani. Alisema mpaka sasa wagombea urais waliojiandikisha wamefikia 22 na wengine bado wanakwenda.

Kikwete aagwa kifalme Uholanzi


RAIS Jakaya Kikwete jana aliagwa kifalme katika ziara yake ya kikazi nchini Uholanzi, huku akielezea kwa kiasi kikubwa mafanikio ya utawala wake katika miaka kumi aliyokaa madarakani.
 
Kikwete aliyewasili juzi usiku mjini hapa akitokea katika ziara yake ya nchi za Finland, Denmark na Sweden, alipokelewa na kupewa heshima zote za kifalme, ikiwa ni pamoja na kupewa makazi katika kasri la Mfalme, akiwa kiongozi wa tatu wa Afrika kupewa hadhi hiyo nchini hapa.
 
Wengine waliowahi kupewa hadhi hiyo ni Rais wa Kwanza mzalendo wa Afrika Kusini, Hayati Nelson Mandela na Askofu Mkuu mstaafu wa mji wa Cape Town, Afrika Kusini na mshindi wa tuzo la Nobel Desmond, Desmond Tutu.
 
Rais Kikwete baada ya kukutana na Balozi wa Tanzania nchini hapa, Wilson Masilingi na maofisa wake, alianza kazi kwa vikao na wawekezaji, ikiwemo kampuni ya Shell, alikutana pia na kuzungumza na Mfalme Willem Alexander na baadaye alikutana na Rais wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) katika makao makuu ya mahakama hiyo, Silvia Alejandra Fernandes de Gurmendi.
 
Jioni alikutana na mabalozi wa Afrika, wanaowakilisha nchi zao nchini Uholanzi, ambapo alitumia fursa hiyo kuwaaga, akiwataka wampe ushirikiano rais ajaye, lakini pia alielezea mafanikio makubwa aliyoyapata katika utawala wake.
 
Alisema ingawa anaondoka madarakani baada ya utawala wake wa miaka kumi, anaamini Tanzania itapata kiongozi mzuri licha ya mchuano mkubwa unaoendelea, akisema alikuwa na taarifa kuwapo kwa makada 34 wa CCM wanaowania kutaka kumrithi.
 
“Ninamaliza muda wangu, hivyo napita kuaga marafiki na nchi wahisani. Tuna historia ndefu na Uholanzi, tangu enzi za Nyerere (Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere). Babu wa huyu Mfalme (Willem) alikuwa na shamba Tanzania, lakini pia baba yake amesoma Tanzania. Hawa ni ndugu zetu,” alisema na kuishukuru Serikali ya kifalme ya Uholanzi kwa kumpa mwaliko rasmi wa kikazi.
 
Hata hivyo, Rais Kikwete alipokuwa akizungumzia kasi ya kuondoa umasikini, alisema bado juhudi za kuondoa umasikini zinahitajika na zitafanikiwa kwa kuelekeza nguvu kwenye kilimo, ambacho ndicho kinachoajiri na kutegemewa na Watanzania wengi zaidi hasa wanaoishi vijijini.
 
Rais Kikwete pia amefanya mazungumzo na Spika wa Bunge la Sweden, Urban Ahlin, pamoja na viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa nchini humo na kushukuru kwa misaada ya maendeleo kwa takribani miaka 50Nsasa.
 
Mabalozi hao wa Afrika wamempongeza Rais Kikwete kwa kufanya ziara ya shukrani na kuwaaga nchi rafiki na wahisani, kwani ni mara chache kwa viongozi wengi wa Kiafrika kuaga na kuondoka madarakani.
 
Kwa upande wa elimu, alisema wakati akiingia madarakani mwaka 2005, alikuta Tanzania, yenye watu wengi zaidi katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), iko nyuma ikilinganishwa na Kenya na Uganda, kwa idadi ya wanafunzi waliokuwa wakisoma shule za sekondari na vyuo.
 
Kwa upande wa elimu ya juu, Rais Kikwete alisema vyuo vikuu vimeongezeka kutoka 26 mwaka 2005 hadi kufikia 52 na idadi ya wanafunzi walio katika vyuo vikuu ilitoka 40,719 hadi kufikia 200,956.
 
Hata bajeti ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu imeongezeka kutoka Sh bilioni 56.1 hadi Sh bilioni 345 mwaka 2014. Rais Kikwete anatarajiwa kurejea nyumbani leo.

TARIME: Mwenyekiti CHADEMA mbaroni Akidaiwa kuiba Mlingoti wa bendera ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)


MWENYEKITI wa Chama cha Demkrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika Kijiji cha Sokini mji mdogo wa Sirari wilayani Tarime, Denisoni Makanya (44),  amepandishwa kizimbani mbele ya Hakimu, Gibogo Wenje, akidaiwa kuiba mlingoti wa bendera ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wenye thamani ya Sh 80,000.

Mwendesha Mashtaka wa Oolisi, George Lutonja, alidai  mshtakiwa  alitenda kosa hilo usiku Mei 29, mwaka huu.

Mshitakiwa alikana shitaka na yuko nje kwa dhamana hadi Agosti 4 mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena.

CHADEMA Wamtaka Mwandosya Ajiunge UKAWA


NAIBU Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Zanzibar, Salim Mwalim, amesema Profesa Mark Mwandosya, ajiunge na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ili awe mshauri kuliko kuendelea kuwepo CCM.
 
Akizungumza jana kwenye mkutano wa hadhara aliofanya katika Jimbo la Rungwe Mashariki linaloongozwa na Mwandosya, alisema CCM imekosa mwelekeo hivyo msomi kama Mwandosya hatakiwi kuwa katika chama hicho.

Alisema japo mbunge huyo alisema hatagombea tena jimbo hilo la Rungwe Mashariki, kinachotakiwa ni kukihama chama hicho na kujiunga na Ukawa ili awe mshauri wa Umoja huo.

“Mwandosya ni msomi mkubwa sana hivyo kutokana na elimu yake aliyonayo, anatakiwa kutoka CCM na kujiunga na Ukawa ili awe mshauri wetu na sio kuendelea kubaki na CCM,” alisema Mwalim.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Mbeya, Joseph China, alisema wananchi wanatakiwa kujiandikisha ili kuweza kupata haki yao ya msingi ya kupiga kura.

China alisema njia pekee ya kuweza kuishinda CCM ni wananchi kujiandikisha kwa wingi na kuhudhuria siku ya kupiga kura.

Alisema katika kata hiyo ya Kandete kumekuwepo na tatizo la kutokuwepo kwa diwani hivyo michango imekuwa ikichangishwa kiholela na watendaji wa vijiji na kata bila kujua matumizi ya hizo fedha.

Mwenyekiti CCM atamba kumng’oa Mchungaji Msigwa


MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa, Jesca Msambatavangu (39) amesema anayo nia na uwezo wa kumuangusha katika Uchaguzi Mkuu wa baadaye mwaka huu, Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini anayemaliza muda wake Mchungaji Peter Msigwa (Chadema).
 
Msambatavangu aliyasema hayo jana ikiwa ni wiki moja tangu Makamu Mwenyekiti wa CCM (Tanzania Bara), Phillip Mangula afike mjini Iringa kumaliza mgogoro wa kisiasa uliosababisha baadhi ya wanachama wa chama hicho jimbo la Iringa Mjini wafukuzwe uanachama huku Mwenyekiti huyo wa Mkoa akipewa onyo kali.
 
Machi mwaka huu, vikao vya chama hicho ngazi ya wilaya na mkoa viliwafukuza uanachama Shukuru Luhambati, Clara Shirima na Hosea Kaberege huku Msambatavangu akipewa onyo kali lililodaiwa kumuondolea sifa ya kugombea nafasi yoyote ya uongozi kupitia chama hicho na kuzusha hofu kubwa ya mpasuko ndani yake.
 
Akizungumzia rufaa walizokata na maamuzi aliyokuja nayo Mangula na kuyawasilisha katika kikao cha Halmashauri ya Wilaya ya CCM Manispaa ya Iringa, Msambatavangu alisema; “CCM kwa kutumia kanuni na Katiba yake imepitia rufaa zetu, ikajifunza kitu na kutumia busara yake kutupilia mbali adhabu hizo ili kulinda maslahi mapana ya chama hiki.
 
“Tunajiandaa kushiriki Uchaguzi Mkuu ujao tukiwa wamoja na niwahakikishieni mimi ni mmoja kati ya wana CCM wenye nia ya kugombea ubunge katika jimbo la Iringa Mjini.
 
 “Sijajua makada gani wengine watajitokeza; wenye uwezo wa kusema ni nani ni CCM wenyewe na wananchi wa jimbo hili.
 
"Kwa mimi kutangaza nia na kujitoa nina hakika na ninafahamu nina uwezo wa kupeperusha bendera na kurudi na ushindi, sitakiletea aibu Chama Cha Mapinduzi pamoja na kwamba nipo tayari kumuunga mkono mgombea atakayeteuliwa,” alisema.
 
Alitaja kipaumbele chake cha kwanza endapo CCM itampa ridhaa ya kuwania nafasi hiyo kuwa ni elimu na katika sekta hiyo atahakikisha miundombinu yake inaboreshwa ili iwe ya kisasa.
 
“Nitahakikisha kunakuwepo na ustawi wa elimu, shule bora zenye nidhamu ili Iringa iingie kwenye ushindani wa juu kitaifa.
 
"Tutajiimarisha kujenga mabweni katika shule zetu ili watoto hasa wa kike wawe jirani na shule,” alisema.
 
 Alisema katika kuboresha ustawi wa sekta hiyo atahakikisha vijana wengi wa shule za msingi na sekondari za mjini Iringa wananufaika kwa uwepo wa vyuo vikuu vinne vya mjini hapa kwa kutengeneza ushirikiano utakaosaidia vijana wengi kujiunga na elimu ya juu.

MTOTO WA WAKIKE WA MHESHIMIWA  MACELA AGOMBEA URAIS CCM 


MKURUGENZI Mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti Magonjwa ya Binadamu Dk Mwele Malecela mtoto wa Makamu wa zamani wa CCM John Malecela ni miongoni mwa wana CCM ambao wamejitosa kugombea urais kupitia CCM.
 
Dk Mwele kesho amepangiwa na CCM kuchukua fomu za kuomba kugombea urais. Ratiba ya CCM iliyotolewa jana Makao Makuu ya chama hicho mjini hapa inaonesha kuwa licha ya Dk Mwele, mwingine ambaye atachukua fomu hiyo kesho ni Nicholaus Mtenda ambaye pia amejitokeza kuomba kugombea urais kupitia CCM.
 
Dk Mwele katika maisha yake mengi kwa zaidi ya miaka 20 amekuwa mtumishi katika Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) ambako alianza kazi akiwa kijana na akapanda hadi kuwa mtafiti mkuu na baadaye akateuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu.
 
Licha ya kukulia katika familia ya mwanasiasa maarufu nchini, lakini Dk Mwele hajawahi kujitokeza hadharani kushiriki kwenye masuala ya siasa. Kama akichukua fomu hiyo kesho, atakuwa ni mwanamke wa pili kuomba kuteuliwa na CCM kugombea urais kumrithi Rais Jakaya Kikwete.
 
Mwanamke mwingine ni Balozi Amina Salum Ali wa Zanzibar. Jana Waziri wa Malisili na Utalii, Lazaro Nyalandu na wanachama wengine wawili wa CCM walichukua fomu za kuwania urais. Nyalandu alikuwa wa kwanza kufika katika ofisi za CCM kuchukua fomu akiwa amefuatana na familia yake na wafuasi wake kadhaa.
 
Baadaye alifuatiwa na mwanachama mwingine wa CCM, Peter Nyalali, ambaye ni Ofisa mstaafu wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) na kufuatiwa na mwanachama wa chama hicho kutoka wilaya ya Muleba, Leonce Mulenda.
 
Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu, Nyalandu alisema hatua hiyo ni ishara ya yeye kuanza safari ya ndoto yake ya kuchukua majukumu ya urais kwa lengo la maendeleo ya nchi hii chini ya misingi aliyoianzisha Baba wa Taifa, hayati, Mwalimu Julius Nyerere.
 
Kwa upande wa Nyalali, alisema atalenga katika kuimarisha uchumi kwa kuzingatia Katiba ya nchi na ya chama na kuleta mabadiliko chanya ndani ya CCM na kwa Watanzania ambao wamekuwa hawanufaiki na fursa zilizopo nchini.
 
Kwa upande wa Leonce Mulenda, alisema atahakikisha Katiba ya Chama na maamuzi yanatekelezwa kama inavyotakiwa na kuwa chama imara kitakachosaidia serikali isiwe legelege.

Membe Atangaza Nia ya Kugombea Urais ......Aahid kuipeleka Nchi kwenye Uchumi wa Viwanda


WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, ametangaza rasmi kuwania urais wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM}, huku akitamba ataipeleka nchi katika uchumi wa viwanda unaobebwa na kilimo na kuahidi kujenga serikali ya waadilifu.
 
Licha ya Membe, wana CCM wengine wawili jana walitangaza pia kugombea urais nao ni Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia Januari Makamba pamoja na Mbunge wa Nzega Dk Hamis Kigwangala.
 
Membe alifichua kuwa alienda kuomba kwenye kaburi la Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere ili kupata ridhaa na kusisitiza kuwa urais si suala la kukurupuka na kwamba atahakikisha anasimamia utawala bora, huku akiongoza mapambano dhidi ya rushwa na kwa kubadili kipengele cha mtu atakayetoa rushwa na kutoa taarifa awe huru.
 
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya CCM Mkoa wa Lindi jana, Waziri Membe alisema kabla ya kuchukua uamuzi wa kufikiria urais alijipima na kuona anatosha kwa nafasi hiyo, pia baada ya kuwaangalia wagombea wenzake wote anaamini yeye ndiye mwenye sifa za kustahili kuwa Rais wa Awamu ya Tano ya Tanzania.
 
Aliwaambia wananchi kwenye mkutano huo kuwa uadilifu wake ni wa kuzaliwa, uwajibikaji usio wa kawaida na ndiyo sababu kila uchaguzi wananchi wa Jimbo lake la Mtama wamekuwa wakimchagua kwa idadi kubwa ya kura.
 
“Mwaka 2010 nilishinda ubunge kwa asilimia 86 ya kura, nimekuwa mbunge tangu mwaka 2000 na kila uchaguzi idadi ya kura zangu zinaongezeka…Niwaahidi jimbo la Mtama litabaki katika mikono salama, hakuna mgombea wa Ukiwa wala Ukawa atakayeshinda, ila milele litabaki kwa CCM.
 
"Nina uzoefu mkubwa ndani ya chama, nimesoma siasa darasani mwalimu wangu akiwa Mzee Mangula (Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula}, mwaka 2007-2012 nimekuwa Katibu wa Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa CCM, Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM kuanzia mwaka 2007 hadi 20012, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM kuanzia mwaka 2012 hadi 2017 hizo ni katika chama."
 
Pia alisema upande wa serikalini ana uzoefu mkubwa baada ya kuwa Ofisa usalama wa Taifa kuanzia mwaka 1978, Ofisa Ubalozi,Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Naibu Waziri wa Nishati, Waziri wa Mambo ya Nje kuanzia Desemba mwaka 2006 hadi sasa.
 
Akielezea uzzoefu wake alitaja nyadhifa mbalimbali alizoshika zikihusisha kimataifa ikiwemo ya sasa ya Mwenyekiti wa Baraza la Kazi Jumuiya ya Madola kwamba zinamfanya aamini anaweza kurithi viatu vya Rais Jakaya Kikwete.
 
Kwa nini anautaka urais? Akizungumza kilichomsukuma kuwania urais, Membe alisema alitaafakari kwa kina uamuzi huo kwani kazi hiyo si jambo jepesi unashika hatima ya Watanzania na masuala mengine kadha wa kadhaa.
 
Nimejiangalia mwenyewe, nikaangalia wenzangu wote, nikasema nikimpata mwenye sifa hizi ningeacha… nimepitia mmojammoja nimeona hakuna kama Membe. Urais si suala la kukurupuka. Unaweza ukakurupuka kazi nyingine, lakini urais muachieni Membe.
 
Kuomba kaburini kwa Nyerere 
Alifichua kuwa Machi mwaka huu alialikwa na Chifu wa Wazanaki kijijini Butiama kwa hayati Mwalimu Nyerere kulikokuwa na sherehe ya wazanaki, ambapo alienda katika kaburi la Nyerere aliyekuwa Rais wa Kwanza wa Tanganyika na baadaye Tanzania na kusali na kuzungumza kuhusu nia yake ya kuomba urais.
 
“Nilisali pale, nikamwambia Mwalimu unanijua vizuri Membe, nataka kutia nia ya urais, nataka kuvaa viatu vyako alivyovaa Mzee Mwinyi, Mkapa na Kikwete. Nilisema nilienda Ikulu nimevikuta viatu bado vipo vizima, kama utaona sitoshi au ni oversize nipitishiwe mbali kikombe hiki.",alisema.
 
Alisema timu yake iliyokuwa inazunguka nchi nzima ilimletea taarifa kwamba anafaa kwa urais na kujiuliza pengine Nyerere amejibu kwa njia hiyo na kusisitiza kuwa ana uhakika Nyerere atafurahi akishinda.
 
Pia aliahidia hatakubali mtu awadhihaki marais wastaafu Mkapa, Mwinyi na Kikwete na kumsifu Kikwete kwamba amefanya kazi kubwa sana katika suala la kuinua elimu nchini.
 
Kigwangala wazee watupishe
Mbunge wa jimbo la Nzega mkoani Tabora Dk,Hamisi Kigwangalla amesema kwamba huu ni wakati wa vijana kuliongoza taifa hili na ameahidi kuwa iwapo atapitishwa na chama chake ana kashinda atahakikisha kila Mtanzania anakuwa na bima ya afya.
 
Alisema ni wakati wa watu ambao hawajaingia serikali kushika wadhifa wa urasi kwani uzoefu umeonesha kuwa marais ambao huwa wameshafanya kazi serikalini huwa wanaharibiwa na mfumo na hivyo kutofanya vizuri. "Umefika wakati wa kuwa na rais ambaye hajafanya kazi serikalini, wazee watupishe sasa ni wakati wa sisi vijana," alisema Dk Kigwangala.
 
Pia alisema hakuna uzoefu katika nafasi ya urais bali wenye uzoefu huo wapo wanne ambao tayari wamekwisha pitia nafasi hiyo na kukaa kwenye jengo la Ikulu ambao aliwataja kuwa Baba wa Taifa Mwl,Julius Nyerere,Ali Hassan Mwinyi, Benjamini Mkapa na Rais Jakaya kikwete.
 
Akihutubia wananchi wa Jimbo la Nzega mjini Nzega, Dk Kigwangalla alisema wengine wote waliobaki sio wazoefu wa kufanya kazi Ikulu bali ni wazoefu wa shughuli nyingine.
 
Alisema kuwa wote wanaowania nafasi hiyo akiwepo yeye mwenyewe wanauzoefu tofauti tofauti katika masuala mbalimbali, huku akiwabeza wenye uzoefu wa ubadhilifu wa mali za umma ikiwemo Rushwa na ufisadi hali ambayo akiteuliwa na kushinda nafasi hiyo atapambana navyo.
 
Dk Kigwangalla katika vipaumbele vyake iwapo atateuliwa na kushinda nafasi hiyo, alisema atahakikisha ndani ya mwaka mmoja, Watanzania wote watakuwa na Bima ya Afya watakao lipiwa na Serikali pamoja na kuwa jari watumishi wa Idara ya Afya na Ustawi wa Jamii ili waweze kutoa huduma bora ya matibabu kwa wananchi.
 
"Iwapo Watanzania hawatapata huduma bora ya Afya kama kiongozi wa Nchi mwisho wa siku utaongoza Taifa la wagonjwa na hivyo kudhoofisha nguvu kazi ya Taifa hali ambayo inayoweza kusababisha kushuka kwa uchumi wa Nchi’’alisema dkt Kigwangalla.
 
Alisema katika kuboresha suala la Elimu kwa watanzania kama atashika nafasi hiyo anatamanai Elimu yote kuanzia Awari,msingi na sekondari bure kwa kuwa atahakikisha nchi inakuwa na uchumi imara kwa kupunguza matumizi ya serikali,safari,posho na ukubwa serikali.
 
Akizungumzia suala la kukuza uchumi kwa wakulima,wafanya Biashara wadogowadogo na viwanda anatamani kuanzisha mfuko wa kukopesha wananchi kwa kuwekeza Bill 500 kwa mwaka pamoja na kuboresha kitengo cha ustawi wa jamii katika Halmashauri kwa ajili ya kwa Elimisha,kuwaunganisha kwenye vikundi vya kudhaminiana na kuratibu shughugili zao.
 
Alisema kwa kufanya hivyo Serikali itakuwa inauwezo wa kuzalisha ajira rasimi laki mbili kila mwaka na ajira zisizo rasimi milioni kumi kila mwaka na uchumi huu utamgusa kila mtu kila mwaka. 
 
Januari Makamba kuunda serikali ndogo 
Kwa upande wake Januari Makamba amesema endapo atapewa ridhaa ya kugombea na kuteuliwa kuwa rais ataunda serikali ndogo yenye mawaziri wasiozidi 18 ambayo utendaji wake utakuwa wa kutukuka.
 
Pia alisema atatoa Sh milioni 50 kila kijiji hapa nchini ili kupambana na umasikini wa wananchi uliokithiri. Alisema akiwa rais atajikita zaidi katika kukuza uchumi wa mtu mmoja moja, kuwezesha upatikanaji wa huduma bora za Jamii ikiwemo afya, elimu, na umeme.
 
Vipaumbele vingine vya serikali yake vitakuwa ni pamoja na kusimamia utawala bora na sheria, kusimamia uchumi na kuziwezesha taasisi za fedha kukuza uchumi kwa kuunda baraza la uchumi la taifa. Kipaumbele kingine ni kulinda amani, umoja na usalama wa taifa kwa kuwashirikisha wananchi na viongozi wa dini.
 
Vilevile atajikita katika kudumisha muungano uliopo na uweze kuwa na manufaa zaidi na kudumu kwa kipindi kirefu. 
 
Katika suala la Kupambana na ukosefu wa ajira, Makamba alisema ataanzisha mfumo maalum wa kuwaunganisha vijana waunde vikundi na kuwapatia mikopo ili waweze kujiajiri na kuondokana na umasikini pamoja na kuwa walipa kodi.
 
Aidha aliahidi endapo atateuliwa kuiongoza nchi, atajenga viwanda 11 vya nguo vitakavyozalisha ajira zaidi 100,000 na kipaumbele kwa watakaoajiriwa ni wanawake na vijana.
 
Katika tasnia ya michezo, alisema atarasimisha kazi zote za wasanii ili waweze kufaidika na kazi zao pamoja na taifa kunufaika kwa kukusanya kodi.
 
Kuhusiana na kukabiliana na migogoro ya ardhi, alisema ataanzisha upimaji wa ardhi kwa kutumia mitambo ya setilaiti na kugawa hati kwa Wakulima, wafugaji na wananchi zenye picha za mipaka Yao ili kuondoa utata na migogoro.
 
Katika huduma ya afya, Makamba alisema atahakikisha wananchi wote wanapata bima ya afya pamoja na kuboresha upatikanaji wa huduma hiyo Karibu Na maeneo ya wananchi.
 
POSTED BY.RASHID HAMZA

MWANZA: Meya Matata ajiengua Chadema, Arejea CCM


HATIMAYE Meya wa Halmashauri ya Ilemela jijini Mwanza, Henry Matata, amejiengua ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kuhamia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Uamuzi aliufanya juzi katika mkutano wa hadhara uliofanyika eneo la Minazi Mitatu Kata ya Kitangiri Manispaa ya Ilemela ambako alikabidhi kadi yake ya Chadema kwa Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza, Miraji Mtaturu na kupewa ya CCM.

Akizungumza baada ya kurudisha kadi ya Chadema, Matata alisema kabla ya kujiunga na upinzani alikuwa ndani ya chama hicho tangu utotoni  lakini baada ya CCM kumfanyia mizengwe kwa kuweka jina lake nafasi ya nne katika kura za maoni kwenye uchaguzi wa  mwaka 2010, aliamua alikimbilia Chadema.
 
Alisema alipokimbilia Chadema alipokelewa kwa shangwe kwa sababu alikuwa anakubalika kwa wananchi na kumpa nafasi ya kuwania udiwani na kushinda Kata ya Kitangiri.

Alisema  baada ya kuanza kutekeleza majukumu ya udiwani  ndani ya upinzani alijikita kutekeleza ilani ya CCM ndipo alipoanza kuchukiwa.

“Mimi damu yangu ilikuwa CCM ingawa nilikuwa Chadema, baada ya kushinda udiwani nikaanza kupigania nafasi ya umeya kwa bahati nzuri nikapata.

“Sasa ukishakuwa meya lazima utekeleze ilani ya CCM kwa sababu ndiyo chama tawala… wenzangu wakaanza kunichukia na kuniundia zengwe kama ilivyokuwa awali CCM.

 “Ikafika wakati nikavuliwa uanachama nikabaki diwani wa mahakama- lakini sikupoteza chochote kwa sababu  stahili zangu zote nilipata,” alisema.

MWANZA : Takukuru yawaburuza kortini vigogo watatu wa Serikali

R D PRODUCTION

TAASISI ya Kupambana na Kudhibiti Rushwa nchini (TAKUKURU) imewaburuza mahakamani vigogo watatu  wa Serikali  kwa makosa mawili ya matumizi mabaya ya madaraka na   kutumia nyaraka mbalimbali kumtapeli mwajiri wao.
 
Vigogo hao ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala Mkoa wa Shinyanga, Patrick Karangwa (45), Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu Mkoa wa Mwanza, Ntinika Paul (51) na Mhasibu Mkuu wa Wilaya ya Magu, Mathayo Masuka.
 
Walifikishwa wiki iliyopita katika Mahakama ya Wilaya ya Nyamagana Mkoa wa Mwanza,  mbele ya Hakimu Mkuu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Janeth Masesa.
 
Ilidaiwa kuwa watuhumiwa hao walitenda makosa hayo mwaka 2009 wakati wakiwa wafanyakazi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza.
 
Ilielezwa kuwa wakati wakitenda makosa hayo, Karangwa alikuwa Mchumi Mkuu Jiji la Mwanza, Paul   alikuwa mweka hazina mkuu  wa jiji hilo wakati  Masuka alikuwa mkaguzi wa ndani wa jiji la Mwanza.
 
Watuhumiwa hao walikana mashtaka hayo na wapo nje kwa dhamana na  kesi hiyo inatarajiwa kutajwa tena Juni 11 mwaka huu.
 
Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mwanza, Kasomambuto Mbengwa, alithibitisha taasisi hiyo kuwakifikisha vigogo hao mahakamni.
Mpekuzi blog
Home » Magazeti » June 08 2015.. Hizi ndio stori kubwa za #Magazeti 26 ya Tanzania leo>> Udaku,Michezo, Dini na Hardnews

January Makamba - Tanzania Mpya

June 08 2015.. Hizi ndio stori kubwa za #Magazeti 26 ya Tanzania leo>> Udaku,Michezo, Dini na Hardnews

PAPERS PB
Good morning mtu wa nguvu.. leo JUNE 08 2015 nimekusogezea tena hii post ya Magazeti ambapo utaona story zote zenye uzito Magazetini kuanzia Udaku, Hardnews, Dini na Michezo.
Hapa ninayo Magazeti haya 26 na stori zake kubwakubwa kwenye kurasa za mwanzo na mwisho.
DSC03425
DSC03426
DSC03427
DSC03428
DSC03429
DSC03430
DSC03431
DSC03432
DSC03433
DSC03434
DSC03435
DSC03436
DSC03437
DSC03438
DSC03439
DSC03440
DSC03441
DSC03442
DSC03443
DSC03444
DSC03445
DSC03446
DSC03447
DSC03448
DSC03450
DSC03451
DSC03452
DSC03453
DSC03454
DSC03455
DSC03456
DSC03457
DSC03458
DSC03459
DSC03460
DSC03461
DSC03462
DSC03463
DSC03464
DSC03465
DSC03466
DSC03467
DSC03468
DSC03469
DSC03470
DSC03471
DSC03472
DSC03473
DSC03474
DSC03475
DSC03476

DSC03478

Unahitaji chochote ninachokipata kisikupite? jiunge na mimi kwenye Twitter, Facebook na Instagram kwa kubonyeza hapa >>> Twitter Insta FB na nitakua nikikutumia kila ninachokipata pia usisahau kusubscribe YouTube kwa kubonyeza hapa >>>Videos ili kila video ya AyoTV ikufikie.
Tags :
Previous post link
Next post link