Nape: CCM itashinda tu hata kwa goli la mkono
CCM imesema kuwa itahakikisha inarudi Ikulu hata “kwa bao la mkono” wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 25.
Katibu
wa itikadi na uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye alisema hayo katika
mkutano wa hadhara uliofanyika jana kwenye viwanja vya Nyehunge wilayani
hapa.
Neno
“bao la mkono” hutumiwa kama goli lililofungwa kwa kuupiga mpira kwa
mkono kinyume cha taratibu za mpira, lakini hukubaliwa kwa kuwa mwamuzi
anakuwa hajaona kitendo hicho.
“Rangi
inayoenda Ikulu ni hii (anaonyesha shati lake la kijani ambayo hutumiwa
na chama hicho). Tuna uhakika na ushindi wa Rais. Kwa namna yoyote ile,
CCM itarudi Ikulu hata kama ni kwa bao la mkono... bao ni bao tu ili
mradi refa hajaona,” alisema Nape.
Nape,
aliye kwenye ziara ya katibu mkuu wa CCM, aliwataka wananchi wa
Sengerema kusubiri ushindi wa chama hicho na kuwakumbusha kuwa wanapaswa
kuiweka CCM kuanzia udiwani mpaka ubunge kwa nafasi ya urais tayari
kuna uhakika.
Katika
mkutano huo, Nape alisema ana uhakika CCM itashinda baada ya kushuhudia
mwitikio wa Watanzania tangu alipoanza kuongozana na Kinana katika
ziara zake za kuizunguka nchi na kuzungumza na wananchi pamoja na
kusikiliza kero zao.
Amebainisha
kuwa amejifunza na kujiridhisha kuwa chama chake bado kinapendwa
miongoni mwa wapigakura waliofikiwa tofauti na vyama vya upinzani.
“Tumefika
maeneo mengi ambayo upinzani haujafika. Huko tuna hazina kubwa ya
wanachama. Hakuna namna Ukawa wanaweza kuingia Ikulu mwaka huu,”
alisisitiza.
Wapinzani waja juu
Kauli
hiyo ya Nape ilipingwa na viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani
waliosema kuwa mtendaji huyo anamaanisha kuwa CCM itaiba kura.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa hakutaka kabisa kuzungumzia kauli ya Nape zaidi ya kusema watakutana Oktoba.
“Kwa
bahati mbaya kauli za Nape siwezi kuzijibu. Kauli za Nape zichukue kama
zilivyo, ingekuwa ni (katibu mkuu wa CCM, Abdulraham) Kinana,
ningemjibu lakini ajue kuwa tutakutana Oktoba,” alisema Dk Slaa alipoulizwa na Mwananchi kuhusu suala hilo.
Naibu
mkurugenzi wa habari wa CUF, Abdul Kambaya alisema kauli ya Nape
inamaanisha kuwa CCM itaiba kura kwani kwa kawaida bao la mkono ni bao
haramu.
“Kauli
hiyo inaonyesha dhahiri kuwa wataiba kura na kwa sababu katiba yetu ni
mbovu matokeo yake yatatangazwa kama yalivyo… hiyo ndiyo maana ya bao la
mkono,” alisema.
Kambaya
alisema hata hivyo CCM isijiaminishe kwa lolote kwani hivi sasa
wananchi wamebadilika kimtazamo kutokana na matatizo mengi yanayoiandama
nchi kama vile afya, elimu duni na migogoro ya ardhi.
“Lakini
CCM wajue kuwa kutatokea machafuko makubwa iwapo wamejipanga kuingia
Ikulu kwa njia hiyo ya bao la mkono. Kauli ya Nape ni ya kidikteta na
inaonyesha dhahiri kuwa wamejikita kwenye utawala wa mabavu,” alisema.
Kadhalika
Kambaya alisema CUF imeshajipanga na kuhakikisha inaziba mianya yoyote
ya wizi wa kura kuanzia kwenye Daftari la Wapigakura hadi katika ujanja
wa kuwapigisha kura marehemu, askari na wanajeshi kama inavyodaiwa
kufanyika Zanzibar.
Katibu
mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe alisema Nape anatoa maneno ya
kuvutia kwake kama njia ya kuwakatisha tamaa wapinzani na wanachama,
hata hivyo alimuonya kuwa siasa za sasa hazitabiriki kwa njia hiyo.
“Lakini
ajue kuwa mambo yanabadilika. Anaweza kushangaa mambo yakawa mengine,
sasa hivi wananchi wana mwamko mkubwa na wanabadilika,” alisema.
Alisema
CCM haina haja ya kujitapa kwa sasa wakati bado haijapata mgombea kwani
huenda wakapata ambaye wananchi hawatamuunga mkono hata kidogo.
“Bado
CCM wana makundi jambo ambalo kwao ni udhaifu. Lakini pia lazima wajue
kuwa wakati wa mchujo utakapofika, wale watakaokatwa hawatafurahia
kuachwa na hapo kuna sababu za wapinzani kushinda,”alisema.
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema wakati Nape anabishana kwenye majukwaa, NCCR inaendelea kupiga kazi.
“Badala ya kujadili hoja za msingi zenye manufaa kwa wananchi yeye anajadili CCM kupiga bao?” alihoji Mbatia.
Akijibu
hoja ya Nape, Naibu Katibu Mkuu wa TLP, Nancy Mrikaria alisema kauli ya
kada huyo imekaa kisiasa na si kiuhalisia kwani ni kawaida kwa chama
cha siasa kujiaminisha kuwa kitashika dola.
“Unajua
chama chochote hata kiwe kidogo lazima kikiri kuwa kitashika dola ili
mradi ilani yao inakubalika na unakubaliwa na wananchi kwa sababu chama
chochote nia yake ni kuingia ikulu,” alisema.
Alisema
hata vyama vidogo kama TLP hukiri ushindi kwa kusema kuwa vinataka
kuingia ikulu kwa sababu chama hakiwezi kukiri mbele ya wananchi kuwa
hakitashinda.