Asimulia mkasa mzima wa vifo vya mumewe na watoto wake Kawe
Mama
wa familia iliyouawa katika ajali ya kifusi iliyoua watu watano jijini
Dar es Salaam wakiwemo baba na watoto wake wawili na binti wao wa kazi,
Gaudensia Ephraim alinusurika baada ya yeye kudamkia katika biashara
yake ya kukaanga maandazi.
Mume
wa Gaudensia, Ephraim Manguli (47), watoto wake wawili Danford (5) na
Fredy Ephraim (2) pamoja na binti wao wa kazi aliyetambulika kwa jina
moja la Mariam, walikufa baada ya nyumba walimokuwa wakiishi kufunikwa
na kifusi kwenye eneo la Kawe katika Manispaa ya Kinondoni, Dar es
Salaam juzi asubuhi.
Baba
mzazi wa Ephraim, Mzee Philemon Manguli alisema kama isingekuwa
biashara hiyo na mkwewe angefariki katika ajali hiyo iliyotokea alfajiri
ya Jumatano Aprili 6, mwaka huu na kusababisha vifo hivyo.
Alisema
Gaudensia hufanya biashara ya kukaanga maandazi hivyo alidamka alfajiri
kwenda katika biashara yake na wakati yupo huko alitaarifiwa kutokea
kwa ajali hiyo na alipofika nyumbani akakuta nyumba imeanguka na familia
yake imefukiwa.
“Mkwe
wangu yeye hufanya biashara ya kukaanga maandazi, na wakati ajali
inatokea tayari alikuwa katika biashara yake mtaa wa pili na
alipoarifiwa na kurudi nyumbani ndio akakuta ajali hiyo ambayo iliua
mumewe, watoto wawe wawili, binti yake wa kazi pamoja na mjukuu wa
mwenye nyumba walimokuwa wakiishi,” alisema.
Akizungumza
kwa niaba ya mkwewe ambaye hakuwa katika hali nzuri ya kuzungumza,
Manguli alisema huenda mkwewe angefariki kama angekuwa ndani alfajiri
ile, ila biashara yake ndiyo imemuokoa.
Manguli
ameliambia gazeti hili kuwa msiba huo wa kijana wake aliyekuwa akifanya
kazi katika kampuni ya ulinzi ya Mahela Night Wash imempa jeraha ambalo
hatokaa kulisahau maishani mwake.
“Siamini
hadi sasa kama mwanangu amefariki pamoja na wajukuu zangu Danfod na
Fredy, lakini ndio hivyo ni mapenzi ya Mungu, ila sijui la kufanya,”
alisema kwa huzuni Mzee Manguli.
Alisema
jambo lingine la kusikitisha kwao ni namna misiba ilivyomuandama kwani
wiki moja iliyopita hapo hapo nyumbani kwake alifariki mdogo wake na
kusafirisha hadi kijijini kwao Mahenge mkoani Morogoro kwa maziko.
“Ijumaa
iliyopita mimi na marehemu mwanangu, tumerudi kutoka Mahenge kumzika
baba yake mdogo, na leo tena matanga yamerejea hapa hapa kwangu,”
alisema Manguli.
Kuhusu
taratibu za mazishi, msemaji wa familia hiyo, Mchungaji Geoffrey
Masanju alisema maandalizi yanaendelea na kutokana na hali ngumu ya
familia hiyo kwa sasa kutokana na kufululiza kwa misiba hiyo,
wanatarajia kuzika Jumamosi katika makaburi ya Kinondoni.
“Mazishi
yanataraji kufanyika Jumamosi katika Makaburi ya Kinondoni, lakini
kubwa zaidi tunasubiri michango kutoka kwa ndugu na jamaa pamoja na
Ofisi ya Mbunge wa Kawe ili kufanikisha mazishi haya,” alisema Mchungaji
Masanju.
Masanju
alisema mawasiliano baina yao na wazazi wa binti wa kazi aliyemtaja kwa
jina la Mariam mwenyeji wa Musoma mkoani Mara yanaendelea ili kufahamu
kama naye atazikwa pamoja na wenzake au atasafirishwa ijapokuwa uwezo wa
kusafirisha kama wao kwa sasa ni mdogo.
Alisema
msaada mkubwa wanaoutegemea wa kufanikisha maziko hayo ni kutoka kwa
Mbunge wa Kawe, Halima Mdee ambaye tangu kutokea kwa tukio alituma
mwakilishi wake ili kusaidiana na familia.
Post a Comment Blogger Facebook