Monday, June 8, 2015

MWANZA: Meya Matata ajiengua Chadema, Arejea CCM


HATIMAYE Meya wa Halmashauri ya Ilemela jijini Mwanza, Henry Matata, amejiengua ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kuhamia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Uamuzi aliufanya juzi katika mkutano wa hadhara uliofanyika eneo la Minazi Mitatu Kata ya Kitangiri Manispaa ya Ilemela ambako alikabidhi kadi yake ya Chadema kwa Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza, Miraji Mtaturu na kupewa ya CCM.

Akizungumza baada ya kurudisha kadi ya Chadema, Matata alisema kabla ya kujiunga na upinzani alikuwa ndani ya chama hicho tangu utotoni  lakini baada ya CCM kumfanyia mizengwe kwa kuweka jina lake nafasi ya nne katika kura za maoni kwenye uchaguzi wa  mwaka 2010, aliamua alikimbilia Chadema.
 
Alisema alipokimbilia Chadema alipokelewa kwa shangwe kwa sababu alikuwa anakubalika kwa wananchi na kumpa nafasi ya kuwania udiwani na kushinda Kata ya Kitangiri.

Alisema  baada ya kuanza kutekeleza majukumu ya udiwani  ndani ya upinzani alijikita kutekeleza ilani ya CCM ndipo alipoanza kuchukiwa.

“Mimi damu yangu ilikuwa CCM ingawa nilikuwa Chadema, baada ya kushinda udiwani nikaanza kupigania nafasi ya umeya kwa bahati nzuri nikapata.

“Sasa ukishakuwa meya lazima utekeleze ilani ya CCM kwa sababu ndiyo chama tawala… wenzangu wakaanza kunichukia na kuniundia zengwe kama ilivyokuwa awali CCM.

 “Ikafika wakati nikavuliwa uanachama nikabaki diwani wa mahakama- lakini sikupoteza chochote kwa sababu  stahili zangu zote nilipata,” alisema.

No comments:

Post a Comment