MTOTO WA WAKIKE WA MHESHIMIWA MACELA AGOMBEA URAIS CCM
MKURUGENZI Mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti Magonjwa ya Binadamu Dk Mwele Malecela mtoto wa Makamu wa zamani wa CCM John Malecela ni miongoni mwa wana CCM ambao wamejitosa kugombea urais kupitia CCM.
Dk Mwele kesho amepangiwa na CCM kuchukua fomu za kuomba kugombea
urais. Ratiba ya CCM iliyotolewa jana Makao Makuu ya chama hicho mjini
hapa inaonesha kuwa licha ya Dk Mwele, mwingine ambaye atachukua fomu
hiyo kesho ni Nicholaus Mtenda ambaye pia amejitokeza kuomba kugombea
urais kupitia CCM.
Dk Mwele katika maisha yake mengi kwa zaidi ya miaka 20 amekuwa
mtumishi katika Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu
(NIMR) ambako alianza kazi akiwa kijana na akapanda hadi kuwa mtafiti
mkuu na baadaye akateuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu.
Licha ya kukulia katika familia ya mwanasiasa maarufu nchini, lakini
Dk Mwele hajawahi kujitokeza hadharani kushiriki kwenye masuala ya
siasa. Kama akichukua fomu hiyo kesho, atakuwa ni mwanamke wa pili
kuomba kuteuliwa na CCM kugombea urais kumrithi Rais Jakaya Kikwete.
Mwanamke mwingine ni Balozi Amina Salum Ali wa Zanzibar. Jana Waziri
wa Malisili na Utalii, Lazaro Nyalandu na wanachama wengine wawili wa
CCM walichukua fomu za kuwania urais. Nyalandu alikuwa wa kwanza kufika
katika ofisi za CCM kuchukua fomu akiwa amefuatana na familia yake na
wafuasi wake kadhaa.
Baadaye alifuatiwa na mwanachama mwingine wa CCM, Peter Nyalali,
ambaye ni Ofisa mstaafu wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) na
kufuatiwa na mwanachama wa chama hicho kutoka wilaya ya Muleba, Leonce
Mulenda.
Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu, Nyalandu alisema hatua hiyo
ni ishara ya yeye kuanza safari ya ndoto yake ya kuchukua majukumu ya
urais kwa lengo la maendeleo ya nchi hii chini ya misingi aliyoianzisha
Baba wa Taifa, hayati, Mwalimu Julius Nyerere.
Kwa upande wa Nyalali, alisema atalenga katika kuimarisha uchumi kwa
kuzingatia Katiba ya nchi na ya chama na kuleta mabadiliko chanya ndani
ya CCM na kwa Watanzania ambao wamekuwa hawanufaiki na fursa zilizopo
nchini.
Kwa upande wa Leonce Mulenda, alisema atahakikisha Katiba ya Chama na
maamuzi yanatekelezwa kama inavyotakiwa na kuwa chama imara
kitakachosaidia serikali isiwe legelege.
No comments:
Post a Comment