UGAIDI Watikisa Tena Morogoro......Watu Watano Wajeruhiwa Kwa Bomu, Vijana Wawili Wanaswa Na Kutoroka Kimafia
Mpekuzi blog
WATU watano akiwemo dereva wa gari linalotumiwa na Mwenyekiti wa
Halmashauri ya wilaya ya Kilombero, David Ligazio ,Novatus Ngope (47),
wamejeruhiwa vibaya na shambulio la kitu kinachodhaniwa ni bomu la
kutupwa na mkono kutoka kwa watu wawili wasiofahamika walipokuwa kwenye
sherehe za Siku ya Wafanyakazi Duniani juzi.
Bomu hilo liliwajeruhi watu hao walipokuwa kwenye maadhimisho hayo
yaliyofanyika katika kijiji cha Msolwa Ujamaa ,Kata ya Sanje ,wilayani
Kilombero, mkoani Morogoro.
Dereva huyo anayeishi Ifakara anayeendesha gari la halmashauri lenye
namba za usajili SM 10632 na wenzake baada ya kulipuliwa na bomu
walikimbizwa Kituo cha Afya cha Nyandeo kilichopo Tarafa ya Kidatu
,baadaye walihamishiwa Hospitali Mtakatifu Kizito iliyopo
Mikumi,wilayani Kilosa.
Mkuu wa wilaya ya Kilombero, Lephy Gembe alithibitisha jana kwa njia
ya simu alipozungumza na mwandishi na kusema tukio hilo lilitokea
majira ya saa 2:00 usiku wa Mei Mosi mwaka huu eneo la Kijiji cha Sanje.
Alisema vijana wawili wanaotuhumiwa kurusha mlipuko huo baada ya
kuwajeruhi watu hao watano, walifanikiwa kukimbia kutoka eneo la tukio
na Polisi inaendelea kuwasaka ili watiwe nguvuni.
Hata hivyo alisema, bado mpaka sasa taarifa kamili kuhusu chanzo na
mazingira yake hakijafahamika na kwamba timu ya askari iliwasili eneo la
tukio kwa ajili ya kukusanya taarifa na kuwasaka wahalifu hao.
Alisema inawezekana huo ni muendelezo wa matukio ya kihalifu kufuatia
kukamatwa kwa watuhumiwa 12 waliokutwa na milipuko hatari na vitu
mbalimbali zikiwemo sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania(JWTZ)Aprili
14, mwaka huu katika Kata hiyo ya Kidatu, wilayani Kilombero.
"Ni wiki chache zilizopita tumewakamata watu 12 na milipuko hatari na
sare za jeshi , inawezekana kundi hili la kihalifu ni kubwa na wengine
wameendelea kujificha msituni,” alisema Mkuu wa wilaya.
Tukio la mlipuko huo umetokea karibu na eneo ambapo hivi karibuni
,Polisi iliwakamata watu kumi wakiwa na milipuko 30,sare za jeshi
,majambia, risasi ,bendera zenye maandishi ya lugha ya kiarabu ,vitabu
na madaftari wakiwa ndani ya msikiti wa Suni, Kidatu wilayani humo.
Kwa mujibu wa Mkuu wa wilaya hiyo, katika tukio hilo watu hao
waliojeruhiwa ni pamoja dereva wa gari la halmashauri ya wilaya ambalo
linatumiwa na Mwenyekiti wake.
“Pamoja na kumjeruhi dereva huyo pia gari limevunjwa kabisa kioo cha
nyuma na kupasuliwa cha mbele kutokana na mlipuko huo,” alisisitiza Mkuu
wa wilaya.
Hata hivyo alisema, timu ya maofisa wa vyombo vya ulinzi na usalama
vya wilaya hiyo tayari vimelekea eneo la tukio hilo kwa ajili ya kufanya
uchunguzi wa kina.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Ligazio , akielezea tukio hilo
alisema kuwa siku hiyo alikuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya siku ya
wafanyakazi ngazi ya kata ya Sanje, akiwa ni diwani wa kata hiyo.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo wa halmashauri, muda mfupi baadaye
alikuja Mwenyekiti wa kitongoji hicho Joseph Mhenga akiambatana na
vijana wawili .
Hata hivyo alisema, mwenyekiti huyo wa kitongoji kabla ya kufikishwa
kwake alishawahoji walipotokea na walionekana si wenyeji wa eneo hilo
kufuatia hofu walizokuwa wakizionesha.
Hata hivyo alisema vijana hao waliletwa kwake na mwenyekiti huyo wa
kitongoji ili kutaka ushauri kuhusu vijana hao na alimwambia vijana hao
wafikishwe katika kituo cha Polisi Kidatu kwa utaratibu mwingine wa
kipolisi.
Kabla ya kupelekwa kituoni , vijana hao walifanyiwa upekuzi na askari
wa mgambo, Thomas Manjole(54) ,mkazi wa Msolwa na walibainika kuwa na
bomu.
Hata hivyo alisema , vijana hao walilitoa bomu hilo kiunoni na
kulirusha kwenye gari la halmashauri ambalo linatumiwa na Mwenyekiti wa
halmashauri hiyo.
Bomu hilo lilipolipuka likamjeruhi dereva wake aliyekuwa ndani ya
gari pamoja na wengine wanne akiwemo askari mgambo.
Kwa mujibu wa
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo ambaye hakuwemo ndani ya gari aliwataja
majeruhi hao ni dereva wake ,askari mgambo alikuwa akiwapekuwa vijana
hao, Amos Msopole(29) na Azama Naniyunya(59) wote wakazi wa Kijiji cha
Msolwa Ujumaa.
Kwa upande wake Ofisa Mtendaji wa Kata ya Sanje , Hawa Ndachuwa
,alidai siku ya tukio watu wawili walikodi bodaboda kutoka Kata ya
Kidatu na kuomba wapelekwe eneo la Kata ya Mkula .
Hata hivyo alidai kuwa, walipofika Msolwa Ujamaa, dereva wa bodaboda
aliwashuku watu hao na kutaka aongezewe fedha za malipo kwani mapatano
hayakulingana na umbali.
Alisema watu hao walikubali kumuongezea fedha na walimwomba
kuwaonesha sehemu ya kutolea fedha na kuwapeleka eneo la kutolea fedha
na kwamba mwendesha bodaboda huyo aliamua kuuarifu uongozi wa serikali
ya kitongoji hicho.
Kwa mujibu wa Ofisa Mtendaji wa Kata hiyo, baada ya wananchi kuwaona
watu hao walipatwa na mshtuko kutokana na mavazi waliyovaa na kisha
kuwaweka chini ya ulinzi na kuanza kuwapekua na ulifanyika chini ya
ulinzi wa askari mgambo wa kijiji.
Hivyo alisema, wakati wanaendelea kupekuliwa, mtuhumiwa mmoja
alikutwa na viberiti vya gesi na wakati upekuzi ukiendelea mtuhumiwa
mwingine aligoma kutoa ushirikiano hali iliyowatia hofu zaidi wananchi
ambapo walimwona akiwa na kitu amekihifadhi kiunoni.
Ofisa Mtendaji huyo alisema, wakati wanaendelea kupekuliwa mtuhumiwa
wa kwanza alifanikiwa kukimbia na wakati wanajiandaa kumdhibiti wa pili
alitoa kitu kama bomu na kurusha lilipo hilo gari la mwenyekiti na kutoa
mlipuko mkubwa na yeye pia kutoroka.
Kutokana na mlipuko huo , askari mgambo Manjole ndiye alijeruhiwa
vibaya kwa kuvunjika mguu na mkono huku dereva wa mwenyekiti Novatus
akiumia begani na wote wanne kuchukuliwa na kupelekwa katika kituo cha
afya cha Nyandeo .
Hata hivyo alisema , Polisi walifika eneo la tukio na kuwasiliana na
wataalamu wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) waliopo eneo ya Kidatu ili kubaini
bomu hilo huku wakiendelea kuwasaka watuhumiwa.
Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mtakatifu Kizito, Maximilian
Mwenda, alithibisha kupokea majeruhi wanne wa tukio hilo, kati yao mmoja
akiwa na hali mbaya ambapo wengine wanaendelea kupatiwa matibabu na
hali zao zinaendelea vyema.