Monday, June 8, 2015

Membe Atangaza Nia ya Kugombea Urais ......Aahid kuipeleka Nchi kwenye Uchumi wa Viwanda


WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, ametangaza rasmi kuwania urais wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM}, huku akitamba ataipeleka nchi katika uchumi wa viwanda unaobebwa na kilimo na kuahidi kujenga serikali ya waadilifu.
 
Licha ya Membe, wana CCM wengine wawili jana walitangaza pia kugombea urais nao ni Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia Januari Makamba pamoja na Mbunge wa Nzega Dk Hamis Kigwangala.
 
Membe alifichua kuwa alienda kuomba kwenye kaburi la Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere ili kupata ridhaa na kusisitiza kuwa urais si suala la kukurupuka na kwamba atahakikisha anasimamia utawala bora, huku akiongoza mapambano dhidi ya rushwa na kwa kubadili kipengele cha mtu atakayetoa rushwa na kutoa taarifa awe huru.
 
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya CCM Mkoa wa Lindi jana, Waziri Membe alisema kabla ya kuchukua uamuzi wa kufikiria urais alijipima na kuona anatosha kwa nafasi hiyo, pia baada ya kuwaangalia wagombea wenzake wote anaamini yeye ndiye mwenye sifa za kustahili kuwa Rais wa Awamu ya Tano ya Tanzania.
 
Aliwaambia wananchi kwenye mkutano huo kuwa uadilifu wake ni wa kuzaliwa, uwajibikaji usio wa kawaida na ndiyo sababu kila uchaguzi wananchi wa Jimbo lake la Mtama wamekuwa wakimchagua kwa idadi kubwa ya kura.
 
“Mwaka 2010 nilishinda ubunge kwa asilimia 86 ya kura, nimekuwa mbunge tangu mwaka 2000 na kila uchaguzi idadi ya kura zangu zinaongezeka…Niwaahidi jimbo la Mtama litabaki katika mikono salama, hakuna mgombea wa Ukiwa wala Ukawa atakayeshinda, ila milele litabaki kwa CCM.
 
"Nina uzoefu mkubwa ndani ya chama, nimesoma siasa darasani mwalimu wangu akiwa Mzee Mangula (Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula}, mwaka 2007-2012 nimekuwa Katibu wa Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa CCM, Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM kuanzia mwaka 2007 hadi 20012, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM kuanzia mwaka 2012 hadi 2017 hizo ni katika chama."
 
Pia alisema upande wa serikalini ana uzoefu mkubwa baada ya kuwa Ofisa usalama wa Taifa kuanzia mwaka 1978, Ofisa Ubalozi,Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Naibu Waziri wa Nishati, Waziri wa Mambo ya Nje kuanzia Desemba mwaka 2006 hadi sasa.
 
Akielezea uzzoefu wake alitaja nyadhifa mbalimbali alizoshika zikihusisha kimataifa ikiwemo ya sasa ya Mwenyekiti wa Baraza la Kazi Jumuiya ya Madola kwamba zinamfanya aamini anaweza kurithi viatu vya Rais Jakaya Kikwete.
 
Kwa nini anautaka urais? Akizungumza kilichomsukuma kuwania urais, Membe alisema alitaafakari kwa kina uamuzi huo kwani kazi hiyo si jambo jepesi unashika hatima ya Watanzania na masuala mengine kadha wa kadhaa.
 
Nimejiangalia mwenyewe, nikaangalia wenzangu wote, nikasema nikimpata mwenye sifa hizi ningeacha… nimepitia mmojammoja nimeona hakuna kama Membe. Urais si suala la kukurupuka. Unaweza ukakurupuka kazi nyingine, lakini urais muachieni Membe.
 
Kuomba kaburini kwa Nyerere 
Alifichua kuwa Machi mwaka huu alialikwa na Chifu wa Wazanaki kijijini Butiama kwa hayati Mwalimu Nyerere kulikokuwa na sherehe ya wazanaki, ambapo alienda katika kaburi la Nyerere aliyekuwa Rais wa Kwanza wa Tanganyika na baadaye Tanzania na kusali na kuzungumza kuhusu nia yake ya kuomba urais.
 
“Nilisali pale, nikamwambia Mwalimu unanijua vizuri Membe, nataka kutia nia ya urais, nataka kuvaa viatu vyako alivyovaa Mzee Mwinyi, Mkapa na Kikwete. Nilisema nilienda Ikulu nimevikuta viatu bado vipo vizima, kama utaona sitoshi au ni oversize nipitishiwe mbali kikombe hiki.",alisema.
 
Alisema timu yake iliyokuwa inazunguka nchi nzima ilimletea taarifa kwamba anafaa kwa urais na kujiuliza pengine Nyerere amejibu kwa njia hiyo na kusisitiza kuwa ana uhakika Nyerere atafurahi akishinda.
 
Pia aliahidia hatakubali mtu awadhihaki marais wastaafu Mkapa, Mwinyi na Kikwete na kumsifu Kikwete kwamba amefanya kazi kubwa sana katika suala la kuinua elimu nchini.
 
Kigwangala wazee watupishe
Mbunge wa jimbo la Nzega mkoani Tabora Dk,Hamisi Kigwangalla amesema kwamba huu ni wakati wa vijana kuliongoza taifa hili na ameahidi kuwa iwapo atapitishwa na chama chake ana kashinda atahakikisha kila Mtanzania anakuwa na bima ya afya.
 
Alisema ni wakati wa watu ambao hawajaingia serikali kushika wadhifa wa urasi kwani uzoefu umeonesha kuwa marais ambao huwa wameshafanya kazi serikalini huwa wanaharibiwa na mfumo na hivyo kutofanya vizuri. "Umefika wakati wa kuwa na rais ambaye hajafanya kazi serikalini, wazee watupishe sasa ni wakati wa sisi vijana," alisema Dk Kigwangala.
 
Pia alisema hakuna uzoefu katika nafasi ya urais bali wenye uzoefu huo wapo wanne ambao tayari wamekwisha pitia nafasi hiyo na kukaa kwenye jengo la Ikulu ambao aliwataja kuwa Baba wa Taifa Mwl,Julius Nyerere,Ali Hassan Mwinyi, Benjamini Mkapa na Rais Jakaya kikwete.
 
Akihutubia wananchi wa Jimbo la Nzega mjini Nzega, Dk Kigwangalla alisema wengine wote waliobaki sio wazoefu wa kufanya kazi Ikulu bali ni wazoefu wa shughuli nyingine.
 
Alisema kuwa wote wanaowania nafasi hiyo akiwepo yeye mwenyewe wanauzoefu tofauti tofauti katika masuala mbalimbali, huku akiwabeza wenye uzoefu wa ubadhilifu wa mali za umma ikiwemo Rushwa na ufisadi hali ambayo akiteuliwa na kushinda nafasi hiyo atapambana navyo.
 
Dk Kigwangalla katika vipaumbele vyake iwapo atateuliwa na kushinda nafasi hiyo, alisema atahakikisha ndani ya mwaka mmoja, Watanzania wote watakuwa na Bima ya Afya watakao lipiwa na Serikali pamoja na kuwa jari watumishi wa Idara ya Afya na Ustawi wa Jamii ili waweze kutoa huduma bora ya matibabu kwa wananchi.
 
"Iwapo Watanzania hawatapata huduma bora ya Afya kama kiongozi wa Nchi mwisho wa siku utaongoza Taifa la wagonjwa na hivyo kudhoofisha nguvu kazi ya Taifa hali ambayo inayoweza kusababisha kushuka kwa uchumi wa Nchi’’alisema dkt Kigwangalla.
 
Alisema katika kuboresha suala la Elimu kwa watanzania kama atashika nafasi hiyo anatamanai Elimu yote kuanzia Awari,msingi na sekondari bure kwa kuwa atahakikisha nchi inakuwa na uchumi imara kwa kupunguza matumizi ya serikali,safari,posho na ukubwa serikali.
 
Akizungumzia suala la kukuza uchumi kwa wakulima,wafanya Biashara wadogowadogo na viwanda anatamani kuanzisha mfuko wa kukopesha wananchi kwa kuwekeza Bill 500 kwa mwaka pamoja na kuboresha kitengo cha ustawi wa jamii katika Halmashauri kwa ajili ya kwa Elimisha,kuwaunganisha kwenye vikundi vya kudhaminiana na kuratibu shughugili zao.
 
Alisema kwa kufanya hivyo Serikali itakuwa inauwezo wa kuzalisha ajira rasimi laki mbili kila mwaka na ajira zisizo rasimi milioni kumi kila mwaka na uchumi huu utamgusa kila mtu kila mwaka. 
 
Januari Makamba kuunda serikali ndogo 
Kwa upande wake Januari Makamba amesema endapo atapewa ridhaa ya kugombea na kuteuliwa kuwa rais ataunda serikali ndogo yenye mawaziri wasiozidi 18 ambayo utendaji wake utakuwa wa kutukuka.
 
Pia alisema atatoa Sh milioni 50 kila kijiji hapa nchini ili kupambana na umasikini wa wananchi uliokithiri. Alisema akiwa rais atajikita zaidi katika kukuza uchumi wa mtu mmoja moja, kuwezesha upatikanaji wa huduma bora za Jamii ikiwemo afya, elimu, na umeme.
 
Vipaumbele vingine vya serikali yake vitakuwa ni pamoja na kusimamia utawala bora na sheria, kusimamia uchumi na kuziwezesha taasisi za fedha kukuza uchumi kwa kuunda baraza la uchumi la taifa. Kipaumbele kingine ni kulinda amani, umoja na usalama wa taifa kwa kuwashirikisha wananchi na viongozi wa dini.
 
Vilevile atajikita katika kudumisha muungano uliopo na uweze kuwa na manufaa zaidi na kudumu kwa kipindi kirefu. 
 
Katika suala la Kupambana na ukosefu wa ajira, Makamba alisema ataanzisha mfumo maalum wa kuwaunganisha vijana waunde vikundi na kuwapatia mikopo ili waweze kujiajiri na kuondokana na umasikini pamoja na kuwa walipa kodi.
 
Aidha aliahidi endapo atateuliwa kuiongoza nchi, atajenga viwanda 11 vya nguo vitakavyozalisha ajira zaidi 100,000 na kipaumbele kwa watakaoajiriwa ni wanawake na vijana.
 
Katika tasnia ya michezo, alisema atarasimisha kazi zote za wasanii ili waweze kufaidika na kazi zao pamoja na taifa kunufaika kwa kukusanya kodi.
 
Kuhusiana na kukabiliana na migogoro ya ardhi, alisema ataanzisha upimaji wa ardhi kwa kutumia mitambo ya setilaiti na kugawa hati kwa Wakulima, wafugaji na wananchi zenye picha za mipaka Yao ili kuondoa utata na migogoro.
 
Katika huduma ya afya, Makamba alisema atahakikisha wananchi wote wanapata bima ya afya pamoja na kuboresha upatikanaji wa huduma hiyo Karibu Na maeneo ya wananchi.
 
POSTED BY.RASHID HAMZA

No comments:

Post a Comment