Kikwete aagwa kifalme Uholanzi
RAIS Jakaya Kikwete jana aliagwa kifalme katika ziara yake ya kikazi
nchini Uholanzi, huku akielezea kwa kiasi kikubwa mafanikio ya utawala
wake katika miaka kumi aliyokaa madarakani.
Kikwete aliyewasili juzi usiku mjini hapa akitokea katika ziara yake
ya nchi za Finland, Denmark na Sweden, alipokelewa na kupewa heshima
zote za kifalme, ikiwa ni pamoja na kupewa makazi katika kasri la
Mfalme, akiwa kiongozi wa tatu wa Afrika kupewa hadhi hiyo nchini hapa.
Wengine waliowahi kupewa hadhi hiyo ni Rais wa Kwanza mzalendo wa
Afrika Kusini, Hayati Nelson Mandela na Askofu Mkuu mstaafu wa mji wa
Cape Town, Afrika Kusini na mshindi wa tuzo la Nobel Desmond, Desmond
Tutu.
Rais Kikwete baada ya kukutana na Balozi wa Tanzania nchini hapa,
Wilson Masilingi na maofisa wake, alianza kazi kwa vikao na wawekezaji,
ikiwemo kampuni ya Shell, alikutana pia na kuzungumza na Mfalme Willem
Alexander na baadaye alikutana na Rais wa Mahakama ya Kimataifa ya
Uhalifu (ICC) katika makao makuu ya mahakama hiyo, Silvia Alejandra
Fernandes de Gurmendi.
Jioni alikutana na mabalozi wa Afrika, wanaowakilisha nchi zao nchini
Uholanzi, ambapo alitumia fursa hiyo kuwaaga, akiwataka wampe
ushirikiano rais ajaye, lakini pia alielezea mafanikio makubwa
aliyoyapata katika utawala wake.
Alisema ingawa anaondoka madarakani baada ya utawala wake wa miaka
kumi, anaamini Tanzania itapata kiongozi mzuri licha ya mchuano mkubwa
unaoendelea, akisema alikuwa na taarifa kuwapo kwa makada 34 wa CCM
wanaowania kutaka kumrithi.
“Ninamaliza muda wangu, hivyo napita kuaga marafiki na nchi wahisani.
Tuna historia ndefu na Uholanzi, tangu enzi za Nyerere (Hayati Baba wa
Taifa, Mwalimu Julius Nyerere). Babu wa huyu Mfalme (Willem) alikuwa na
shamba Tanzania, lakini pia baba yake amesoma Tanzania. Hawa ni ndugu
zetu,” alisema na kuishukuru Serikali ya kifalme ya Uholanzi kwa kumpa
mwaliko rasmi wa kikazi.
Hata hivyo, Rais Kikwete alipokuwa akizungumzia kasi ya kuondoa
umasikini, alisema bado juhudi za kuondoa umasikini zinahitajika na
zitafanikiwa kwa kuelekeza nguvu kwenye kilimo, ambacho ndicho
kinachoajiri na kutegemewa na Watanzania wengi zaidi hasa wanaoishi
vijijini.
Rais Kikwete pia amefanya mazungumzo na Spika wa Bunge la Sweden,
Urban Ahlin, pamoja na viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa nchini
humo na kushukuru kwa misaada ya maendeleo kwa takribani miaka 50Nsasa.
Mabalozi hao wa Afrika wamempongeza Rais Kikwete kwa kufanya ziara ya
shukrani na kuwaaga nchi rafiki na wahisani, kwani ni mara chache kwa
viongozi wengi wa Kiafrika kuaga na kuondoka madarakani.
Kwa upande wa elimu, alisema wakati akiingia madarakani mwaka 2005,
alikuta Tanzania, yenye watu wengi zaidi katika nchi wanachama wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), iko nyuma ikilinganishwa na Kenya na
Uganda, kwa idadi ya wanafunzi waliokuwa wakisoma shule za sekondari na
vyuo.
Kwa upande wa elimu ya juu, Rais Kikwete alisema vyuo vikuu
vimeongezeka kutoka 26 mwaka 2005 hadi kufikia 52 na idadi ya wanafunzi
walio katika vyuo vikuu ilitoka 40,719 hadi kufikia 200,956.
Hata bajeti ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu imeongezeka kutoka
Sh bilioni 56.1 hadi Sh bilioni 345 mwaka 2014. Rais Kikwete
anatarajiwa kurejea nyumbani leo.
No comments:
Post a Comment