Baadhi ya benki nchini zinadaiwa kuajiri baadhi ya wafanyakazi walio
kwenye mtandao wa majambazi kutokana na wateja wengi kupigwa risasi na
kufa wakitoka kuchukua pesa, uchunguzi wa baadhi ya askari wa Jeshi la
Polisi Tanzania umebaini.
Hayo yalisemwa na baadhi ya askari hao wiki iliyopita walipozungumza na
mwandishi wetu na kusema kwamba, waajiri wasipokuwa makini katika
kuajiri watashangaa kuona wateja wao wanapigwa risasi na kuuawa kila
kukicha.
“Haiwezekani kuwa wanaonyang’anywa fedha ni wale wanaotoka kuchukua
benki kuliko wanaopeleka! Ina maana wezi wapo katika baadhi ya mabenki
hivyo kunatakiwa kuwepo na umakini wakati wa kuwaajiri,” alisema askari
mmoja kutoka makao makuu ya jeshi hilo, Dar akiomba hifadhi ya jina lake
kwa vile yeye si msemaji.
Afande huyo aliendelea kusema kuwa, baadhi ya wafanyakazi wasio
waaminifu wa benki hizo wanapoona mteja anachukua fedha nyingi hufanya
mawasiliano kwa njia ya simu kuwaeleza majambazi walio nje namna
alivyovaa mteja huyo na kiasi cha fedha alichochukua.
Uchunguzi zaidi unaonesha kuwa, endapo hali hiyo haitadhibitiwa haraka
huenda wananchi wakapatwa na hofu ya kuweka fedha zao benki kwa kuogopa
kuporwa na kupigwa risasi wakienda kuzichukua.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, DCP Simon Sirro
(pichani) ambapo alikiri kuwepo kwa baadhi ya wafanyakazi wenye mtandao
na majambazi huku akisema jeshi lake limeweka mikakati kuhakikisha
mtandao huo unasambaratishwa mara moja.
“Ni kweli kwamba, baadhi ya mabenki, si yote, yameajiri baadhi ya
wafanyakazi, si wote wenye mtandao na majambazi. Kwa hiyo hata wao ni
majambazi tu.
“Sasa tumejipanga vizuri ikiwa ni pamoja na kukamata pikipiki
zinazohusika katika uhalifu. Pia tumeamua kuweka makachero nje na ndani
ya mabenki, wapo polisi wa miguu, pikip iki na magari. Nina uhakika
tutawadhibiti,” alisema Kamanda Sirro.
Aliendelea kusema kuwa, majambazi waliopo katika Kanda ya Dar es Salaam
waanze kufunga virago kwani bila kufanya hivyo wajue watakamatwa wote na
mtandao wao kumalizika. Pia aliwataka wamiliki wa mabenki kuwa makini
wakati wa kuajiri wafanyakazi ili kuwapata wenye sifa njema na kuweka
imani kwa wateja wao.
Aliyekuwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishina
Suleiman Kova aliwahi kutamka kuwa, baadhi ya wafanyakazi wa ndani wa
baadhi ya benki wana ushirikiano na majambazi. Akawatahadharisha
wamiliki kuwa makini wakati wa kuajiri.