Pombe Zitamtoa Roho Mwigizaji Johari ..Adaiwa Kuwa na Msongo wa Mawazo
Johari Chagula |
Pombe zitamtoa roho! Unywaji wa pombe kupita kiasi anaoufanya staa wa sinema za Kibongo, Blandina William Chagula ‘Johari’ umetafsiriwa kama kujihatarisha kiafya baada ya hivi karibuni kunaswa mchana wa jua la utosini akifakamia ulabu huku akionekana kuzidiwa, jambo lililozua minong’ono kwa baadhi ya watu, Risasi Mchanganyiko lilimnyatia.
Tukio hilo lililopigwa chabo na mwanahabari wetu lilijiri juzikati maeneo ya Sinza-Mori jijini Dar ndani ya baa moja (jina tunachikichia) akiwa peke yake na mwenye kuonekana kughubikwa na lindi zito la mawazo.Awali, mwandishi wetu aliyekuwa ‘akineng’eneka’ kwenye baa hiyo kwa kazi maalum, alimshuhudia Johari akiingia na kukaa huku akionesha tahadhari kwa kuangaza macho huku na kule mara kwa mara kama aliyekuwa akimtafuta mtu na kumuita mhudumu kisha kumnong’oneza jambo ambapo mhudumu huyo alionekana akielekea kaunta.
Akiwa ‘ametumbua’ macho, mwandishi wetu alimfuatilia mhudumu huyo na kubaini kinywaji kilichoagizwa na Johari ni pombe ndipo akaweka sawa kamera yake kwa ajili ya lolote. Kwa kasi, paparazi wetu alimfotoa picha za mbali na kwa tahadhari ya kutoshtukiwa kabla ya kuondoka eneo la tukio.
Hata hivyo, baadhi ya watu waliomshuhudia Johari kabla na baada ya kuagiza ‘masanga’, walisikika wakionesha mshangao wa wazi.“Mmh, unajua huyu msanii pombe zitamtoa roho, lakini si kawaida yake, kutakuwa na jambo kwani anaonekana ana msongo,” alisikika mmoja wa wateja waliokuwa wamekaa karibu na mwandishi wetu.
Mwandishi wetu hakuweza kumfuata Johari mahali alipoketi na badala yake aliondoka kisha kumpigia simu ambapo awali alikataa kutokuwepo kwenye baa hiyo lakini baada ya kubanwa kwa hoja nzito, alijikuta akikiri na kufunguka jambo jipya.
“Dah! Ulikuwa umekaa wapi? Lakini siyo mawazo nimeamua tu kupumzika na kazi kwa leo hivyo nikaona si vibaya kama nitajiburudisha kwa kinywaji hiki,” alisema Johari.
GPL