Monday, June 8, 2015


WAGOMBEA URAIS VIKUMBO KILA KONA YA NCHI


 mangula press

NA WAANDISHI WETU
MAKADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliotangaza nia ya kugombea urais, sasa ni wazi wanapigana vikumbo kila kona ya nchi.
Hatua hiyo inatokana na kila mtangaza nia kwa nyakati tofauti kutoa kauli nzito.
Wapo makada ambao kauli zao zinaonyesha wazi kuwa kuna mgongano ndani ya CCM, huku wengine wakitangaza nini watakifanya endapo watateuliwa kuongoza nchi.

MEMBE: SINA UNDUGU NA JK

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, amesema hana undugu na Rais Jakaya Kikwete.
Membe ambaye pia ni Mbunge wa Mtama, alikanusha undugu wake na Rais Kikwete mjini Dodoma jana wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuchukua fomu ya kuomba kuwania urais kupitia CCM.
Akijibu maswali ya waandishi wa habari, alisema hana undugu na Rais Kikwete, ingawa baadhi ya nchi ambazo amekuwa anatembelea wamekuwa wakimfananisha naye.
Alisema baadhi ya sehemu hushindwa kumtofautisha kiasi cha kumpa hadhi ya urais ikiwamo kumwomba wapige naye picha.
“Mimi siyo ndugu wa damu wa Rais Kikwete, nimechukua sura, rangi na ufupi kutoka kwa mama yangu. Kwa bahati mbaya na Rais Kikwete pia kachukua sura kutoka kwa mama yake, bado mama zetu siyo ndugu.
“Hata hivyo, kungekuwa na aibu gani kiasi cha mimi kuficha kwamba Rais Kikwete siyo ndugu yangu, ningepata hasara gani kukubali ni ndugu yangu kwa sababu kama ni madaraka tayari nilishajipatia vyeo,” alisema.
Alisema wakati mwingine huwa anaenda katika kaburi la wazazi wake kuwaomba awasamehe wale wote ambao wanazusha maneno kuhusu undugu wake na Rais Kikwete.
“Wazazi wangu walishafariki dunia, wawaache wapumzike kwa amani na waniache niendelee na njia yangu,” alisema.
Katika hatua nyingine, Membe aliahidi kutoa ushirikiano kwa waandishi wa habari pindi akiingia madarakani.
Alisema ataangalia sheria zote zinazohusu vyombo vya habari.
Membe alikuwa akijibu swali jinsi atakavyohakikisha vyombo vya habari vinafanya kazi kwa uhuru kutokana na kauli yake kwamba endapo atapata nafasi ya kuongoza nchi, atavitaka kuhakikisha vinafichua rushwa.
“Ili waandishi wa habari wafanye kazi kwa uhuru, lazima waandaliwe mazingira ya kufanya kazi vizuri, tutaziangalia sheria zote zinazoendesha vyombo vya habari.
“Lengo ni kujenga mazingira mazuri ya kuwaweka waandishi wa habari kuwa na uhuru wa kuandika chochote bila kuogopa kufungwa au kunyanyaswa,” alisema Membe.
Alirejea kauli ya Rais Barack Obama wa Marekani walipokutana katika mazungumzo ambapo alisema ‘kabla ya kufikiria kuvishitaki vyombo vya habari kwa kumshambulia, lazima kwanza ashauriane na mwanasheria wake’.
Alisema hadi sasa Rais Obama hajawahi kushitaki chombo cha habari chochote kutokana na mwanasheria huyo kukataa.
“Rais Obama aliniambia nchi inapumua kupitia waandishi wa habari, nchi inatoa dukuduku lake kupitia vyombo vya habari na mimi nitapita huko,” alisema.
Akizungumzia baadhi ya vipaumbele vyake kama akifanikiwa kuwa rais, alisema atahakikisha nchi inakuwa na uchumi wa viwanda.
Alisema jambo hilo litawezekana kutokana na ugunduzi wa gesi asilia, hivyo nchi itakuwa na nishati ya kutosha.
“Nitahakikisha Serikali yangu inazingatia utawala bora, utawala wenye nidhamu, isiyo na ufisadi na inayopiga vita rushwa na harufu yake,” alisema.

LOWASA APATA MAPOKEZI MAKUBWA GEITA, AZOA WADHAMINI 3,000

WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa jana aliingia wilayani Geita na kupokewa na umati wa wananchi ambako alidhaminiwa na zaidi ya wana CCM 3,000.
Kaimu Katibu wa Wilaya ya Geita, Killian Balindo alisema waliotakiwa kumdhamini Lowassa katika wilaya hiyo ni wanachama 45, lakini waliojitokeza wamefikia zaidi ya 3,000.
Akizungumza na wananchi waliokusanyika mbele ya ofisi ya CCM Mkoa wa Geita, Lowassa alisema japo haruhusiwi kufanya kampeni ameahidi kushughulikia matatizo ya maji, wachimbaji wadogo na mawe yaliyoisha dhahabu (magwangala).
“Hayo ya bodaboda, mamantilie kushughulikia. Nikiingia ikulu ni kuweka tu kalamu nyekundu. Kazi yangu ikikamilika nitashughulikia magwangala,” alisema Lowassa.
Kuhusu wachimbaji wadogo, alisema atawapa kipaumbele kwa kuwamilikisha maeneo ya uchimbaji na mitaji.
“Nilipokuwa mbunge miaka ya 80, niliondoa shilingi bungeni kupinga wachimbaji wadogo kunyanyasika. Nitahakikisha kila mchimbaji anapata eneo lake. Serikali inajua maeneo yote yenye madini. Halafu tutawapa fedha ili wawekezaji wakubwa wakija waweze kushindana,” alisema Lowassa.
Msafara wa Lowassa ulikuwa na magari, pikipiki na baiskeli huku ikisindikizwa na helikopta ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita, Joseph Msukuma.
Awali Lowassa jana aliingia katika Jimbo la Chato linaloshikiliwa na Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli na kupata mapokezi makubwa ya wanachama waliojitokeza kumdhamini.
Dk. Magufuli ambaye pia amechukua fomu za kugombea urais bado hajafika jimboni humo kutafuta wadhamini.
Lowassa aliingia Chato saa 8:30 mchana na kuelekea kwenye ukumbi wa ofisi ya CCM wilaya walikokuwa wamekusanyika wana CCM.
Akizungumzia udhamini huo, mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM wilayani humo, Deusdedith Katwale, alisema wanachama waliojitokeza kumdhamini wamefikia 430.
“Tunashukuru kwa kuipa kipaumbele Chato, hiyo ina maana sana siku zijazo,” alisema Katwale.
Naye Lowassa aliwashukuru wanachama hao na kurudia wito wake wa kuchagua rais aliyebobea katika chama.
“Tunakwenda kuchagua rais, tutafute mtu anayekijua chama. Angalieni historia yake na rekodi ya mambo aliyofanya,” alisema Lowassa.

AWAPONGEZA WANA CCM PEMBA

Awali akiwa kisiwani Pemba jana asubuhi, Lowassa amewasifu wanachama wa CCM kisiwani Pemba kwa kujiimarisha dhidi ya upinzani mkali wa Chama cha Wananchi (CUF).
Tangu kuanza kwa siasa za upinzani mwaka 1995, CCM imekuwa katika wakati mgumu visiwani Zanzibar, na hasa Pemba.
Akizungumza na wana CCM wilayani Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba alikokwenda kutafuta udhamini kwa ajili ya kupitishwa kugombea urais kupitia chama hicho, Lowassa alisema wana CCM kisiwani humo wanastahili pongezi.
Alisema alifika kisiwani humo mara ya mwisho mwaka 1984 na kwamba akifanikiwa kupata urais atafanya ziara ya muda mrefu kisiwani humo.
“Nilifika hapa mwaka 1984 na sijawahi kurudi tena. Lakini endapo nitafanikiwa safari yangu, nitakuja siku mbili tatu tuzungumze.
“Nawapongeza kwa jitihada zenu, licha ya upinzani mkali wa CUF bado mmeendelea kujiimarisha. Nitakuja Pemba siku mbili tatu nitakapofanikiwa ili tuzungumze,” alisema.
Lowassa pia alizungumza na wana CCM wa Wilaya ya Chakechake, Mkoa wa Kusini Pemba na kuwapongeza kwa jitihada zao za kukilinda chama chao licha ya upinzani mkali.
Lowassa alifanikiwa kupata udhamini wa wana CCM 90 katika wilaya za Wete na Micheweni Mkoa wa Kaskazini.
Akizungumzia hali ya chama hicho wilayani Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba, mmoja wa makada wa CCM, Juma Amir Juma alisema wanachokitegemea ni rehema za Mwenyezi Mungu.
“Hatusemi tutaendelea kushindwa, Mungu ni mkubwa ipo siku tutashinda. Lakini hali ni mbaya sana, kwani kama Mbunge wa CUF anapata kura zaidi ya 5,000 wa CCM anapata kura 500, wapi na wapi? Lakini hatukati tamaa,” alisema Juma.
Katibu wa CCM mkoa wa Kaskazini Pemba, Ali Haji Makame, alisema kuna wana CCM wengi walitamani kumdhamini Lowassa, lakini wameshindwa kutokana na idadi maalumu kuwekwa na kanuni za chama hicho ambayo ni wanachama 45 kwa kila wilaya.
Lowassa aliwasili Zanzibar juzi na kupokewa na umati mkubwa wa wanachama wa CCM walioandamana naye hadi katikati ya mji wa Unguja.
Kwa ujumla Lowassa amepata wadhamini 450 katika visiwa vya Unguja na Pemba.

NYALANDU ATANGAZA MAGEUZI YA KISERA

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, amesema endapo atafanikiwa kuwa Rais wa Tanzania, atahakikisha anafanya mageuzi makubwa ya kisera kwa kuweka vipaumbele vya uchumi ili kuwanufaisha wananchi wa kipato cha chini.
Alisema mageuzi hayo yataendana na mabadiliko ya mifumo ya kiutawala kwa kutengeneza uwiano wa mgawanyo wa rasilimali sawa kwa wananchi wa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wale wa Zanzibar.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumaliza ziara ya kutafuta wadhamini mjini Unguja, Zanzibar jana, Nyalandu alisema haitoshi kusikia pato la taifa linakua na uchumi wa nchi unaimarika katika ngazi ya Serikali Kuu pekee, bila ya kuwanufaisha wananchi wa kipato cha chini.
Nyalandu, alieleza kwamba endapo atapata ridhaa ya wananchi na kumchagua kuwa rais, anatarajia kuleta mabadiliko makubwa ya kimaendeleo katika nyanja za kiuchumi, kijamii na kisiasa kwa kuzingatia utu na haki ili kujenga jamii moja ya Watanzania watakaonufaika na matunda ya nchi yao.
Alisema jambo la kwanza atakapopata nafasi ya urais, atahakikisha anaondosha dhana ya watunga sera ambao ni wabunge na wawakilishi kuhakikisha wanatunga sera imara zisizokuwa na chembe ya kulinda masilahi yao, bali ziwe na upana wa kulinda masilahi ya wananchi.
Nyalandu alisema ataweka mifumo imara ya kisheria inayodhibiti viongozi wa ngazi za juu ambao ni watumishi wa umma kufanya biashara na uwekezaji pindi wanapokuwa madarakani, bali mtu afanye kazi moja ya kuwatumikia wananchi ama kufanya biashara.
“Tanzania kwa awamu hii inahitaji kuwa na rais anayefahamu tafsiri halisi ya umasikini na anayechukia jinamizi la ubaguzi na utengano baina ya wananchi wa nchi moja na kuondosha nyufa zilizopo katika Muungano, nami nimejipima nikaona uwezo huo ninao na sababu za kuiongoza nchi kwa uadilifu pia ninazo hivyo wananchi nakuombeni mfanye maamuzi ya kunichagua ili niwatumikieni,” alisema.

LUHAGA MPINA ACHUKUA FOMU, AAHIDI KUONGEZA MAPATO YA SERIKALI

MBUNGE wa Kisesa, Luhaga Mpina, naye ameungana na makada wengine wa CCM kuchukua fomu za kuwania kuteuliwa kugombea urais.
Mpina alichukua fomu hiyo mjini Dodoma jana, huku akijinasibu kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani na kudhibiti mapato yanayokusanywa.
“Nitakuja na njia mbadala ya kuhakikisha mapato ya ziada yanapatikana ili kupata fedha kwa ajili ya huduma za jamii katika sekta mbalimbali kama vile elimu na afya.
“Kwa sasa watu hawalipi kodi, mikataba mibovu inatafuna taifa, mikataba ya gesi ina kasoro kubwa, makampuni makubwa ya madini yanakwepa kodi kwa kiwango kikubwa, haya mambo ninayafahamu na nitayasimamia,” alisema.
Mpina aliahidi kuongeza mapato ya Serikali mara tatu zaidi.
“Wale waliozoea kufuja mali za umma, kuiba na kufanya ubadhirifu, nitakuja na mbadala wa kumwajibisha mwenye jukumu la kuchukua hatua.
“Watanzania wanipe dhamana, wizi huu, utoroshaji wa fedha za umma utafika mwisho, kama kuna watendaji wanaona hawawezi kuacha basi siku wakisikia naapishwa wajiondoe kabisa mana watakiona cha mtema kuni,” alisema.
Mpina aliahidi kuboresha hospitali na shule nchini ili viongozi wakiwamo wabunge waache kuzinyanyapaa hospitali zao kwa kwenda kutibiwa nje ya nchi pamoja na kutowasomesha watoto wao katika shule za Serikali.

CHIFU WA RUNGWE AMPIGIA DEBE MAKONGORO

CHIFU wa Wilaya ya Rungwe, Prince Mwaihojo amesema Makongoro Nyerere ni kiongozi mzuri ambaye ameonekana kuwa na uwezo mkubwa wa kuwaunganisha watu.
Aliyasema hayo jana wilayani Rungwe, Mbeya wakati Makongoro – mtoto wa tano wa Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alipokwenda kutafuta wadhamini watakaomdhamini kwenye nafasi ya urais.
“Nchi ilivyo sasa imekosa kiunganishi, ukiangalia wagombea wote wanajinadi kwa kufuata sera za Baba wa Taifa na hiyo inatokana na chama kupoteza dhana nzima ya kuwa chama cha wafanyakazi na wakulima, na badala yake kugeuka na kuwa chama cha walanguzi,” alisema.
Alisema Makongoro anaweza kuifanya kazi ya kurudisha amani na upendo kwa asilimia 60 kutokana na mtaji wa baba yake, huku asilimia 40 ni kutokana na uadilifu na uzoefu katika siasa.
Naye Makongoro ambaye ni Mbunge wa Afrika Mashariki, akizungumza na umati mkubwa wa wafuasi wa CCM, aliwataka wakazi wa Mkoa wa Mbeya kuhakikisha wanamuunga mkono na kumchagua kuwa rais wa Tanzania.

MANGULA : MATENDO YA WATANGAZA NIA YANAREKODIWA

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Philip Mangula, amesema vitendo vyote vinavyofanywa na wagombea wa urais ndani ya chama hicho wakati huu wanapotafuta wadhamini vinaingia katika rekodi ya chama.
Mbali na hilo, aliwataka wanachama wa chama hicho kutambua mchakato wa kugombea au kuwapata wagombea kwa nafasi ya udiwani, ubunge na uwakilishi bado haujaanza.
Mangula, alitoa kauli hiyo mjini Dodoma jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mchakato unaoendelea sasa ndani ya CCM wa kumpata mwanachama atakayegombea urais wa Jamuhuri ya Muungano na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Alisema rekodi hizo zitatumika katika mchakato wa uteuzi wa wagombea hao ambapo majina matano ndiyo yatateuliwa kwa ajili ya kwenda kupigiwa kura katika kikao cha Halmashauri Kuu (NEC).
“Vikao vya uteuzi vitafanyika kwa kutumia kanuni za uteuzi wa wagombea wa CCM katika vyombo vya dola na kanuni za viongozi na maadili za chama chetu,” alisema.
Kanuni hizo pamoja na mambo mengine zinaeleza mambo ya kuzingatia kwa wagombea na pia zinaeleza sifa za mgombea wa urais.
“Kwa mujibu wa Kanuni ya Uteuzi kifungu cha 20(5) kutangaza nia kunaruhusiwa ila ni marufuku kwa mgombea au wakala wake kufanya vitendo vinavyoonekana ni kufanya kampeni kabla ya muda,” alisema.
Alisema kifungu za 20 cha Kanuni za Uteuzi, kinasema kwamba maadili na nidhamu ya chama katika kusimamia na kutekeleza shughuli za uteuzi wa wagombea wa CCM katika vyombo vya dola lazima vizingatiwe na wale wote wanaohusika.
Mangula alisema kanuni hiyo pia inapiga marufuku wagombea kutumia ukabila, dini, rushwa, rangi, hila na eneo analotoka katika shughuli ya uchaguzi.
“Ni mwiko pia kwa mgombea kufanya kampeni za kupakana matope na ya aina nyingine yoyote dhidi ya mgombea mwingine, ni mwiko kwa mgombea aliyekabidhiwa dhamana ya usimamizi, uchujaji na uteuzi kufanya vitendo vya ukiukwaji wa kanuni,” alisema Mangula.
Alisema kanuni hizo zinaeleza sifa 13 za mgombea wa urais ambazo vikao vya uteuzi vitazingatia sifa hizo wakati wa mchujo wa wagombea.
“Baadhi ya sifa hizo, ni pamoja na awe na elimu kuanzia chuo kikuu, awe na upeo wa kudumisha na kuendeleza muungano na asiwe mwenye hulka ya udikteta,” alisema.
Alizitaja sifa nyingine kwamba awe mtetezi wa wanyonge, asiwe na tamaa ya kujitafutia umaarufu, mpenda haki, asitumie nafasi yake kujilimbikia mali, awe na uwezo wa kuilinda katiba, sheria za nchi na utawala bora, atambulike na wananchi na awe na uwezo wa kusimamia majukumu ya utendaji na uwajibikaji.
Alisema wagombea wote watapimwa kwa sifa hizo katika vikao vya mchujo.
Kwa upande wa nafasi za udiwani, ubunge na uwakilishi, Mangula alisema mchakato wa kuwapata wagombea wa nafasi hizo ndani ya chama bado haujaanza.
“Hivyo napenda kuwaambia wenye nia ya kugombea nafasi hiyo wajiepushe na vitendo vitakavyoonekana ni kufanya kampeni.
Taarifa hizi zimeandaliwa na Pendo Fundisha (Mbeya), Debora Sanja (Dodoma), Is-haka Omar (Zanzibar) na Elias Msuya (Pemba)

CHANZO: MTANZANIA

No comments:

Post a Comment