Monday, June 8, 2015

CHADEMA Wamtaka Mwandosya Ajiunge UKAWA


NAIBU Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Zanzibar, Salim Mwalim, amesema Profesa Mark Mwandosya, ajiunge na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ili awe mshauri kuliko kuendelea kuwepo CCM.
 
Akizungumza jana kwenye mkutano wa hadhara aliofanya katika Jimbo la Rungwe Mashariki linaloongozwa na Mwandosya, alisema CCM imekosa mwelekeo hivyo msomi kama Mwandosya hatakiwi kuwa katika chama hicho.

Alisema japo mbunge huyo alisema hatagombea tena jimbo hilo la Rungwe Mashariki, kinachotakiwa ni kukihama chama hicho na kujiunga na Ukawa ili awe mshauri wa Umoja huo.

“Mwandosya ni msomi mkubwa sana hivyo kutokana na elimu yake aliyonayo, anatakiwa kutoka CCM na kujiunga na Ukawa ili awe mshauri wetu na sio kuendelea kubaki na CCM,” alisema Mwalim.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Mbeya, Joseph China, alisema wananchi wanatakiwa kujiandikisha ili kuweza kupata haki yao ya msingi ya kupiga kura.

China alisema njia pekee ya kuweza kuishinda CCM ni wananchi kujiandikisha kwa wingi na kuhudhuria siku ya kupiga kura.

Alisema katika kata hiyo ya Kandete kumekuwepo na tatizo la kutokuwepo kwa diwani hivyo michango imekuwa ikichangishwa kiholela na watendaji wa vijiji na kata bila kujua matumizi ya hizo fedha.

No comments:

Post a Comment