Mhasibu feki atiwa mbaroni kwa wizi wa Tsh. 873,000
Na Nathaniel Limu, Singida
Mhasibu
wa hospitali ya mkoa mjini Singida aliyeachishwa kazi kwa kosa la
kumiliki vyeti feki, Edith Talasi (49) mkazi wa Minga,anashikiliwa na
jeshi la polisi kwa tuhuma ya kuvunja milango ya ofisi yake ya zamani na
kuiba shilingi 873,000 taslimu, kwa kutumia funguo bandia.
Talasi
ambaye imelelezwa kwamba alifanya kazi hospitalini hapo kwa muda na
baadaye alirejeshwa kwenye kituo chake cha kazi manispaa ya
Singida,kwenye wizi huo, alimshirikisha mlinzi wake wa nyumba ya kulala
wageni Nandau, Antony Felix (51).Mlinzi huyo naye anashikiliwa na
polisi.
Akizungumza
na waandishi wa habari ofisini kwake Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani
hapa, ACP Debora Magiligimba, alisema tukio hilo limetendeka Novemba, 21
saa 6.30 usiku huko katika hospitali ya mkoa mjini hapa.
Alisema
siku ya tukio muuguzi wa zamu Shamir Omari (27) akitokea maeneo ya
mapokezi akielekea wodini, alimwona mtu akiwa amesimama karibu na ofisi
ya mhasibu, alisimama akamsalimia na mtu huyo aliondoka.
“Muuguzi
huyo aliamini kuwa mtu aliyemwona,huenda alikuwa mgonjwa au mtu
aliyeleta mgonjwa hospitalini.Lakini aliporudi,alimwona mtu yule yule
amerudi eneo lile lile, kitendo kilichopelekea amshuku kuwa sio mtu
mzuri,” alisema kamanda huyo.
Alisema
muuguzi huyo baada ya kumtilia shaka mtu huyo, alitoa taarifa kwa
mlinzi wa zamu wa hospitali hiyo, Abubakari Jumanne,ambaye alimweka
chini ya ulinzi mtu huyo.
ACP
Magiligimba alisema hata hivyo mtu huyo alijitetea kuwa amefika
hospitalini hapo, kwa ajili kuchoma sindano na kuonyesha dawa ya unga na
kichanganyio chake.
“Wakati
wanaendelea na mahojiano hayo,waliona makufuli mawili ya mlango wa
nje/grili yapo chini na mlango huo wa chuma upo wazi. Mtuhumiwa mlinzi
Antony alieleza kuwa bosi wake (mtuhumiwa Edith) kwa wakati huo,alikuwa
ndani ya ofisi ya mhasibu amejifungia ndani,” alisema.
Akifafanua
alisema jeshi la polisi baada ya kupata taarifa ya wizi huo, liliweza
kufika eneo la tukio na kukuta mlango wa ndani ukiwa umefungwa kwa
ndani.
“Walipoamuru
mhasibu afungue mlango huo kwa kutumia funguo zake,walimkuta mtuhumiwa
(Edith) akiwa amejibanza kwenye kona ya mlango na watumishi wa hospitali
hiyo, waliweza kumtambua. Alipohojiwa ameingiaje humo ndani,alionyesha
funguo saba (07) na zilipojaribiwa ziliweza kufungua milango yote ya
ofisi ya mhasibu,” alisema Magiligimba.
Alisema
pamoja na wizi huo wa shilingi 873,000,imeelezwa kwamba aprili mwaka
huu,wahasibu wa hospitali hiyo,walibaini upotevu wa shilingi
1,800,000.Oktoba mwaka huu,pia walibaini upotevu wa shilingi 3,600,000.
Kaimu
mganga mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk. David Mwasita,amekiri kutokea
upotevu huo lakini wahasibu katika wakati huo,waliweza kuziba upotevu
huo, kwa fedha zao za mishahara.
Ameeleza
kuwa wahasibu hao walilazimika kutoa fedha zao binafsi, na wasingeweza
kutoa taarifa ya upotevu huo, kwa vile milango na kasiki, ilikuwa
imefungwa kama kawaida.
ACP
Magiligimba amesema kwa sasa wanaendelea kuwahoji watuhumiwa hao na
baada ya kumalizika kwa mahojiano hayo,watuhumiwa watafikishwa
mahakamani kujibu tuhuma inayowakabili.