Tuesday, May 5, 2015

Mtoto wa Miaka 8 Auawa na Mbwa


Aisha Ally mwenye umri wa miaka 8 (pichani), mkazi wa Mtaa wa NSSF, Mbezi Beach jijini Dar es Salaam ambaye pia alikuwa mwanafunzi wa darasa la tatu  wa Shule ya Msingi ya St. Joseph, Dar, amefariki dunia baada ya kung’atwa na mbwa anayedaiwa kuwa na kichaa.

Tukio hilo lilijiri hivi karibuni nyumbani kwao Mbezi wakati mtoto huyo alipotumwa na mama yake mkubwa kwenda dukani kununua vocha ya simu.Akisimulia tukio zima kwa waandishi wetu, baba mzazi wa marehemu, Ally Ayub alisema:
 
“Siku ya tukio mwanangu alitumwa na mama yake mkubwa kwenda dukani kumnunulia vocha, sasa wakati anarudi nyumbani njiani alikutana na mbwa huyo akamshambulia kwenye mguu wa kushoto, mkono wa kushoto na mdomoni.
 
“Mwanangu alijitahidi kupambana naye ili kujiokoa lakini mbwa naye alikuwa na nguvu, akamng’ata sehemu hizo.”
 
“Baadhi ya watu waliokuwepo dukani waliona, wengine walianza kulia baada ya kumtambua mwanangu, wengine  walikimbilia eneo la tukio kwa lengo la kumwokoa, mmoja wao alimpiga teke yule mbwa akatokomea kusikojulikana.
 
“Ndipo yule mtu aliyempiga teke mbwa na watu wengine walimleta mwanangu nyumbani akiwa anavuja damu sehemu alizong’atwa. Niliumia sana! Na bado  nikikumbuka naendelea kuumia.”
 
Mzazi huyo alisema kwamba, kabla ya kumkimbiza hospitali Aisha, alimpaka dawa aina ya spiriti kwa lengo la kumkausha damu.Aliendelea kusema: 
 
“Baada ya hapo tulimkimbiza Hospitali ya Muhimbili, tulipokelewa vizuri lakini cha ajabu hata dawa aina ya yuso tuliambiwa tukanunue nje jambo lililotusikitisha sana.
 
“Shida kubwa ilikuwa ni mtoto wangu atibiwe hivyo jirani yangu aliyenisaidia gari pamoja na kunisindikiza, alikwenda kununua hiyo yuso, akapakwa na kuchomwa sindano moja, akafungwa majeraha kisha tukaambiwa turudi nyumbani na kupangiwa tarehe nyingine ya kurudi.”

Akiendelea kusimulia mkasa huo kwa masikitiko makubwa huku machozi yakimtiririka, mzazi huyo alisema:
 
“Kumbe kiutaratibu mwanangu alipaswa achomwe sindano nyingine baada ya saa 72 kitu ambacho hakikufanyika wala kushauriwa na wataalam wa hospitali hiyo.
 
“Baada ya kurudi nyumbani tulishauriana na mke wangu kwamba mwanangu akakae kwa shangazi yake Kibamba kutokana na shughuli zetu kutofautiana, hivyo muda wa kukaa na mtoto mgonjwa ulikuwa finyu.”
 
“Siku chache baadaye nikiwa safarini, nilipigiwa simu na mke wangu, akaniambia amepigiwa simu na wifi yake (Salima) na kumwambia kwamba, Aisha anaumwa.
 
“Alisema alimpeleka hospitali akapimwa na kukutwa ana malaria 2 hivyo alianzishiwa dozi ya dawa ya mseto.
 
“Siku mbili mbele nikiwa nimerejea kutoka safari, shangazi wa mtoto alinipigia simu na kunifahamsha kwamba Aisha alikuwa anashtukashtuka.
 
“Kesho yake nilikwenda kumchukua, nikampeleka Muhimbili kwa maana ya kutibiwa. Ilikuwa majira ya saa sita mchana, akalazwa Wadi B, Chumba J, Jengo la Watoto kisha akapewa vidonge vya kutuliza maumivu.”
 
“Kesho yake saa sita usiku, siku ya Ijumaa hali ya mtoto wangu ilizidi kuwa mbaya, akawekewa dripu lakini hali iliendelea kuwa mbaya, akahamishiwa Chumba I ambako tulikaa naye kwa takriban saa moja tu, akafariki dunia.” Machozi yakamtoka.Marehemu Aisha alizikwa saa 9 alasiri Aprili 27, mwaka huu kwenye Makaburi ya Ngazija yaliyopo Kisutu jijini Dar.
Credit: Uwazi/Gpl

Picha 8 za Mwenyekiti wa ‪ CHADEMA‬ Freeman Mbowe Alivyoungana na DC wa Kinondoni Paul Makonda Kutatua Mgomo wa Mabasi leo Ubungo Dar es salaam

Mpekuzi blog
Mwenyekiti wa chama cha demokrasia na maendeleo CHADEMA mh Freeman Mbowe aliwasili leo katika stend ya mabas ubungo kuzungumza na madereva ambao walikuwa wakiendelea na mgomo na kuitaka serikali iwasikilize shida zao.
 
Mbowe ambaye aliwasili  majira ya saa nne kasoroo asubuhi alijikuta katika wakati mgumu baada ya wananchi kumshangilia kwa nguvu huku wengine wakifuta barabara ili gari yake ipite huku nyimbo za Ukawa zikiimbwa,jambo ambalo lilizua taharuki katika eneo hilo.

Kuhusu mgomo huo mkuu wa wilaya ya Kinondoni mh PAUL MAKONDA aliwaomba madereva hao kuendelea na kazi na ndani ya siku saba serikali itakua tayari imeshatoa tamko.

Madereva hao wamekubali kuanza safari kwa sharti la ndani ya siku saba wawe wamesikilizwa kero zao.








Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Jumatano Tarehe 6 May 2015

























Mgombea Urais Chadema Kupatikana Agosti


CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kinatarajia kumpata mgombea wake wa urais Agosti 4, mwaka huu.
 
Kupatikana kwa mgombea huyo kutatokana na uamuzi wa mkutano mkuu wa taifa, ambacho ndio chombo cha juu cha uamuzi.
 
Kauli hiyo ilitolewa jijini Dar es Salaam jana na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, wakati akitangaza kwa waandishi wa habari uamuzi wa kikao cha Kamati Kuu kilichoketi kwa siku mbili.
 
Alisema pamoja na mambo mengine kikao hicho kilijadili ratiba ya kuwapata wagombea wa udiwani, ubunge na urais ambao utaratibu wa kuwapata utaanza Mei 18 hadi Agosti 4.
 
Kwa mujibu wa ratiba hiyo, uchukuaji na urejeshaji wa fomu kwa ngazi ya udiwani utaanza Mei 28 hadi Juni 25.
 
“Julai Mosi hadi 10 itakuwa ni kuchukua na kurejesha fomu kwa kata ambazo tuna madiwani na Julai 15 hadi 20 utakuwa uteuzi wa mwisho wa wagombea udiwani wa kata pamoja na wale wa viti maalumu.
 
“Mei 18, hadi Juni 25 itakuwa ni kuchukua na kurejesha fomu za ubunge kwa majimbo ambayo hatuna wabunge kwa sasa pamoja na viti maalumu, na Julai 6 hadi 10 ni uchukuaji na urejeshaji fomu za ubunge kwa majimbo ambayo tuna wabunge kwa sasa.
 
“… Julai 20 hadi 25 ni uteuzi wa awali kwa wagombea ubunge kazi itakayofanywa na Kamati tendaji za majimbo. Hata hivyo pia Julai 20 hadi 25 ni kuchukua na kurejesha fomu za mgombea urais ambazo zitasimamiwa na Makao Makuu,” ilionyesha ratiba hiyo iliyotolewa na Chadema.
 
Pamoja na mchakato huo, Chadema imesema kuwa uteuzi wa mwisho wa wagombea ubunge utafanyika Agosti 1-2 kazi ambayo itafanywa na Kamati Kuu ya chama hicho.
 
“Agosti 3, mwaka huu kitaketi kikao cha Baraza Kuu chini ya utaratibu wa Kamati Kuu na Agosti 4 utafanyika Mkutano Mkuu wa Taifa ambao utafanya kazi ya kuchagua mgombea urais kwa mujibu wa Katiba ya Chadema,” alisema Mbowe.
 
Akizungumzia kuhusu maazimio ya kikao cha Kamati Kuu, Mbowe alisema wamepokea, kujadili na kukubaliana makubalino yaliyokwishafikiwa na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
 
Ukawa – umoja ulioanzishwa Februari mwaka jana ukiwa ni kikundi shinikizi katika mchakato wa Katiba katika siku za mwanzo za Bunge Maalumu la Katiba, inaundwa na vyama vya NCCR-Mageuzi, Chadema, CUF na NLD.
 
Kuhusu Uchaguzi Mkuu, Mbowe alisema wamebaini Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Serikali hawana dhamira ya dhati ya kisiasa wala maandalizi ya kutosha yakiwamo matakwa ya kisheria, kitaalamu na kibajeti ili kuhakikisha unafanyika kwa mujibu wa Katiba.
 
Kuhusu kura ya maoni ya Katiba Inayopendekezwa, alisema baada ya kujadili kwa kina wamebaini kuna haja kura hiyo isogezwe mbele hadi baada ya kumalizika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.