UMOJA WA KATIBA YA WANANCHI (UKAWA),
DAR ES SALAAM,
TANZANIA.
TAARIFA KWA UMMA,
DAR ES SALAAM, ALHAMIS, 30 APRIL 2015
UCHAGUZI MKUU OKTOBA 2015 LAZIMA, KIKWETE ASIONGEZEWE MUDA, KURA YA MAONI BAADAE
Vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) leo vimetoa
msimamo wao juu ya njama za kuahirisha Uchaguzi Mkuu unaotakiwa
kufanyika Oktoba mwaka huu. UKAWA imesisitiza kwamba kuahirisha Uchaguzi
Mkuu huo ni sawa na kumuongezea Rais Jakaya Kikwete na Chama chake cha
Mapinduzi muda wa kuendelea kutawala Tanzania. UKAWA imesema jaribio
lolote la kuahirisha Uchaguzi Mkuu kwa kisingizio chochote kile litakuwa
kinyume na Katiba ya sasa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
litahesabika kuwa ni sawa na mapinduzi dhidi ya Katiba (constitutional
coup d’etat). Msimamo wa UKAWA unafuatia kumalizika kwa Kikao cha
Viongozi Wakuu wa Vyama vinavyounda UKAWA (UKAWA Summit) kilichofanyika
katika Makao Makuu ya Chama cha Wananchi (CUF), jijini Dar es Salaam
kati ya tarehe 28 na 29 Aprili mwaka huu.
Akielezea msimamo wa UKAWA juu ya suala hili, mwenyeji wa Kikao hicho na
Mwenyekiti wa CUF Profesa Ibrahim Lipumba alisema kwamba kuna dalili za
kuonyesha kwamba zipo njama za kuahirisha Uchaguzi Mkuu na kumuongezea
Rais Kikwete na CCM muda wa kutawala. “Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)
haijaanza maandalizi yoyote kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu licha ya kwamba
imebaki miezi sita tu Uchaguzi huo ufanyike kwa mujibu wa Katiba.
Shughuli zinazohusiana na maandalizi ya Uchaguzi Mkuu na vifaa
vinavyotumika kwa ajili yake ambavyo kwa taratibu za miaka yote huanza
kufanyika angalau mwaka mmoja na nusu kabla ya Siku ya Uchaguzi
hazijaanza kufanyika, vifaa vinavyohitajika havijanunuliwa na fedha kwa
ajili hiyo hazijatengwa hadi sasa.”
Profesa Lipumba aliongeza kwamba jambo hili limefanyika kwa makusudi kwa
sababu vyama vya UKAWA vimekuwa vinapigia kelele suala la maandalizi ya
Uchaguzi Mkuu tangu mwaka 2012. “Licha ya madai ya muda mrefu ya Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni kwamba ratiba ya Uchaguzi Mkuu wa 2015
imevurugwa kwa makusudi kwa kutokutenga fedha kwa ajili hiyo katika
bajeti ya Serikali tangu mwaka 2012, Serikali hii ya CCM haijatoa fedha
kwa NEC kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu. Badala yake, NEC imeendelea
kutangaza kwamba inafanya maandalizi kwa ajili ya Kura ya Maoni kuhusu
Katiba Inayopendekezwa ambayo imepitwa na muda kisheria na haiwezi
kufanyika tena bila kwanza kufanyika kwa marekebisho katika Sheria ya
Kura ya Maoni (the Referendum Act) ya mwaka 2013.”
Kwa mujibu wa Profesa Lipumba, Kura ya Maoni ilitakiwa ifanyike ndani ya
siku 124 kutoka tarehe Rais Kikwete alipotoa Tangazo la Kura ya Maoni
na kutamka kuwa Kura hiyo itafanyika tarehe 30 Aprili, 2015, yaani leo.
Profesa Lipumba alisema: “Kwa Sheria ya Kura ya Maoni ilivyo kwa sasa,
hakuna uwezekano wa Kura ya Maoni kufanyika tena bila kwanza kufanya
marekebisho ya Sheria hiyo. Kila hatua inayotakiwa kuchukuliwa chini ya
Sheria hiyo imewekewa muda wake na muda huo haubadiliki. Tangazo la Kura
ya Maoni likishatolewa na tarehe kutangazwa haibadilishwi kwa sababu
yoyote ile. Hakuna namna yoyote ya kuahirisha Kura ya Maoni na kuifanya
tarehe nyingine yoyote.”
Profesa Lipumba aliongeza: “Haya ndio masharti ya Sheria ya Kura ya
Maoni. Yasipofuatwa hakuna namna ya kuyarekebisha bila kwanza
kurekebisha Sheria yenyewe. Na hadi sasa Serikali hii ya CCM haijapeleka
Muswada wa Sheria kuirekebisha Sheria hiyo ili kuwezesha Kura ya Maoni
kufanyika kwa tarehe nyingine. Tunashangazwa na Tume inayoongozwa na
aliyekuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani ambayo ndio mahakama ya juu kabisa
katika nchi yetu, na Mkurugenzi wa Uchaguzi ambaye ni Mwanasheria
Mwandamizi wa Serikali, kuendelea kutangaza kwamba Kura ya Maoni
itafanyika kwa terehe itakayotangazwa baadae wakati Tume inafahamu
kwamba jambo hilo haliwezekani kisheria. Kama bado CCM na washirika wake
wanataka Katiba Inayopendekezwa ipigiwe Kura ya Maoni na Watanzania ni
lazima wapeleke Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Kura ya Maoni
Bungeni. Vinginevyo itakuwa na ubatilifu mtupu kama tuliouona wakati wa
Bunge Maalum.”
Aidha, UKAWA imesema haiko na haitakuwa tayari kuunga mkono jitihada
zozote za kumuongezea Rais Kikwete na CCM muda wa kutawala kwa
kuahirisha Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu. Kwa mujibu wa Mwenyekiti Mwenza
wa UKAWA na Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, Mheshimiwa James
Mbatia, haijawahi kutokea Uchaguzi Mkuu ukaahirishwa kwa sababu yoyote
tangu mwaka 1960 tulipofanya Uchaguzi Mkuu uliotupatia Serikali ya
Madaraka ya Ndani hadi sasa.
Mheshimiwa Mbatia alisema: “Watu hawa wanafahamu kuwa tumekuwa tukifanya
Uchaguzi Mkuu kila baada ya miaka mitano tangu mwaka 1960. Hata mwaka
1980, miezi michache baada ya kutoka vitani dhidi ya nduli Iddi Amin wa
Uganda na licha ya Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere kutangaza miezi 18 ya
kujifunga mikanda kwa sababu ya hali mbaya ya uchumi iliyosababishwa na
Vita ya Uganda, hatukuahirisha Uchaguzi Mkuu wa mwaka huo. Watu hawa
wanafahamu kwamba Katiba yetu hairuhusu Uchaguzi Mkuu kuahirishwa kwa
sababu yoyote ile.
Wanafahamu kwamba tangu mwaka 1985, Rais anatakiwa atumikie vipindi
viwili tu vya miaka mitano mitano. Wanafahamu kwamba maisha ya Bunge ni
miezi sitini au miaka mitano kuanzia tarehe ya Uchaguzi Mkuu na
haiwezekani kwa maisha hayo kuongezewa muda kikatiba bila ya kufanyika
Uchaguzi Mkuu. Na wanafahamu kwamba Rais Kikwete anakamilisha kipindi
chake cha pili mwezi Oktoba mwaka huu na maisha ya Bunge la Kumi
yanamalizika mwezi huo. Kuruhusu Uchaguzi Mkuu uahirishwe kwa kisingizio
chochote kile ni kuwazawadia wazembe na kuwaongezea mafisadi
wanaolimaliza taifa letu kwa ufisadi muda wa kuendelea na ufisadi huo.
UKAWA haitakubali kuruhusu jambo hilo litokee.”
Aidha, UKAWA imesisitiza kwamba haitakubali na haitaunga mkono jaribio
lolote la kufanya marekebisho katika Katiba ya sasa kwa lengo la
kumuongezea Kikwete, chama chake na Serikali muda wa kutawala. Akielezea
msimamo huo, Mwenyekiti Mwenza wa UKAWA na Mwenyekiti wa chama cha
National League for Democracy (NLD) Dkt. Emmanuel Makaidi amesisitiza
kwamba suala la vipindi viwili vya miaka mitano mitano kwa Rais wa
Jamhuri ya Muungano ni nguzo kuu muhimu ya Katiba ya sasa na UKAWA
haitakubali nguzo hiyo iguswe au kufumuliwa kwa sababu au kisingizio
chochote kile. Dkt. Makaidi alisema: “Kubadilisha Katiba ya sasa kwa
lengo la kuahirisha Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka sio tu kutaathiri
misingi muhimu ya Katiba ya sasa, bali pia kutahatarisha amani ya nchi
yetu. Tumeona kinachoendelea Burundi baada ya Rais Pierre Nkurunzinza na
chama chake kuamua kujiongezea muda wa kutawala nchi hiyo. Tumeona
yanaoendelea Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) baada ya Joseph
Kabila kutaka kufanya hivyo hivyo. Kikwete na wanaCCM wenzake wasitake
kuiingiza nchi yetu katika majanga yasiyokuwa na sababu.”
Kwa upande mwingine, UKAWA imeitaka NEC kuhakikisha kwamba wananchi wote
wenye sifa ya kuandikishwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura
wanaandikishwa kwenye Daftari hilo. Katika Mkutano wake na vyama vya
siasa uliofanyika Dar es Salaam tarehe 9 Julai mwaka jana, Mwenyekiti wa
Tume Jaji Damian Lubuva alisisitiza kwamba NEC ilikuwa na uwezo na
vifaa vya kuandikisha takriban wapiga kura milioni 24 katika vituo vya
kuandikishia 40,000 nchi nzima kwa muda wa siku 14 katika kila kituo cha
kuandikishia. Mwenyekiti Mwenza wa UKAWA na Mwenyekiti wa CHADEMA
Mheshimiwa Freeman Mbowe alieleza kushangazwa kwa UKAWA na matamko ya
Tume kwamba sasa Tume itaandikisha wapiga kura kwa muda wa siku saba
katika kila kituo.
Mwenyekiti Mbowe alisema: “Tume iliwaahidi Watanzania kwamba watu wote
wenye sifa wataandikishwa katika Daftari la Wapiga Kura. Sisi wa UKAWA
tulishauri muda wa kuandikisha uongezwe hadi angalau siku 28 kama
ilivyokuwa kwa Uchaguzi Mkuu uliopita lakini Tume iling’ang’ania kwamba
muda wa siku 14 unatosha. Leo Tume inapunguza muda huo wakati tunafahamu
kwamba Tume ina vifaa pungufu vya kuandikishia wapiga kura kuliko
ilivyoomba kupatiwa na Serikali hii ya CCM. Hii ni njama ya Tume na ya
Serikali hii ya CCM kuhakikisha wapiga kura wengi hawaandikishwi. Sisi
UKAWA hatutakubali jambo hilo litokee.”
Wakati huo huo, Viongozi Wakuu wa UKAWA wameeleza kushangazwa na taarifa
zilizosambazwa na baadhi ya vyombo vya habari hapa nchini kwamba Chama
cha NCCR-Mageuzi kimejitoa au kimeandika barua ya kuomba kujitoa kwenye
UKAWA. Viongozi hao wamesema kwamba taarifa hizo ni uzushi mtupu
unaosambazwa na wapiga ramli na wanajimu wa kiama cha UKAWA kwa lengo la
kuipatia CCM na vyama vibaraka wake ahueni ya kisiasa. Akikanusha
taarifa hizo, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi Mheshimiwa Mbatia amesema
kwamba yeye mwenyewe na Katibu Mkuu wake Mosena Nyambabe pamoja na
maafisa wa chama chake wamekuwa katika hatua zote za vikao vya UKAWA
kuanzia Kamati ya Ufundi na ile ya Wataalam hadi Kikao cha Viongozi
Wakuu kilichomalizika jana.
Mheshimiwa Mbatia alisisitiza: “Tangu juzi tupo hapa tukijadiliana namna
ya kupata wagombea wa UKAWA wa ngazi zote kuanzia Urais, Ubunge hadi
Udiwani. Kwa kiasi kikubwa tumeshakamilisha kazi ya kupata wagombea
Ubunge wa UKAWA. Tumeshapata muafaka kwa zaidi ya asilimia 95 ya majimbo
yote ya Uchaguzi Tanzania, na majimbo 12 yaliyobakia tunaendelea
kuyashughulikia na tutayapatia ufumbuzi muda si mrefu. Tunaendelea na
majadiliano juu kupata Mgombea Urais na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano atakayepeperusha bendera ya UKAWA. Tumeshakamilisha kazi hiyo
kwa upande wa Zanzibar na tutaikamilisha kwa upande wa Jamhuri ya
Muungano katika muda muafaka. UKAWA iko imara sasa kuliko kipindi
kingine chochote tangu Bunge Maalum mwaka jana. Hao wanaosambaza uzushi
kwamba tumefarakana na kwamba sisi NCCR tumejitoa au tunataka kujitoa
watafute hoja nyingine. Hii imebuma.”
Mungu Ibariki Tanzania!
Imetolewa na;
---------------------------------------
Prof. Ibrahim Haruna Lipumba,
Mwenyekiti – CUF – Chama Cha Wananchi,
-----------------------------------
Mh.Freeman Mbowe (MB),
Mwenyekiti - CHADEMA
--------------------------------------
Mh.James Francis Mbatia(MB),
Mwenyekiti – NCCR MAGEUZI.
--------------------------------------
Mh. Dkt. Emmanuel Makaidi
Mwenyekiti – NLD.