Friday, April 8, 2016

KATIBU Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, ameanza rasmi azma yake ya kutoshiriki mikusanyiko ya kitaifa, ikiwa hatua ya kutekeleza msimamo wa chama chake wa kutoitambua Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, inayoongozwa na Dk. Ali Mohamed Shein.

Maalim Seif alifanya hivyo, baada ya kususia hitima ya kumkumbuka Sheikh Abeid Amani Karume, aliyeuawa Aprili 7, 1972 na wapinga maendeleo.

Mkusanyiko wa viongozi wa kitaifa ulianza saa tatu asubuhi na kuhudhuriwa na Rais Dk. Shein na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli, aliyewakilishwa na Makamu wa Rais, Samia Hassan Suluhu.

Wengine waliokuwapo ni Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi, Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi, Rais mstaafu wa Zanzibar, Dk. Amani Abeid Karume, Waziri Mkuu mstaafu Dk. Salim Ahmed Salim na Makamu wa Rais mstaafu, Dk. Mohamed Gharib Bilal.

Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Abdallah Mwinyi Khamis, alisema viongozi wote wastaafu walipewa mialiko akiwaemo Maalim Seif lakini hadi shughuli hiyo inamalizika, hakutokea ikiwa ni mara ya pili baada ya kususia sherehe za miaka 52 ya Mapinduzi zilizofanyika Januari 12, mwaka huu.

“Viongozi wote wana mialiko maalum. Hata Maalim Seif amepata mwaliko wake, lakini suala la kuhudhuria au kutohudhuria ni hiari ya mwalikwa mwenyewe” alisema.

Msemaji wa CUF, Hamad Masoud, alisema hafahamu kama Maalim Seif amealikwa katika hitima hiyo, lakini anakumbuka mwaliko alioupokea ni ule wa uzinduzi wa Baraza la Wawakilishi, lakini kutokana na msimamo wa CUF hakuna kiongozi aliyehudhuria kutokana na kutoitambua Serikali ya Dk. Shein.

Hata hivyo, alisema Maalim Seif yuko Zanzibar tangu kukamilika kwa vikao vya baraza kuu la uongozi na kutoa msimamo wa kutoitambua serikali iliyoko madarakani, kupingia kufanyika kwa uchaguzi wa marudio baada ya ule wa Oktoba 25, mwaka jana, uliofutwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar(ZEC), Jecha Salim Jecha.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baada ya kukamilika kwa hitima hiyo, wanasiasa wakongwe Zanzibar na viongozi wa dini walisema wakati huu Zanzibar ikiwa katika mpasuko wa kisiasa, wananchi wanapaswa kulinda amani na umoja wa kitaifa katika kumuenzi Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Mzee Abeid Amani Karume.

Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Zanzibar, Augustino Shayo, alisema Karume atakumbukwa kutokana na tabia yake na mifano aliyoionesha katika uongozi wake. Alisema wakati wa uongozi wake, alisaidia watu masikini wawe na maisha bora.

Alisema ni jambo la kusikitisha wakati huu kumuenzi Karume, mwasisi wa Zanzibar huru, huku Zanzibar ikiwa na mpasuko mkubwa wa kisiasa.

Naye Balozi Ali Abeid Karume, mtoto wa Mzee karume, alisema CUF imefanya kosa kubwa kuwanyima haki wanachama wake kuchagua viongozi kwa vile wameingilia uhuru binafsi wa mtu kidemokrasia.

Aliwaasa wananchi kuendeleza ushirikiano kama hatua ya kumuenzi Mzee  Karume katika kujenga amani na umoja wa kitaifa kama alivyokuwa akipigania wakati wa uhai wake.

Viongozi wengine waliohudhuria hitima hiyo ni Spika wa Baraza la Wawakilishi, Zubeir Ali Maulid, Mufti wa Tanzania Abubakar Zubeir, Katibu wa Mufti wa Zanzibar Sheikh Fadhil Soraga, Spika wa zamani Pandu Ameir Kificho, na Mjane wa Rais Karume, Mama Fatma Karume.

Karume aliuwawa kwa kupigwa na risasi na mlinzi wake, Luteni Humud Mohamed Humud, wakati akicheza dhumna.

Alikuwa pamoja na aliyekuwa Katibu Mkuu wa ASP, Sheikh Thabit Kombo Jecha, ambaye alijeruhiwa kwa risasi, katika shambulio hilo lililofanywa na wapinga maendeleo wa Zanzibar.

No comments:

Post a Comment