MUME ACHINJA MKE WAKE KAMA KUKU,KISA " KAPATA WAPI PESA YA SALUNI"
HII
ni zaidi ya ukatili! Jiji la Tanga bado linazizima kufuatia mauaji ya
kutisha yanayodaiwa kufanywa na mwanaume aitwaye Khalfan Hamad (46),
dhidi ya mkewe, Mary Lucas (20) kwa kumchinja na panga kisa kikidaiwa ni
wivu wa mapenzi.
Tukio
hilo lililoacha simulizi ya kushangaza miongoni mwa wanandoa na
wanaotarajia kuingia, lilijiri Aprili 18, mwaka huu nyumbani kwa
mwanaume huyo, Mtaa wa Mapinduzi ‘A’ Kata ya Duga jijini hapa.
WANACHOKIJUA POLISI WA TANGA
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Tanga, ACP Zuberi Mwombeki alitangaza kwa waandishi
wa habari kwamba, mauaji hayo yalitokea saa nne na nusu asubuhi ya
Aprili 18 mwaka huu.
Alisema
chanzo cha tukio hilo ni wivu wa kimapenzi kati ya wawili hao ambapo
marehemu alimuomba mumewe pesa kiasi cha shilingi elfu kumi aende saluni
kutengeneza nywele lakini mwanaume akasema hana.
“Mwanaume
hakumpa pesa marehemu lakini baadaye alimkuta amesuka na ndipo ugomvi
ulipoanzia hapo hadi kutokea mauaji hayo,” alieleza kamanda huyo.
MAJIRANI WANASEMAJE?
“Jamani
sisi wenyewe tumeshtuka sana kwa kifo cha Mary, mimi nimeongea naye
akiwa anakwenda saluni na hata aliporudi. Kama angejua ndiyo siku yake
ya kufa naamini asingekwenda. Inauma sana!
“Mary
alitoka saluni akiwa amependeza maana alitengenezwa nywele vizuri sana.
Mimi mwenyewe nilimsifia. Kufika nyumbani kwake, mzozo ukaanza.
“Mumewe
alitaka kujua alikotoa shilingi elfu kumi ya kuendea saluni maana yeye
hakumpa. Mzozo ulikwenda hadi mwanaume akachukua panga na kumchinja.
Naamini ni wivu,” alisema jirani mmoja.
KUMBE WALIKUWA NA HISTORIA YA UGOMVI
Jirani
mwingine, Shaban Juma yeye alisema: “Hawa watu wameishi katika hali ya
kutoelewana na walikuwa wakigombana kila wakati, lakini hatukujua kama
litatokea hili kwani mara zote katika kugombana kwao, mwanaume ndiye
aliyekuwa akipigwa jambo ambalo liliwafanya watu wa karibu yake
kumshauri kuvunja uhusiano wao kulikoni aibu ya kupigwa na mke.”
Jennifer
Charles yeye pia ni jirani, alisema: “Siku ya tukio Mary alimwomba
mumewe hela ya kwenda kutengeneza nywele saluni lakini mume hakuwa na
pesa siku hiyo lakini baada ya kuondoka nyumbani, marehemu naye
alikwenda saluni.
“Baadaye
mume aliporudi nyumbani hakumkuta Mary lakini mara alirudi akiwa
ametengenezwa nywele jambo lililomfanya bwana kuhisi kuwa fedha hizo
amehongwa na mwanaume mwingine tofauti na yeye na hivyo kuzuka ugomvi
huo.”
MUME ALITOKA NJE AKITAMBA KUUA
Baada
ya Jennifer kumaliza kusimulia hayo, Juma Ally, naye ni jirani,
akaendeleza: “Hatukujua kilichoendelea katika mzozo wao, lakini baadaye
ukimya ulitawala. Muda mfupi mbele mume alitoka nje na kutuambia kwamba
ameshaua huko ndani kwani amechoka kupigwa na sasa amejibu mapigo.
“Kwanza tulijua anatutania lakini tulivyoona kimya kimezidi tukaamua kuingia ndipo
tulipomkuta
marehemu akiwa chini, akitoka damu nyingi. Tuliogopa kwa kweli. Mary
mrembo tunayemjua sisi, amelala chini na damu chapachapa.
“Alikuwa
ana majeraha makubwa sehemu ya shingo na kichwani yaliyotokana na
kupigwa na panga. Ilionekana panga lilikuwa kali sana na panga lenyewe
lilikuwa pembeni yake. Ndipo tulipoamua kumkimbiza Hospitali ya Mkoa,
Bombo ambapo alipoteza maisha wakati madaktari wakihangaika kuokoa uhai
wake.”
ASINGEKUFA MKE
Naye,
Fatuma Ramadhani alisema kutokana na ugomvi wa mara kwa mara kati ya
wawili hao na mwanaume kupigwa kila wakati, majirani waliamini siku moja
mume huyo ndiye angekuja kupata madhara hata kufa kutokana na
alivyokuwa akipigwa.
MTUHUMIWA KUPANDA MAHAKAMANI WAKATI WOWOTE
Kamanda Mwombeki alisema upelelezi unaendelea ili kuweza kumfikisha mahakamani mtuhumiwa huyo.
Marehemu Mary alizikwa katika eneo la Mwakizaro jijini Tanga, siku ya pili baada ya tukio hilo la kuhuzunisha.
No comments:
Post a Comment