Friday, May 1, 2015
Serikali yaipa Taboa wiki mbili, mgomo wasitishwa rasmi
Serikali imewapa Wamiliki wa Mabasi (Taboa) wiki mbili za kutafakari namna gani watapata hasara, iwapo watatumia nauli mpya zilizopendekezwa na Mamlaka ya Udhibiti na Usimamizi wa Usafiri wa Nchikavu na Majini (Sumatra).
Hatua hiyo imekuja baada ya wamiliki hao juzi
kutangaza kuwa wangeanza mgomo wa siku saba kuishinikiza Serikali
ibatilishe matumizi ya nauli mpya ilizozipitishwa kutokana na kushuka
kwa bei ya mafuta duniani.
Akizungumza jana, Katibu Mkuu wa Taboa, Enea Mrutu
alisema kuwa baada ya mazungumzo na katibu mkuu wa Wizara ya Uchukuzi
walifikia mwafaka huo na kwamba vielelezo hivyo vitakapokamilika
wataendelea na majadiliano.
“Tumepewa wiki mbili za kuandaa ushahidi wa namna
tutakavyopata hasara kwa matumizi ya nauli mpya tutaendelea na biashara
kama kawaida wakati tukilifanyia kazi suala hilo.
"Tutawapa vielelezo vya namna gharama nyinginezo zilivyopanda na kuathiri ustawi wetu,” alisema Mrutu.
Mrutu alifafanua kuwa kigezo kilichotumika
kushusha bei kilikuwa cha muda mfupi na hakikuzingatia mambo mengine
yanayoongeza gharama za biashara ya usafirishaji na kuitaka Serikali
kuanzisha ruzuku au kuondoa ushuru kwa vipuri vya vyombo vya safari.
“Ni kama walitaka kutukomoa hivi…kama mafuta
yameshuka bei kwa nini mabasi ya masafa marefu tu ndiyo yatakiwe
kupunguza nauli ilhali sekta nyingine zikiendelea kama kawaida,” alisema
na kuongeza:
“Daladala zinatumia mafuta kama ilivyo malori na
hata mashine za kusaga nafaka, lakini wao wameachwa. Unga haujashuka bei
wala gharama za kukodi lori hazijapungua pia.”
Baada ya taarifa za mgomo kusambaa, wasafiri wengi
walibadili ratiba zao huku baadhi ya mabasi yakisitisha uuzaji wa
tiketi kwa ajili ya safari za jana kabla ya saa mbili usiku taarifa za
kutokuwapo kwa mgomo huo kutolewa.
Hali hiyo ilisababisha mabasi mengi kuondoka na abiria wachache tofauti na siku nyingine.
“Ni lazima yaondoke hata kama yana abiria watano
kwa sababu yana wateja huko mikoani ambao ni lazima wasafiri kuja mjini
kesho, taarifa zisizo na uhakika ambazo zilikuwa zinabadilika, ndizo
zilizochangia hasara watakayoipata leo,” alisema Hussein Abdul mmoja wa
makarani katika stendi ya Ubungo.
Licha ya kuahirishwa kwa mgomo huo, kuanzia
alfajiri jana mpaka saa nne asubuhi wakati mabasi ya mikoani na nchi
jirani yakiendelea kuondoka, Jeshi la Polisi lilikuwa limeimarisha
ulinzi.
Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani katika stendi hiyo,
Inspekta Yusuf Kamotte alisema walifanya hivyo ikiwa ni tahadhari dhidi
ya wahuni ambao hutuma fursa kama hizo kufanya uhalifu.
“Jeshi lazima lijiridhishe hata kwa lolote
linalosemwa na kuonekana kuwa na dalili za kutokea kwa uhalifu. Wanaweza
wasiwe Taboa, lakini vibaka wangeweza kufanya yao dhidi ya abiria na
wapita njia,” alisema Inspekta Kamotte.
CHANZO Mpekuzi blog
No comments:
Post a Comment