Friday, May 1, 2015

HAO NDIO VIONGOZI WETU WANASEMA BAADA YA KUTOLEWA

Mzee Moyo: Nilitumwa Kumshawishi Seif Akubali Matokeo 2010.......Pamoja Na Kuifanya Kazi Hiyo, Tuzo Waliyonipa CCM ni Kunivua Uanachama


Mwanasiasa mkongwe aliyevuliwa uanachama wa CCM, Hassan Nassor Moyo (80) amesema yeye ndiye aliyefanya kazi kubwa, usiku kucha, kumshawishi Maalim Seif Sharrif Hamad, aliyekuwa mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF, akubaliane na matokeo ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2010 kabla ya hata kutangazwa.
 
Akizungumza katika mahojiano maalumu na mwandishi wa habari hizi nyumbani kwake Tanga siku chache baada ya Halmashauri Kuu ya CCM ya Mkoa wa Magharibi, Unguja kumvua uanachama, Moyo alisema alitumwa na Rais Amani Abeid Karume kufanya kazi hiyo kwa bidii, utiifu na uadilifu hadi akafanikiwa.
 
Moyo alifanya kazi mbalimbali akiwa waziri kwenye Baraza la Mapinduzi Zanzibar na akiwa waziri katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano katika maisha yake ya utumishi wa kisiasa, lakini akajikuta akipata tuzo ya kuvuliwa uanachama wa CCM akiwa ameshastaafu siasa kwa madai ya kuhudhuria mikutano ya hadhara ya CUF.
 
Moyo alisema kuwa Mohamed Riyami, ambaye ni mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Maridhiano, alikwenda nyumbani kwake na kumpa ujumbe huo kutoka kwa Rais Karume, na baada ya majadiliano naye, alikubali.
 
“…Ni kweli Mohamed Riyami alikuja kuniamsha saa 10:00 alfajiri hivi akisema ametumwa na Rais Karume aje aniambie nikamwombe Maalim Seif aridhie matokeo ya uchaguzi mkuu yatakayotangazwa,” alisema Moyo.
 
“Nilimuuliza Riyami, nikamwambie nini Seif? Akaniambia utajua wewe. Nikamwambia au ndo tumeshindwa? Riyami akatabasamu tu!
 
“Kwa hiyo, nilikwenda kuzungumza naye. Nilimwambia wewe (Seif) umezoea kushindwa na mimi (CCM) nimezoea kushinda, kubaliana na matokeo,” alisema.
 
Alipoulizwa kama ni kweli maneno hayo tu ndiyo yalimlainisha Maalim Seif aridhie matokeo hayo, Moyo alijibu;

“Hapana, nilizungumza naye kwa kina historia ya mabadiliko, tulikotoka, kufikia kuundwa kwa kamati za miafaka mpaka sasa, naye alikubali.”
 
Baada ya kukubaliana, Moyo alisema kuwa Maalim Seif alikwenda kuwaambia vijana wake waliokuwa kwenye kituo cha kuhesabia kura katika Hoteli ya Bwawani waondoke, na baada ya vijana wake kuondoka, Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) ikatangaza matokeo yaliyompa ushindi Dk Ali Mohamed Shein.
 
Hata hivyo, Moyo alikataa kuweka wazi kama hatua yake kwenda kwa Maalim Seif ililenga kumshawishi akubali kushindwa wakati matokeo yalionyesha ameshinda. Pia, hakutaka kuweka bayana kama wakati anakwenda kwa Seif alikuwa anajua matokeo.
 
Alipoulizwa kama atakuwa tayari mwaka huu kutumwa tena kwenda kumshawishi Maalim Seif akubaliane na matokeo, alisema:“Hapana. Sithubutu. Hapa inatosha.”
 
Aidha, Moyo amewashauri wanaCCM wasimbeze wala kumdharau Maalim Seif.


“Watu wajiulize, miafaka mingapi ilifikiwa Zanzibar, lakini haikutekelezwa? Mwafaka wa sasa uliowezesha kufanyiwa marekebisho Katiba na kuundwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ni matokeo ya mchango wa Seif na Rais Karume.”
 
Awaonya CCM
Pia, amewataka wana-CCM kujifunza historia ya chaguzi zilizopita kuanzia ule wa mwaka 1963 ambao ASP ilijinasibu kuwa itashinda na ikapeleka hivyo ujumbe kwa Mwalimu Julius Nyerere wa Tanganyika, lakini muungano wa ZNP (Zanzibar Nationalist Party) na ZPPP (Zanzibar na Pemba People’s Party ndio ulishinda.
 
“Lakini historia ya leo inaonyesha Pemba nzima iko chini ya CUF, CCM haiko kule iko Unguja tu ambako CUF imeanza kushinda viti. Tunatumia sana hisia kwamba tutashinda, dhana hii ni potofu,” alisema.
 
“Na mwaka huu CUF wanapata nguvu zaidi kwani wanaungwa mkono na vijana wanaotaka misingi iliyoasisiwa na Afro Shiraz Party ya kupinga ukabila, rangi na udini; vijana ambao wanapigania Zanzibar iwe na mamlaka yake.”
 
Alipoulizwa kuwa haoni kwamba alifanya kosa kuhudhuria na kuhutubia mikutano ya hadhara ya CUF, alijibu kuwa hakwenda kama mwana-CCM bali alialikwa kama mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano na kwamba CCM hawana kawaida ya kumwalika.
 
Aonyesha hekima
Pia, alipoulizwa anawaambia nini waliomfukuza, Moyo alijibu: “Sina cha kuwajibu kwa sababu daima mwanasiasa hupaswi kuongeza maadui bila sababu za msingi. Wao hawanitaki basi na wala sina mpango wa kujiunga na chama chochote cha siasa.”
 
Moyo ni kati ya waasisi wawili wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao wako hai, mwingine akiwa rais wa zamani wa Zanzibar, Alhaji Aboud Jumbe.

No comments:

Post a Comment