MCHEZAJI KANU WA NIGERIA ATOA MAFUNZO KWA WATOTO WA KITUO CHA MICHEZO CHA JAKAYA KIKWETE YOUTH PARK
Mchezaji wa zamani wa timu ya Taifa ya
Nigeria, Super Eagles, Nwankwo Kanu (kulia), akiwaelekeza jinsi ya
kucheza mpira wachezaji wa Timu ya vijana waliochini ya miaka 20 ya
Sunderland alipotembelea Kituo cha Michezo cha Jakaya Kikwete Youth Park
kilichopo Kidongo Chekundu Mnazi Mmoja Dar es Salaam jana. Kanu yupo
nchini kwa ziara ya siku tano kwa mwaliko wa Kampuni ya StarTimes
Tanzania ambapo jana alitoa msaada wa vyakula, magodoro, sabuni na
vyombo vya matumizi ya jikoni kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu
katika Shule ya Msingi ya Majimatitu ya Mbagala wilayani Temeke.
Hapa akiwa katika picha ya pamoja na timu hiyo ya watoto.
Akielekeza namna ya kucheza mpira.
Maelekezo yakiendelea.
Watoto hao wakichezwa kwa kufuata maelekezo ya Kanu
(hayupo pichani)
Kanu akiwagawia fulana wachezaji hao.
Hapa akiwa katika picha ya pamoja na walimu wa watoto hao.
Akiendelea kutoa maelekezo ya jinsi ya kucheza mpira.
Watoto wa kituo hicho wakimshangilia Kanu (hayupo pichani)
Kanu akiwa katika picha ya pamoja ya Buguruni Youth Centre.
Kanu akizungumza na watoto wanaopata mafunzo ya soka katika kituo hicho.
Kanu akikagua timu ya watoto hao.
Na Dotto Mwaibale
MCHEZAJI nyota wa zamani wa timu ya taifa ya Naijeria, Nwankwo Kanu ambaye kwa sasa ni balozi
wa makampuni ya StarTimes barani Afrika ametembelea na kushiriki kwenye
mafunzo na watoto kwenye kituo cha Jakaya Mrisho Kikwete Youth Park cha
jijini Dar es Salaam jana.
Kanu ambaye amekuja kwa shughuli za
kampuni hiyo atakuwepo nchini Tanzania kwa muda wa siku tano alifurahi
sana kuona watoto wameandaliwa mazingira mazuri kwa ajili ya michezo
mbalimbali kwani sio wote waliopata fursa hiyo.
“Wakati mimi ninaanza kucheza mpira
hakukuwa na kituo kizuri kama hiki wala jezi, viatu na walimu wazuri
mlio nao sasa. Hii ni fursa ya kipekee kwenu nyinyi kuweza kuonyesha
juhudi za kujifunza ili mje kuwa kama mimi siku za mbeleni.
Leo mimi nimekuwa maarufu ni kwa sababu
nilikuwa na nidhamu, bidii, dhamira na kuwasikiliza walimu wangu
walipokuwa wananifundisha. Hatimaye leo hii nina mafanikio makubwa,
ninaishi maisha mazuri, wazazi wangu pia wanaishi mahali pazuri,
wanasafiri na kupata wanachokitaka kwa sababu tu ya mimi kufanikiwa.”
Kanu aliwaambia watoto wa kituo cha Jakaya Kikwete Kampuni ya StarTimes
ambayo imo zaidi ya nchi kumi barani Afrika imemtua mchezaji huyo kama
balozi katika
kuwawakilisha katika shughuli mbalimbali.
Kanu anatarajia kuwa chachu kwa katika
kampuni hiyo hususani katika kuboresha na kuongeza vipindi na chaneli za
michezo kwani waafrika wengi wanapenda soka.
“Ninaamini mchezo wa soka ndio
unaopendwa na watu wengi zaidi duniani na waafrika ni miongoni mwao.
StarTimes mpaka sasa wamepiga hatua kubwa katika kulisimamia hili, mpaka
sasa tayari wana haki miliki za kuonyesha ligi za Budensiliga na Serie A
za Ujerumani na Italia.
Hiyo ni hatua kubwa kwani wateja wanafurahia michezo hiyo inyoonekana moja kwa moja kwa
vifurusushi vya bei nafuu. Kama balozi ninaahidi kushirikiana na
kampuni katika kuboresha zaidi vipindi vyake na pia kuishauri kujikita
zaidi na michezo ya nyumbani.
Kama mnavyoona kwa mara ya kwanza
tumedhamini ligi daraja la kwanza.” Aliongezea mchezaji Kanu
alihitimisha kwa kuwataka watoto wa kituoni hapo kuonyesha bidii, utii
na dhamira ya dhati kwa kila wanachokifanya, “Ningependa kuwashauri
wadogo zangu kuwa popote utakapokwenda duniani kwenye mchezo wa soka,
viwanja na mipira inayotumika ni hii hii wala hakuna tofauti yoyote.
Hivyo basi sioni kama kuna kitu cha
kuwazuia na nyinyi msifanikiwe. Kama nilivyowaambia awali, bidii,
nidhamu, dhamira na utii kwa walimu wenu ndio msingi wa mafanikio ya
mwanasoka yeyote Yule duniani. Nawatakia kila la kheri na siku nyingine
nikija Tanzania naahidi kuwatembelea tena.”
Kwa upande wake Kocha Mkuu wa Kituo cha
Vijana cha Jakaya Mrisho Kikwete, Eduard Tamayo alielezea furaha yake
kwa kampuni ya StarTimes kuandaa kitu kama hiko na kukiteua kituo hiko
kuwa mwenyeji wa ugeni wa Kanu nchini Tanzania.
“Nimefurahi sana kwa ujio aliyekuwa
mchezaji wa timu ya taifa ya Naijeria na vilabu vikubwa barani Ulaya
kama vile Ajax, Inter Milan na Arsena, Nwankwo Kanu kutembelea hapa na
kushiriki mafunzo na watoto. Hii ni bahati kubwa sana kwa watoto hawa
kwani ni nadra sana kutokea, kupata mafunzo, kuzungumza, kupata ushauri
na kuuliza maswali moja kwa moja kwa Kanu. Ninatumaini itakuwa imewapa
motisha kubwa sana.” Alisema Tamayo
Kocha Mkuu huyo kituoni hapo
alihitimisha kwa kuwataka wazazi kuwapeleka na kuwasajili watoto kituoni
hapo kwa mafunzo kwani wanapokelewa na kuwapatia mafunzo mazuri kwa
kuviendeleza vipaji vyao. Na kwamba kituo hiko ni fursa kwa watanzania
hivyo ni vema kukitumia vizuri.
Post a Comment