Saturday, April 9, 2016

MCHEZAJI KANU WA NIGERIA ATOA MAFUNZO KWA WATOTO WA KITUO CHA MICHEZO CHA JAKAYA KIKWETE YOUTH PARK

 Mchezaji wa zamani wa timu ya Taifa ya Nigeria, Super Eagles, Nwankwo Kanu (kulia), akiwaelekeza jinsi ya kucheza mpira wachezaji wa Timu ya vijana waliochini ya miaka 20 ya Sunderland alipotembelea Kituo cha Michezo cha Jakaya Kikwete Youth Park kilichopo Kidongo Chekundu Mnazi Mmoja Dar es Salaam jana. Kanu yupo nchini kwa ziara ya siku tano kwa mwaliko wa Kampuni ya StarTimes Tanzania ambapo jana alitoa msaada wa vyakula, magodoro, sabuni na vyombo vya matumizi ya jikoni kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu katika Shule ya Msingi ya Majimatitu ya Mbagala wilayani Temeke.
 Hapa akiwa katika picha ya pamoja na timu  hiyo ya watoto.
 Akielekeza namna ya kucheza mpira.
 Maelekezo yakiendelea.
 Watoto hao wakichezwa kwa kufuata maelekezo ya Kanu 
(hayupo pichani)
 Kanu akiwagawia fulana wachezaji hao.
 Hapa akiwa katika picha ya pamoja na walimu wa watoto hao.
 Akiendelea kutoa maelekezo ya jinsi ya kucheza mpira.
 Watoto wa kituo hicho wakimshangilia Kanu (hayupo pichani)
 Kanu akiwa katika picha ya pamoja ya Buguruni Youth Centre.
 Kanu akizungumza na watoto wanaopata mafunzo ya soka katika kituo hicho.
Kanu akikagua timu ya watoto hao.

Na Dotto Mwaibale

MCHEZAJI nyota wa zamani wa timu ya taifa ya Naijeria, Nwankwo Kanu ambaye kwa sasa ni balozi wa makampuni ya StarTimes barani Afrika ametembelea na kushiriki kwenye mafunzo na watoto kwenye kituo cha Jakaya Mrisho Kikwete Youth Park cha jijini Dar es Salaam jana.

Kanu ambaye amekuja kwa shughuli za kampuni hiyo atakuwepo nchini Tanzania kwa muda wa siku tano alifurahi sana kuona watoto wameandaliwa mazingira mazuri kwa ajili ya michezo mbalimbali kwani sio wote waliopata fursa hiyo.

“Wakati mimi ninaanza kucheza mpira hakukuwa na kituo kizuri kama hiki wala jezi, viatu na walimu wazuri mlio nao sasa. Hii ni fursa ya kipekee kwenu nyinyi kuweza kuonyesha 
juhudi za kujifunza ili mje kuwa kama mimi siku za mbeleni. 

Leo mimi nimekuwa maarufu ni kwa sababu nilikuwa na nidhamu, bidii, dhamira na kuwasikiliza walimu wangu walipokuwa wananifundisha. Hatimaye leo hii nina mafanikio makubwa, ninaishi maisha mazuri, wazazi wangu pia wanaishi mahali pazuri, wanasafiri na kupata wanachokitaka kwa sababu tu ya mimi kufanikiwa.” Kanu aliwaambia watoto wa kituo cha Jakaya Kikwete Kampuni ya StarTimes ambayo imo zaidi ya nchi kumi barani Afrika imemtua mchezaji huyo kama balozi katika 
kuwawakilisha katika shughuli mbalimbali. 

Kanu anatarajia kuwa chachu kwa katika kampuni hiyo hususani katika kuboresha na kuongeza vipindi na chaneli za michezo kwani waafrika wengi wanapenda soka.

“Ninaamini mchezo wa soka ndio unaopendwa na watu wengi zaidi duniani na waafrika ni miongoni mwao. StarTimes mpaka sasa wamepiga hatua kubwa katika kulisimamia hili, mpaka sasa tayari wana haki miliki za kuonyesha ligi za Budensiliga na Serie A za Ujerumani na Italia. 

Hiyo ni hatua kubwa kwani wateja wanafurahia michezo hiyo inyoonekana moja kwa moja kwa vifurusushi vya bei nafuu. Kama balozi ninaahidi kushirikiana na kampuni katika kuboresha zaidi vipindi vyake na pia kuishauri kujikita zaidi na michezo ya nyumbani. 

Kama mnavyoona kwa mara ya kwanza tumedhamini ligi daraja la kwanza.” Aliongezea mchezaji Kanu alihitimisha kwa kuwataka watoto wa kituoni hapo kuonyesha bidii, utii na dhamira ya dhati kwa kila wanachokifanya, “Ningependa kuwashauri wadogo zangu kuwa popote utakapokwenda duniani kwenye mchezo wa soka, viwanja na mipira inayotumika ni hii hii wala hakuna tofauti yoyote. 

Hivyo basi sioni kama kuna kitu cha kuwazuia na nyinyi msifanikiwe. Kama nilivyowaambia awali, bidii, nidhamu, dhamira na utii kwa walimu wenu ndio msingi wa mafanikio ya mwanasoka yeyote Yule duniani. Nawatakia kila la kheri na siku nyingine nikija Tanzania naahidi kuwatembelea tena.”

Kwa  upande wake Kocha Mkuu wa Kituo cha Vijana cha Jakaya Mrisho Kikwete,  Eduard Tamayo alielezea furaha yake kwa kampuni ya StarTimes kuandaa kitu kama hiko na kukiteua kituo hiko kuwa mwenyeji wa ugeni wa Kanu nchini Tanzania.

“Nimefurahi sana kwa ujio aliyekuwa mchezaji wa timu ya taifa ya Naijeria na vilabu vikubwa barani Ulaya kama vile Ajax, Inter Milan na Arsena, Nwankwo Kanu kutembelea hapa na kushiriki mafunzo na watoto. Hii ni bahati kubwa sana kwa watoto hawa kwani ni nadra sana kutokea, kupata mafunzo, kuzungumza, kupata ushauri na kuuliza maswali moja kwa moja kwa Kanu. Ninatumaini itakuwa imewapa motisha kubwa sana.” Alisema  Tamayo

Kocha Mkuu huyo kituoni hapo alihitimisha kwa kuwataka wazazi kuwapeleka na kuwasajili watoto kituoni hapo kwa mafunzo kwani wanapokelewa na kuwapatia mafunzo mazuri kwa kuviendeleza vipaji vyao. Na kwamba kituo hiko ni fursa kwa watanzania hivyo ni vema kukitumia vizuri.

No comments:

Post a Comment