Thursday, July 23, 2015

Jana ilikuwa siku ya kwanza kati ya siku kumi za kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura kwa kutumia mfumo wa Biometric Voters Registry (BVR) katika jiji la Dar es Salaam.

Namshukuru Mungu tayari nina kadi yangu kwa ajili ya kuwapata viongozi wangu bora hapo 25 Oktoba mwaka huu.

Sikufaidi tu kupata hiyo hati, la hasha! Katika kubadilishana mawazo na wajiandikishaji wenzangu, nikabahatika kuongea na kiongozi wa chama cha Wananchi CUF ngazi ya kijiji.

Pamoja na mambo mengine nilivuna kutoka kwake msimamo wa CUF kwenye UKAWA,nani mgombea urais kupitia UKAWA na nani hakubaliki na kwanini.

Ambalo lilinivutia sana ni msimamo wa ACT kuhusu mgombea wa UKAWA atakayeteuliwa.

Kimsingi kiongozi huyo alinihakikishia kuwa CUF bado hawajajitoa kwenye UKAWA. Kuhusu mgombea ambaye viongozi wengi kutoka vyama vinavyounda UKAWA wanaona anafaa kupeperusha bendera ya UKAWA ni Prof. IBRAHIM HAROUNA LIPUMBA.

Lipumba anaungwa mkono na FREEMAN MBOWE na HALIMA MDEE kwa vigezo kuwa ana busara, ni mtu mwenye subira na staha na asiyekurupuka kufanya maamuzi.

Slaa anaelezwa kuwa mwenye jazba na visasi jambo ambalo kwenye kuunda serikali linaweza kuwagharimu.

Nilitaka kujua sababu za Mbowe kutomkubali Katibu wake Mkuu, Wilbroad Slaa kupeperusha bendera ya UKAWA.

Inasemekana kuna maandamano waliandaa yeye MBOWE na SLAA lakini mambo yalipoharibika, Slaa akamruka na akashtakiwa yeye jambo ambalo Mbowe aliona ni usaliti na anachokifanya sasa ni kulipiza kisasi. Kitendo cha Lowassa kutakiwa na Mbowe ndani ya CHADEMA huku SLAA hamtaki nayo ni sababu nyingine.

Chama cha Alliance for Change & Transparency ( ACT) kama chama cha Upinzani na ambacho bado ni kichanga kabisa kwa mujibu wa kiongozi huyo wa CUF kinasema endapo UKAWA watamsimamisha LIPUMBA kama mgombea urais wao ACT hawatamsimamisha mgombea na badala yake watamuunga mkono Lipumba vinginevyo watamsimamisha mgombea wao.

kwa mujibu wa kiongozi huyo, kuna uwezekano mkubwa wa CUF kujitoa UKAWA na kutengeneza muungano na ACT na kumuweka mgombea urais atakayepeperusha bendera ya vyana hivyo viwili.

Tusubiri tuone namna itakavyokuwa.

No comments:

Post a Comment