Friday, June 12, 2015

Urais 2015: Wassira Awashambulia Wagombea Wenzake......Awabeza Wanaojaza Watu Wengi kwenye Mikutano, Asema hata yeye Akiamua Anaweza!!



Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Steven Wasira amewashambulia  watangaza  nia  wenzake  kwa  madai  kuwa  wanatumia  pesa kusaka uongozi.
 
Alisema Tanzania inapita katika msimu mgumu kisiasa kutokana na baadhi ya watu kutumia mabilioni ya fedha kusaka uongozi wa nchi, wakati uongozi si biashara. 
 
Wasira alitoa kauli hiyo jana wakati akiwashukuru wanachama wa CCM waliojitokeza kumdhamini katika Uwanja wa CCM Kirumba, kama sehemu ya utaratibu wa chama hicho kuelekea mchakato wa kumpata mgombea urais katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu. 
 
“Jamani wakati wa kujaza watu kwenye viwanja bado haujafika, mikutano ya hadhara bado. Kwa hiyo si kwamba hatuwezi kujaza watu, tukitaka tunaweza, lakini wakati bado, utafika tutajaza watu. 
 
“CCM na taifa kwa sasa vipo katika mazingira magumu kisiasa, rushwa sasa inainyemelea kwa kasi kubwa siasa, hii ni hatari sana, kamwe tusije kubali nchi yetu kuwekwa rehani na kundi la mafisadi. 
 
“Mtu ambaye anataka kuiweka rehani nchi kamwe hawezi kuwa na hoja, ndio sababu mmeanza kuona watu wanaishiwa hoja. Mtanzania yoyote yule anayetumia mabilioni kununua nchi mwisho wa siku ataiuza tu,” alisema Wasira huku wadhamini wake wakishangilia. 
 
Wasira alisema tatizo la rushwa katika siasa ni kubwa kiasi cha kuwafanya baadhi ya watu kuamini kuwa wanaweza kuinunua CCM. 
 
“Hivi nani kakutuma kuinunua CCM? Unainunua kwa niaba ya nani. Nchi yetu haipo sokoni, na wala hatujawahi kutangaza tenda ya kuuza nchi, sasa mabilioni kwenye siasa ya kazi gani?” alihoji. 
 
Aliwasihi Watanzania kuwa makini kwa sababu kuna kila dalili nchi inapelekwa sokoni na watu wachache wasio itakia mema. 
 
Kada huyo mkongwe wa CCM aliwataka Watanzania kujiuliza na kutafakari ni wapi mabilioni yanayotumika yanatoka, na kuongeza kuwa wanaotoa fedha hizo uwezo wao kifedha hauonekani katika kulipa kodi. 
 
Aliwataka wananchi kukataa kugeuzwa kuku wa kienyeji, ambapo alitoa mfano wa mtu anayetaka kuwakusanya kuku huwakusanya kwa kuwarushia mtama au pumba, nao hukimbilia kula bila hata kutaza nyuma au kufikiri. 
 
 “Kuna wenzetu ambao kwa malengo yao maovu wameamua kuwageuza wananchi na kuwafanya kuku wa kienyeji, wanakuja na fedha zao na wanazitumia kuwakusanya kwenye viwanja, wananchi kataeni, vinginevyo majuto ni mjukuu,” alisema. 
 
Tayari Wasira amekwishapata wadhamini katika mikoa 20, ikiwamo sita ya Tanzania Visiwani na jana alidhaminiwa katika mikoa ya Mwanza, Shinyanga na Geita. 
 
Kwa mujibu wa utaratibu wa CCM, kila mtangaza nia anapaswa kupata wadhamini wasiopungua katika mikoa 15 (12 Tanzania Bara na mitatu Tanzania Visiwani), ambapo jumla ya wadhamini wanapaswa kuwa 450. 
 
Mbali ya Wasira kutimiza sharti hilo ndani muda wa siku 8, alisema atakwenda mikoa yote ya Tanzania ili kudhihirishia kuwa amekusudia na ana nia ya dhati ya kuomba kuteuliwa kupeperusha bendera ya CCM, Oktoba, mwaka huu. 
 
Pia alitumia fursa hiyo kuwahakikishia Watanzania kuwa yupo imara kabisa kiakili na kimwili kuhakikisha CCM inashinda kwa kishindo katika uchaguzi huo, na kusema kama atateuliwa, basi ataongoza kampeni mwanzo hadi mwisho bila kutetereka. 
 
Mchakato wa kuchukua na kurejesha fomu kwa wana-CCM wanaoomba kuteuliwa utahitimishwa Julai 2, mwaka huu mjini Dodoma, na kufuatiwa na vikao vya mchujo vitakavyoanza Julai 9.

No comments:

Post a Comment