Bajeti kuu ya Serikali 2015/ 2016: Kodi ya Pombe na Sigara Haijaongezwa.....Petrol, Dizel na Mafuta ya taa Kodi Imepanda.....PAYE Imepunguzwa, Penshen Imeongezeka
Kwa
mara kwanza Bajeti ya 2015/16, ambayo ni ya mwisho ya Serikali ya Awamu
ya Nne, haijaongeza kodi katika bidhaa za pombe na sigara, badala yake
imeendelea kupandisha kodi katika mafuta huku ikiminya uingizaji wa
bidhaa nchini kwa ajili ya kulinda viwanda na wazalishaji wa ndani na
kuongeza ajira.
Pia,
bajeti hiyo ya mwisho kwa utawala wa Rais Jakaya Kikwete imeweka
kipaumbele katika kugharamia Uchaguzi Mkuu, kuweka msukumo maalum kwenye
miradi ya umeme vijijini, maji vijijini, kukamilisha miradi ya
kimkakati inayoendelea pamoja na kuwekeza kwenye rasilimali watu.
Bajeti
hiyo imeeleza mikakati mbalimbali ya ukusanyaji mapato kwa kufanya
mageuzi kwenye mfumo wa kodi, kudhibiti mianya ya matumizi ya fedha za
Serikali, kupunguza misamaha ya kodi, kupunguza kero za wastaafu kwa
kuwaongezea mafao ya mwezi kutoka Sh50,000 hadi Sh85,000, kupunguza Kodi
ya Malipo ya Kadri ya Mapato (Paye) kwa asilimia moja na kuanzisha
mafao ya kila mwezi kwa wazee.
Akiwasilisha
bajeti hiyo ya mwaka wa fedha wa 2015/16, Waziri Mkuya alipendekeza
mabadiliko ya sheria mbalimbali zitakazosaidia kupunguza na kuongeza
kodi zitazoisadia Serikali kuongeza mapato ili iweze kufanikisha
utekeleji wa bajeti ya Sh22.5 trilioni.
Waziri
Mkuya aliliomba bunge liridhie mabadiliko katika Sheria ya Sheria ya
Mafuta ya Petroli Sura namba 392 ili kuongeza tozo ya mafuta ya petroli
na dizeli kutoka Sh50 hadi Sh100.
Pia,
tozo ya mafuta ya taa imependekezwa kuongezwa kutoka Sh50 hadi Sh150
ikiwa ni moja ya njia ya kupunguza uwezekano wa uchakachuaji.
“Hatua
ya kuongeza Tozo ya Mafuta ya Petroli inatarajiwa kuongeza mapato ya
Serikali kwa kiasi cha Sh139.78 bilioni na fedha zote zitaelekezwa
katika mfuko wa Rea kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa usambazaji
umeme vijijini,” alisema Mkuya huku baadhi ya wabunge wakionyesha kupinga.
Pia,
Mkuya alipendekeza mabadiliko katika Sheria Tozo za Mafuta na Barabara
namba 220 ili kuongeza tozo katika mafuta ya Dizeli, Petroli na kwa Sh50
hadi kufikia Sh313.
Alisema
hatua hiyo ya kuongeza tozo hiyo pia itaongeza mapato kwa takribani
Sh136.4 bilioni ambayo alisema yataelekezwa katika mradi wa kusambaza
umeme vijijini wa Rea.
Pamoja
na maumivu hayo, Mkuya alipendekeza Waziri wa Fedha apatiwe mamlaka ya
kusamehe Tozo ya Mafuta ya Petroli kwenye miradi inayotekelezwa kwa
misaada ya wafadhili na yenye mikataba isiyohusisha utozaji wa tozo hiyo
ili kuondoa usumbufu na ucheleweshaji katika utekelezaji wake.
Katika
jitihada za kulinda viwanda vya ndani na kuongeza ajira, Serikali
inapendeleza mabadiliko ya Sheria za Kodi ya Mapato namba 332, Sheria ya
mauzo ya nje namba 196, Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika
Mashariki ya mwaka 2004 na Sheria ya Uwekezaji Tanzania Sura 196.
Waziri
Mkuya alibainisha kuwa ili kumpunguzia mzigo mfanyakazi wamependekeza
kupunguza kiwango cha chini cha kutoza kodi ya mapato ya ajira kutoka
asilimia 12 hadi asilimia 11 akibainisha ni dhamira ya Serikali tangu
mwaka mwaka 2006/07 kodi hiyo ilipokuwa asilimia 18.5.
Pia,
mabadiliko ya Sheria ya Mapato yatashuhudia wafanyabiashara wadogo
wakipunguziwa kiwango cha kutozwa kodi kwenye mapato ghafi kwa asilimia
25 ikiwa ni njia ya kuwahamasisha ulipaji wa kodi kwa hiari.
Mbali
na kutoa nafuu hizo, Serikali inatarajia kufanya marekebishao ya Sheria
hiyo kwa kuondoa msamaha wa kodi kwenye miradi ya Serikali
inayotekelezwa kutokana na mikataba baina ya Serikali na taasisi
mbalimbali inayohusisha mikopo ya kibiashara kuanzia Julai Mosi, 2015.
“Hatua hizi za Kodi ya Mapato zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 47.2 bilioni,” alisema Mkuya.
Serikali
pia, imependekeza kurejesha msamaha wa tozo ya ufundi stadi kwa sekta
ya kilimo ili kutoa unafuu wa kodi kwenye shughuli za kilimo mashambani
ambazo hutegemea nguvukazi kwa kiasi kikubwa kabla ya kuanza kupata
manufaa kutokana na uwekezaji kwenye kilimo.
Hata
hivyo, hali si shwari kwa wafanyabiashara wa bidhaa za ngozi nje ya
nchi kutokana na bajeti hiyo kuongeza kiwango cha tozo kinachotozwa
kwenye kwenye ngozi ghafi.
Bidhaa
zinazosafirishwa kwenda nje ya nchi zitatozwa asilimia 80 ya thamani ya
ngozi inapokuwa bandarini (FOB) au dola ya Marekani 0.52 kwa kilo moja
kutegemea kiwango kipi ni kikubwa kutoka asilimia 60 ya awali au
shilingi 600 kwa kilo moja.
Hatua
hiyo, kwa mujibu wa Mkuya inazingatia makubaliano ya nchi wanachama wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki ya kuwianisha viwango vya kodi kwenye ngozi
ghafi na pia kuzuia biashara ya magendo na kuhamasisha usindikaji wa
ngozi ndani ya ukanda wa Jumuiya ili kuongeza thamani, mapato na ajira.
Hata
hivyo, bidhaa za ngozi zilizosindikwa kwa kiwango cha kati zitatozwa
asilimia 10 ya kodi ya mauzo ya nje ili kuhamasisha uongezaji thamani wa
bidhaa hizo na uwekezaji katika viwanda vya kutengeneza bidhaa za ngozi
nchini.
Alisema hatua hizo mbili kwa pamoja zinatarajia kuongeza mfuko wa Serikali kwa Sh920 milioni.
Kampuni
zinazozalisha bidhaa za mabomba ya PVC na HDPE zinatarajiwa kupata
ahueni baada ya Serikali kuziondoa katika orodha ya bidhaa
zinazotambuliwa kuwa ni za mtaji (Deemed Capital Goods) ambazo kwa sasa
zinapata msamaha wa kodi kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).
“Mapendekezo
haya yanazingatia kwamba bidhaa hizi hivi sasa zinazalishwa hapa nchini
kwa kiasi cha kutosheleza mahitaji. Hatua hii itasaidia kulinda viwanda
vinavyotengeneza mabomba ya aina hiyo na hivyo kuchochea ongezeko la
ajira na mapato ya Serikali,” alisema.
Ahueni
hiyo itawafikia pia watengenezaji wa matela ya kusafirishia mizigo
nchini baada ya bajeti hiyo kufuta msamaha unaotolewa kupitia Kituo cha
Uwekezaji kwenye matela hayo, hatua itakayowezesha ushindani katika
soko, kuhamasisha uwekezaji mkubwa wa kutengeneza matela nchini,
kuongeza ajira na kuongeza mapato ya Serikali.
Wawekezaji
wenye nia ya kuwekeza nchini ili watambuliwe kuwa ni mahsusi kwa
watatakiwa kutimiza masharti kadhaa ili kupata ahueni ya kikodi,
likiwemo la kuwa mtaji wa jumla usiopungua dola za Marekani 300 milioni
(630 bilioni) na mtaji huo upitie taasisi za ndani za kifedha.
“Pia
anatakiwa kuwa na uwezo wa kutengeneza ajira za moja kwa moja kwa
Watanzania zisizopungua 1,500; ikiwa ni pamoja na idadi inayoridhisha
katika ngazi za juu za uongozi wa kampuni. Kuwa na uwezo wa kuzalisha
fedha za kigeni au kuzalisha bidhaa mbadala wa zile zinazoagizwa nje,” alieleza Mkuya.
Pia,
bajeti hiyo inabana uingizaji wa mchele, sukari na vyuma kwa kuongeza
ushuru huku bidhaa za nyuzi za kutengezea nyavu, malighafi za
kutengenezea pasta na tambi zikiondolewa kodi.
Yaiokoa Sukari
Katika
kudhibiti uingizaji wa sukari kiholela na kulinda viwanda vya ndani,
Serikali imeongeza kiwango cha ushuru wa forodha kutoka Dola 200 za
Marekani kwa tani au asilimia 100 ya thamani ya bidhaa hiyo inapokuwa
imefika bandarini, hadi Dola 460 za Marekani kwa tani au asilimia 100 ya
thamani ya bidhaa hiyo inapofika bandarini, kutegemea kiwango cha
mzigo.
“Sukari
inayotumika viwandani hivi sasa hulipiwa ushuru wa forodha wa asilimia
10 badala ya kiwango cha ushuru kilichoainishwa kisheria cha asilimia
100. Katika utaratibu maalumu unaopendekezwa, waagizaji watatakiwa
kulipia ushuru wa asilimia 50 na mara baada ya kuzalisha bidhaa
viwandani na kuthibitishwa na Mamlaka ya Mapato kwamba sukari hiyo
imetumika ipasavyo watarejeshewa asilimia 40,” alisema Mkuya.
Serikali
imepunguza ushuru wa mabasi yenye uwezo wa kubeba abiria zaidi ya 25
kwa kutoza asilimia 10 badala ya 25 kwa ajili ya mradi wa mabasi wa jiji
la Dar es Salaam (DART) kwa mwaka mmoja.
No comments:
Post a Comment