Urais 2015: January Makamba Apokelewa Kishujaa Mkoani Iringa, Apata Wadhamini 600
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, ameungwa mkono na Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) mkoani Iringa ambako alipata wadhamini zaidi ya 600.
Akizungumza na wadhamini wake hao, January alisema endapo atafanikiwa
kuwa rais atahakikisha CCM inalirudisha Jimbo la Iringa Mjini ambalo kwa
sasa linaongozwa na Mchungaji Peter Msigwa kutoka Chama cha Demokrasia
na Maendeleo (Chadema) kwani ataweka kambi katika mji huo.
Alisema kuwa ataimarisha miundombinu, ikiwa ni pamoja na kutanua
kiwanja cha ndege cha Nduli na kukifanya kuwa cha kimataifa ili wananchi
waweze kupata ajira kitakappingiza watalii wengi na kuongeza pato la
mkoa huo pamoja na kuzijenga barabara kwa kiwango cha lami.
Aidha, January, alisema anaamini CCM kitamchagua kiongozi kwa kujiamini
na kuwaomba wananchi wapuuze kauli za watu wanaodai kuwa endapo chama
hakitawasimamisha katika nafasi hiyo basi kitasambaratika.
Alisema wananchi wanapaswa kutambua kuwa dhamana ya nchi hii iko
mikononi mwa CCM, hivyo akipata nafasi hiyo au asipopata atakuwa mstari
wa mbele katika kukirudisha chama pamoja kutokana na kuwa na makundi
katika kipindi hiki cha uchaguzi.
Aliongeza kwa kuwaomba wananchi wa mkoa huo kupitisha ushawishi kwa
viongozi wanaopitisha majina kuwa wamchague kijana anayekusudia kuleta
mabadiliko ya kweli ambaye ndiyo yeye.
Kwa Upande wake Mwenyekiti wa Wenyeviti wa UVCCM mkoani humo, Kaunda
Mwaipiana, alisema vijana hao wanamuunga mkono January katika kipindi
chote kwani wanaamini anaweza kuivusha nchi hapa ilipo kutokana na
hotuba yake nzuri aliyoitoa wakati akitangaza nia iliyobeba mikakati
thatibi ya maendeleo.
Naye Mwenyekiti wa Wilaya ya Iringa, Abeid Kiponza, alimpongeza kwa
uthubutu wake wa kuomba nafasi hiyo na kwamba kama alivyoona vijana
wenzake wa mkoa wa Iringa wameonesha nia ya kumuunga mkono.
No comments:
Post a Comment