Friday, June 12, 2015

Urais 2015: Profesa Lipumba Kuchukua Fomu ya Urais Jumapili ya Wiki hii.......Tukio hilo Litarushwa Moja Kwa Moja na Runinga Kadhaa



Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa  Ibrahim Lipumba, Jumapili atachukua fomu ya kugombea urais ndani ya chama hicho na atawaeleza Watanzania sababu ya kuwania nafasi hiyo. 
 
Akizungumza jana, Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa chama hicho, Shaweji Mketo alisema, Profesa Lipumba ndiye mgombea pekee wa urais aliyetangaza nia ya kuwania nafasi hiyo.
 
Alisema muda wa kutangaza nia kwa wagombea urais kupitia chama hicho ulianza Mei 10 hadi Juni 10, mwaka huu.
 
“Kalenda yetu inaonyesha muda wa mwisho wa kutangaza nia ilikuwa juzi na aliyefanya hivyo ni Profesa Lipumba pekee yake,” alisema.
 
Alisema muda wa kuchukua fomu kwa nafasi ya urais kupitia chama hicho ulianza jana na utakamika Juni 14, mwaka huu.
 
“Mkutano huo utakaoonyeshwa moja kwa moja kupitia runinga,” alisema.
 
Mketo alisema vikao vya Baraza Kuu la Uongozi la chama hicho vitaanza Julai 11 hadi Julai 12, mwaka huu ili kumpitisha mgombea urais, wabunge na madiwani.
 
“Wagombea watakaopitishwa na Baraza watasubiri vikao vya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vitakavyotoa mgombea mmoja katika nafasi ya urais, ubunge na udiwani,” alisema. 
 
Kama Ukawa itamteua Profesa Lipumba ambaye kitaalamu ni mchumi itakuwa ni mara ya tano kuwania nafasi ya urais.
 
Akizungumzia nafasi za ubunge, Mketo alisema kati ya majimbo 189 ya Tanzania Bara, wamepata wagombea kwenye majimbo 133.
 
Alisema majimbo 56 bado hayajapata wagombea na kuwataka wafuasi wa chama hicho wenye sifa kuwania. 
 
Mkurugenzi huyo alisema, bado mchakato wa kura za maoni kwa nafasi za ubunge na udiwani zinaendelea katika kanda mbalimbali.

No comments:

Post a Comment