Wednesday, June 24, 2015

Dkt. Nchimbi Atangaza Rasmi Kutogombea Ubunge Songea


Katika hali isiyokuwa ya kawaida baadhi ya wananchi wakiwemo wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) jimbo la Songea mjini mkoani Ruvuma, wamejikuta katika hali ya sintofahamu huku wengine wakimwaga machozi baada ya mbunge wa jimbo hilo, mh. Dkt. Emmanuel Nchimbi kutangaza rasmi kutogombea tena ubunge katika jimbo hilo.

Nchimbi aliyelitumikia jimbo hilo kwa miaka 10 alikutana na wanachama wa chama cha mapinduzi Katika uwanja  wa majimaji mjini Songea pamoja na kuelezea mafanikio mbalimbali ya maendeleo aliyoyafanya katika jimbo hilo ikiwemo ujenzi wa barabara, zahanati na shule za sekondari lakini pia akatumia nafasi hiyo kutangaza rasmi kutogombea tena ubunge katika jimbo la songea mjini.

Tamko hilo la dkt. Nchimbi lilizua simanzi kwa baadhi ya wananchi na wanachama wa CCM  Songea huku wengine wakishindwa kujizuia na kujikuta wakimwaga machozi.

Katika maelezo yao wanachama hawa walisema kuachia ngazi kwa Dkt, Nchimbi kutogombea katika jimbo hilo kunatoa fursa kubwa kwa vyama vya upinzani kuchukua jimbo hilo hali ambayo hawakubaliani nayo.

Hata hivyo wanachama hao walimuomba mbunge huyo kutengua msimamo wake na kumtaka arejee tena kugombea jimbo la Songea mjini, jibu la dkt. Nchimbi likawa anaenda kufikiria.

No comments:

Post a Comment