Mkulima Msaka urais Atua Morogoro Kusaka Wadhamin
MKULIMA wa Kigoma anayewania kupitishwa na CCM agombee urais kwa
chama hicho, Idelphonce Bilole, ametua mkoani Morogoro akiendelea
kutafuta wadhamini katika mikoa 15 nchini, huku akisisitiza elimu si
kigezo cha yeye kushindwa kuwania nafasi hiyo ya juu.
Bilole aliyasema hayo jana katika ofisi ya CCM Wilaya ya Morogoro
ambapo alisema Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema
kiongozi ni lazima ajue kusoma na kuandika na kwamba CCM ni chama pekee
ambacho hakina ubaguzi.
Aidha, alisema mwaka 2003 alifuatwa na baadhi ya viongozi wa chama
hicho wakimtaka ajiandae ili aweze kuwania nafasi hiyo kwa mwaka 2005
ambapo alisema alikubali na aliandika barua ya kuomba kuteuliwa, lakini
kutokana na sababu ambazo yeye hakuzifahamu barua ile ilichelewa na
hivyo kuamua kuvuta subira.
Hata hivyo alisema kuwa mwaka huu ameona ni muda muafaka wa yeye
kuwania nafasi hiyo ambayo wanachama wenzake wamekuwa wakimuomba
kugombea ambapo alisema kuwa ameshafika katika mikoa kadhaa ikiwemo
Dodoma, Kigoma, Mwanza, Simiyu, Singida, Shinyanga, Geita na sasa
Morogoro kwa ajili ya kutafuta wadhamini.
No comments:
Post a Comment