CCM inapenda kutoa taarifa kuhusu masuala kadhaa kwa wanachama, wapenzi na mashabiki wake na kwa umma wa Watanzania.
Kufunga Kampeni
CCM itafunga kampeni zake kwa utaratibu mpya na kwa kishindo.
Kampeni za CCM zitafungwa Kitaifa kwa mikutano mikubwa ya kampeni katika
mikoa mitano. Mikutano hiyo itaongozwa na viongozi wa CCM Kitaifa
waliopo madarakani na wastaafu. Mikoa hiyo na viongozi watakaoongoza
mikutano hiyo ni kama ifuatavyo:
1. Mwanza – Ndugu Jakaya Mrisho Kikwete, Mwenyekiti wa CCM, Dkt.
John Pombe Magufuli, Mgombea Urais, na Ndugu Samia Hassan Suluhu,
Mgombea Makamu wa Rais
2. Tanga – Ndugu Abdulrahman Kinana, Katibu Mkuu wa CCM
3. Mbeya – Ndugu Benjamin William Mkapa, Mwenyekiti wa CCM Mstaafu
4. Mtwara – Ndugu Ali Hassan Mwinyi, Mwenyekiti wa CCM Mstaafu
5. Kigoma – Ndugu Philip Mangula, Makamu Mwenyekiti wa CCM
6. Kilimanjaro – Ndugu Yusuf Makamba, Katibu Mkuu wa CCM Mstaafu
7. Mara – Ndugu Joseph Warioba, Mjumbe wa Kamati Kuu na Waziri Mkuu Mstaafu
Kati ya leo na kesho, maeneo mengine yanaweza kuongezeka.
Mikutano hii itaanza saa sita mchana na itarushwa, yote kwa pamoja, kwa
matangazo ya moja kwa moja ya vituo vya televisheni vitano na vituo vya
redio 67. Vilevile, watakaohudhuria katika mikutano hii wataunganishwa
moja kwa moja na mkutano wa Mwanza, alipo Mwenyekiti, Mgombea na Mgombea
Mwenza, na wataweza kusikiliza hotuba ya Dkt. Magufuli moja kwa moja
kupitia screens zitakazokuwa katika viwanja vyote hivi saba.
Namna hii ya ufungaji wa kampeni itakuwa ni ya kihistoria, na
inadhihirisha nguvu ya CCM inayoiwezesha kufanya mikutano mikubwa ya
kampeni kwa siku moja katika maeneo mbalimbali nchini. Lakini pia
tutaweka historia katika tasnia ya utangazaji wa televisheni hapa nchini
kwa kutangaza na kuunganisha kwa pamoja matukio saba kwa wakati mmoja.
Kwa upande wa Dar es Salaam, tutafanya mkutano mkubwa wa
ufungaji wa kampeni za Mkoa wa Dar es Salaam, katika Uwanja wa Jangwani,
kesho, Ijumaa, tarehe 23 Oktoba 2015. Siku ya Jumamosi, tarehe 24
Oktoba 2015, Wagombea Ubunge katika majimbo ya Mkoa wa Dar es Salaam
watafunga kampeni katika maeneo ya majimbo yao kwa namna mahsusi.
Tathmini ya Kampeni
Kama Chama, tumeridhika na ubora na ukubwa wa kampeni
tulizofanya licha ya changamoto za hapa na pale. Dkt. Magufuli na Ndugu
Suluhu wamefanya kazi kubwa, na kwa bidii kubwa, na maarifa makubwa.
Wamekuwa barabarani kwa siku 57 wakifanya mikutano kati ya 8 hadi 12 kwa
siku. Imani yetu ya ushindi inatokana na kazi kubwa waliyofanya. Pia,
CCM inawashukuru viongozi, wapenzi wa washabiki wake – wa makundi
mbalimbali ya kijamii – kote nchini kwa kazi kubwa ya kampeni
waliyoifanya.
Kutokana na kazi kubwa na nzuri iliyofanyika, na kutokana na
mwenendo wa tafiti huru na tafiti zetu za ndani, CCM inategemea ushindi
wa asilimia zisizopungua 69.
Uchaguzi wa Amani
CCM haitachoka kuendelea kusisitiza uchaguzi wa amani na
utulivu. Sisi kama chama kikubwa cha siasa nchini, chenye wafuasi wengi
zaidi, na chenye dhamana ya uongozi wa dola, tutatimiza wajibu wetu wa
kuhimiza utulivu kwa wapenzi, washabiki na wanachama wetu. Tunawataka na
wenzetu wafanye hivyo.
Kauli za wenzetu kwamba kura zitaibiwa ni kauli za kutojiamini
na kujiandaa kufanya vurugu. Kauli za kwamba washabiki wa UKAWA
wakishapiga kura wabaki vituoni kulinda kura si kauli za wanaotaka
uchaguzi wa amani.
Kwa utaratibu wetu wa uchaguzi, utaratibu wa pekee kwa Chama
kulinda kura zake ni kwa kupitia wakala wa vyama waliopo kwenye kila
kituo cha kupiga kura na wenye nguvu na mamlaka ya kisheria ya
kushuhudia zoezi zima, kuanzia kupiga kura, kuhesabu kura hadi kutangaza
matokeo. Kura zinapigwa na kuhesabiwa vituoni mbele ya Wasimamizi wa
Uchaguzi, Mawakala wa vyama na Waangalizi wa Uchaguzi wa ndani na nje ya
nchi. Mawakala wa vyama na Wasimamizi wa Uchaguzi wanaweka sahihi
kwenye fomu za matokeo, na matokeo hayo yanatangazwa na kubandikwa
kwenye kituo. Kwenye kituo kikuu cha Tume cha kujumlisha matokeo,
mawakala wa vyama pia huwepo na Tume hujumlisha matokeo kutoka kwenye
fomu za matokeo za vituo vya nchi nzima zilizosainiwa na mawakala wa
vyama kwenye kila kituo. Kwa viongozi wa UKAWA kuwaambia watu waingie
barabarani au kuvizunguka vituo vya kupigia kura eti ili kulinda kura
hakuna maana yoyote zaidi ya kutafuta namna ya kuhalalisha fujo, vurugu
na uporaji na kuwazuia watu wengine, hasa wanawake, kupiga kura.
Tunaviomba vyombo vya ulinzi na usalama vizuie hili jambo kwa sababu
halina nia njema.
Mkakati wa UKAWA ni kufanya vurugu baada ya kushindwa na
kutengeneza mazingira ya mgogoro wa kisiasa ili Jumuiya ya Kimataifa
iingilie kati na kupendekeza kugawana madaraka. Mkakati huo
hautafanikiwa. Tunaviomba vyombo vya ulinzi na usalama vihakikishe
ulinzi na usalama wa watu wote na mali zao siku ya uchaguzi na baada ya
uchaguzi.
CCM haitakubali hata kidogo ushindi wake kuhojiwa au kutiliwa shaka kwa sababu tu ya vurugu zilizoanzishwa na watu wengine.
Siku ya Jumamosi, CCM itatangaza namba maalum za simu kwa
Watanzania wote ili siku kabla ya Uchaguzi, siku ya Uchaguzi na mara
baada ya uchaguzi, waweze kupiga simu au kutuma ujumbe pale watakapokuwa
wanabaini au kushuhudia vitendo vya kuvuruga amani na kuvuruga
utaratibu mzima wa Uchaguzi.
Kupokea Matokeo
CCM imeweka utaratibu wa kupokea matokeo kwa kutumia Mawakala
wake moja kwa moja vituoni na kupitia mtandao wa Chama. CCM inategemea
kuwa na matokeo ya Uchaguzi nchi nzima ifikapo saa nne usiku, siku ya
Uchaguzi, tarehe 25 Oktoba 2015.
Imetolewa na:
January Makamba
MJUMBE WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA
MJUMBE WA KAMATI YA KAMPENI
22 OKTOBA 2015