Thursday, October 22, 2015

Mkuu wa Jeshi (IGP) Apiga Marufuku Mikusanyiko ya Watu siku ya Kupiga Kura

Jeshi la Polisi nchini, limepiga marufuku mikusanyiko ya watu siku ya  kupiga kura kwa madai kwamba imekuwa ndiyo chanzo cha uvunjifu wa amani.

Pia, Jeshi hilo limesema mikusanyiko ya aina yoyote haitakiwi baada kuhitimishwa kwa kampeni  Oktoba 24, mwaka huu badala yake wanaweza kukusanyika na kusherehekea baada ya matokeo kutangazwa.

Tamko hilo limetolewa leo na mkuu wa jeshi (IGP), Ernest Mangu  akiwa kwenye mazungumzo na wanahabari kuhusu Uchaguzi Mkuu utakaofanyika siku ya jumapili.

Amesema uzoefu wa jeshi hilo unaonyesha kuwa uwepo wa watu kwenye mikusanyiko baada kupiga kura una sababisha vitendo vya uvunjifu wa amani.

Alipoulizwa na wanahabari kuruhusiwa kwa mikusanyiko hiyo katika chaguzi zilizopita, Mangu alijibu: “Polisi inafanya kazi na kupanga mikakati yake kutokana na hali halisi ya mazingira ilivyo, uchaguzi huu ni tofauti na zilizopita.”

Mikusanyiko au vikundi hivi  vinachangia pia kuwatisha watu  wasiopiga kura .Ndiyo maana tunasema  kampeni zikiisha  na ukishapiga kura rudi nyumbani kwako. Kikundi au watu watakaokiuka sheria na taratibu za uchaguzi kwa kisingizio cha kulinda kura, jeshi halitawavumilia,” amesema.

Mangu amesema lengo la kupiga marufuku mikusanyiko hiyo ni kuhakikisha mchakato wa kupiga kura unamalizika katika hali ya amani na utulivu. Amesisitiza kuwa jeshi la polisi linaongozwa na falsafa ya kuelimisha, kushauri, kushawishi na kutumia nguvu inapobidi.

Tumejiandaa vizuri kukabiliana na watu wote watakaobanika kwenda kinyume na utaratibu. Wananchi wasiwe na wasiwasi siku hiyo, wajitokeze kwa wingi kupiga kura, ulinzi utaimarishwa,” amesema Mangu.

No comments:

Post a Comment