MAMBO 5 YALIYOMPONZ LOWASSA
Waziri Mkuu wa zamani na aliyekuwa mtangaza nia ya kugombea urais wa
Serikali ya Jamhuri ya Muungano Tanzania, Edward Lowassa akipokea fomu
zilizosainiwa na wadhamini wake.
TAYARI Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimemtangaza Waziri wa Ujenzi, John
Pombe Joseph Magufuli kuwa mgombea urais mwaka huu huku Samia Suluhu
Hassan akiwa mgombea mwenza, lakini bado jina la mgombea aliyekatwa,
Edward Lowassa linazungumzika, safari hii yakibainishwa mambo matano
yanayoolezwa ndiyo yalichangia kukatwa kwake.
Akizungumza na
Uwazi juzi mjini hapa kwa sharti la kutotajwa jina lake gazetini, mjumbe
mmoja wa Halmashauri Kuu ya CCM-Taifa (Nec) alisema nguvu ya Lowasaa
kichama ilikuwa kubwa lakini mambo hayo matano ndiyo yalisababisha
akashindwa kufikia hata hatua ya Tano Bora.
“Sisi
kama wajumbe, tunajua mengi. Lowassa alikuwa mgombea mwenye nguvu,
alikuwa na watu ndani ya Nec, lakini sasa Kamati Kuu (CC) ilimkata kwa
vigezo vyake, lakini naamini ndani ya hayo mambo matano ndiyo maana
alikatwa.
MAKANISA, MISIKITI YATAJWAKwa mujibu wa
mjumbe huyo kutoka Mkoa wa Tanga, kitendo cha Lowassa kuchagisha fedha
kwa njia ya harambee kwenye misikiti na makanisa akiwa kama mgeni
mwalikwa, kulichangia CC ya CCM kumwona kama alianza kampeni mapema.
“Unajua
ndani ya makanisa mengi yanasemwa. Baadhi ya watu ndani ya chama chake
walisema alianza kampeni mapema kwa vile kule kuzungumza na waumini
kuliweza kumpa nguvu ya kisiasa. Hii nayo ilichangia,” alisema mjumbe
huyo.
STAILI YA KUTANGAZA NIAMjumbe huyo alikwenda
mbele zaidi kwa kusema kuwa, jambo la pili ambalo lilimtia doa ya
kuteuliwa Lowassa ni staili aliyoitumia kutangaza nia.
Alisema:
“Unajua CCM inakataza kabisa mtu mwenye kutangaza nia kufanya vitendo
vyovyote vyenye dalili ya kampeni. Lowassa alipoyakaribisha yale makundi
ya kumshawishi kugombea na kuzungumza na vyombo vya habari pia ilikuwa
ni kigingi kwake. Kama itakumbukwa kuwa, kuna wakati Katibu wa Itikadi
na Uenezi, Nape Nnauye ilibidi aseme.”
KUFUNGIWA NA KAMATI“Pia
itakumbukwa kuwa, Februari 18, mwaka jana, Kamati Kuu ya CCM
iliwafungia makada wake sita kwa kosa la kuanza kampeni mapema jambo
ambalo ni kinyume na utaratibu wa chama.
“Lowassa alikuwemo,
lakini wengine pia walikuwemo kama Bernard Membe (Waziri wa Mambo ya Nje
na Ushirikiano wa Kimataifa), Januari Makamba (Naibu Waziri wa
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia), William Ngeleja (Mbunge wa
Sengerema), na Frederick Sumaye (waziri mkuu msatafu).
“Sasa,
walipofunguliwa, Lowassa alionekana kama anaendelea kwa kitendo chake
cha kuzungumza na wananchi kwa kupitia kigezo cha makundi kwenda
kumshawishi,” alisema mjumbe huyo.
MATAJIRI, WAFANYABIASHARA WAKUBWAKitendo
cha kudaiwa kuwa na ukaribu na baadhi ya matajiri na wafanyabiashara
wakubwa ambao wanatiliwa shaka na baadhi ya wananchi pia kunatajwa kuwa
sababu ya CC kuamua kumuweka kando Lowassa.
DOA LA RICHMONDLicha
ya mwenyewe kuwahi kusema mbele ya mkutano mkuu wa Nec wakati fulani
kwamba, katika mchakato wa upatikanaji wa tenda ya kufua umeme kwa
Kampuni ya Richmond, hakuna alilolifanya bila serikali kuu kujua lakini
bado doa lile lililosababisha akajiuzulu uwaziri mkuu limeonekana kuwa
kikwazo kwake.
“Ni kweli Lowassa alijiuzulu kwa sababu ya nafasi
yake lakini si kwamba alihusika na ufisadi. Lakini nahisi iko haja kwake
kuweka bayana kuhusu ule mchakato kwani baadhi ya wanasiasa wenzake
wamekuwa wakitumia ishu ile kama jiwe la kumpigia.
“CC iliona
kwamba, kama wangempeleka yeye kwenye kinyang’anyiro labda wapinzani
wangetumia sakata la Richmond kujizolea kura kwa madai kwamba, Lowassa
alijiuzulu kwa sababu hiyo,” alisema mjumbe huyo.
KUTOKA NDANI ZAIDIHata
hivyo, pia kuna madai kwamba, wajumbe wa CC walimtafakari Lowassa kwa
umakini na kugundua kuwa, alitakiwa kukatwa jina mapema kabla ya kuingia
kwenye Tabo Bora.
“Kama Kamati Kuu ya CCM ingempitisha Lowassa
kwenye Tano Bora, hakuna ambaye angemshinda mbele ya safari kwenye Nec
na Mkutano Mkuu. Alikuwa na nguvu kubwa kwa wajumbe. Ndiyo maana
wakamdhibiti kule mwanzoni kabisa,” kilisema chanzo kimoja na kuongeza:
“Lakini
hata Nec na Mkutano Mkuu walipopelekewa jina la Magufuli walifurahia
kwa sababu hana makundi ndiyo maana akazoa hizi kura 2104 na ndiye
mgombea aliyepeleka hofu kwenye vyama vya upinzani (Ukawa) kwa sababu
hana kashfa.”
KISA CHA KUKATWA MEMBEChanzo hicho kilisema kuwa, Bernard Membe ilibidi akatwe ili kutuliza upepo wa kisiasa ndani ya chama.
“Unajua
Membe ndiye aliyekuwa mpinzani mkubwa wa Lowassa. Kuingia kwake kwenye
Tano Bora na kuachwa Lowassa kusema kweli kulizua taharuki kubwa. Baadhi
ya watu walikusudia kuibua uasi. Ndiyo maana ukawasikia wajumbe
wakiimba wana imani na Lowassa wakati mwenyekiti wetu (Jakaya Kikwete)
akiingia ukumbini.
“Ilibidi jina la Membe likatwe ili kambi ya
Lowassa waone kifo cha wengi ni harusi na upepo mbaya ukatulia ndani ya
chama la sivyo mpaka leo (Jumapili) kungekuwa bado Tano Bora iko
mikononi mwa wajumbe wa Nec,” kilisema chanzo hicho.