MAMBO HAYA KUMI(10) YANAWEZA KUOKOA MAHUSIANO AU NDOA YAKO
Katika pitapita nimekutana na hii mada hapa nikaona niwashirikishe na mwenzangu karibu upata hii elimu nawe hata kama wajua si mbaya kurudia.
Mahusiano sio jambo rahisi. Haishangazi kuona kwamba eneo la mahusiano ya binadamu, iwe ni kwenye ndoa, mapenzi, kazi, biashara na jamii ni mojawapo ya eneo linalopewa kipaumbele cha kila aina. Wataalamu wa saikolojia kila siku wanakesha wakijaribu kugundua mbinu mpya za kuboresha mahusiano ya binadamu.
Pamoja na “ugumu” wa mahusiano ya kibinadamu, yapo mambo kadhaa ambayo yanakubalika miongoni mwa wengi wetu kwamba yakifanyika kwa uwazi,upendo na bila hila, yanaweza kusaidia sana katika kuboresha mahusiano hayo. Haya hapa ni mambo 10 ambayo yanaweza sio tu kuboresha bali hata kuokoa mahusiano yako hususani mahusiano ya kimapenzi au ndoa.
1.Kuomba Msamaha (Samahani)- hakuna binadamu aliye
kamili. Sote tuna mapungufu. Mapungufu hayo huja au kuwa dhahiri kwenye
mahusiano na hata kwenye ndoa. Kuna kukosea. Kuna kumkosea mwenzako. Na
mara nyingine unaweza kukosea kwa bahati mbaya tu bila kukusudia.
Ukigundua kwamba mwenzako hajafurahishwa na ulichofanya au kutofanya,
omba msamaha. Hata kama huelewi kwa undani kwanini mwenzako kakasirika
au hata kama wewe unaona ni jambo dogo tu, omba msamaha.
2.Tumia Neno Tafadhali- Unapoomba kufanyiwa au
kusaidiwa kitu, tumia neno tafadhali au naomba. Badala ya kusema Baba
Nanihii, niletee maji ya kunywa,sema, “Baba nanihii tafadhali naomba
niletee maji ya kunywa”. Ni maneno madogo tu lakini yanatosha kuonyesha
heshima na upendo kwa mwenzako.
3. Sema Asante(Shukuru)- Kila unapopewa kitu, kufanyiwa
jambo, kusifiwa nk onyesha upendo wako kwa kusema “Asante”. Usiposema
asante usishangae siku nyingine usipopewa au kufanyiwa kitu fulani.
4. Mwambie mwenzako Unampenda- Anajua kwamba unampenda
na pengine ndio maana yupo na wewe. Lakini hakikisha unamkumbusha.
Usimchukulie poa tu. Hapana. Haya mwambie mwenzako unampenda sasa hivi.
5. Samehe na Sahau- Kama nilivyosema hapo juu, binadamu
hatupo kamili. Tunakosea. Mara nyingine tunakosea kila mara na kwa
jambo lile lile. Jifunze kusamehe na kusahau. Usisamehe kwa minajili ya
kuzuga amani ili ulipize kisasi. Samehe na sahau. Usikumbushe
yaliyopita. Jifunze kutokana na yaliyopita ila samehe na muombe Mungu
usahau.
6 Ongea Lugha Ya Umoja Badala ya Umimi- Binadamu
tu-wabinafsi. Ni hulka. Tunajiangalia sisi kwanza kabla ya kumwangalia
mtu mwingine hata akiwa mpenzi, mume au mke. Lakini ukitaka mahusiano
yadumu, ni muhimu kubadili “lugha”. Badala ya kuongelea mambo katika
umimi, ongea katika wingi(sisi). Kwa mfano badala ya kusema,’ nyumba
yangu au gari langu” (hususani kwa walio kwenye mahusiano ya ndoa) sema,
“nyumba yetu na gari letu”. Hutopungukiwa kitu ila utaijaza akaunti
yako ya mahusiano mema.
7. Muite kwa Jina Lake- Ushakwenda mahali kama benki vile ukasoma jina la mhudumu aliyepo mbele yako kupitia kitambulisho chake kisha ukamuita kwa jina? Uliona jinsi alivyokupa huduma nzuri zaidi? Binadamu (hususani wanaume) tunapenda kusikia majina yetu yakitajwa. Ni hulka. Hakikisha unamuita mwenzako kwa jina lake. Litumie katika mazungumzo ya kila siku na kila mara.
8. Sikiliza- Kuna nyakati mpenzi wako anachotaka ni
sikio lako tu. Sikiliza kwa makini anachokuambia. Onyesha wazi kwamba
unasikiliza. Epuka na tabia ya “kumsikiliza” mwenzako huku unachezea
simu yako au unakodolea macho televisheni.
9. Mheshimu- Hili linaonekana kuwa la wazi, si ndio?
Kwa bahati mbaya mahusiano mengi yanavunjika huku wanaoachana wakisema
“kutoheshimiwa” ndio sababu kubwa ya wao kuamua kujitoa. Kila mtu ana
jinsi yake ya kuona anaheshimiwa au kudhauraliwa. Kwa makini jaribu
kujua mambo yanayomfanya mwenzako aone umemdharau au kutomheshimu.
Ikiwezakana muulize. Msome. Kisha yaepuke kama ukoma.
10 Msaidie Mwenzako- Ni muhimu sana kusaidiana. Hata pale ambapo mwenzako hajaomba msaada, fikiria kama Ingekuwa wewe ungehitaji msaada? Kama ni ndio, basi msaidie. Kwa mfano, msaidie kupika, kufua, kusafisha gari, kununua mahitaji ya Nyumbani, kusafisha nyumba, kuvalisha watoto. Kila inapowezekana (na mara nyingi inawezekana) msaidie.
KILA LA KHERI WOTE!
No comments:
Post a Comment