Sunday, January 10, 2016

Wafanyakazi 360 wa Kiwanda cha Saruji cha Dangote Wakamatwa Kwa Kufanyakazi Nchini Bila Kibali

Mpekuzi blog
Wafanyakazi zaidi ya 360 wa kiwanda cha saruji cha Dangote mkoani Mtwara, wamekamatwa kwa kufanya kazi nchini bila kuwa na vibali vya Uhamiaji.
Kamatakamata hiyo imekuja baada ya agizo la Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga la kuwakamata wahamiaji haramu na wageni wanaofanya kazi bila vibali.
Jana, ofisi ya Uhamiaji ya mkoa ilifanya operesheni katika kiwanda hicho, lakini haikupewa ushirikiano na uongozi.
Ofisa Uhamiaji wa mkoa, Zakayo Mchele alisema walifika kiwandani hapo kufanya ukaguzi, lakini walikosa ushirikiano kutoka kwa Meneja Mkuu aliyefahamika kwa jina la Vidya Digixt.
Mchele alisema kutokana na meneja huyo kutotoa ushirikiano, wanamshikilia ili kusaidiana na Uhamiaji kuwabaini wafanyakazi wanaoishi bila uhalali na pia watamfikisha mahakamani.
Alisema licha ya kukosa ushirikiano, wafanyakazi 117 wa kiwanda hicho walipeleka maombi ya kutaka kupewa vibali vya kazi.
Mchele alisema walifanya msako katika mpaka wa Kilambo na Wilaya ya Tandahimba na kuwakamata watu 48 raia wa Ethiopia ambao walisafirishwa kwa malori kutoka Kenya.
“ Pia, tuliwakamata raia wengine wawili wa Msumbiji wakiwa na kadi za kupigia kura (za Tanzania) na kukamatwa siyo kwamba msako ulikuwa haufanyiki siku za nyuma,” alisema.
Alisema mwaka jana idadi ya watu walioingia nchini bila kibali kwa Mkoa wa Mtwara walikuwa 121.
Ofisa huyo alisema katika operesheni hiyo kesi zilizopelekwa mahakamani ni 36 ambazo zilikamilika na wahusika kutiwa hatiani na kutozwa faini, huku wengine wakipewa adhabu ya kutumikia kifungo.

No comments:

Post a Comment