Kesi ya Mtanzania ( Rashidi Mberesero) Anayetuhumiwa Kwa Ugaidi Kenya Yaanza Kusikilizwa
Mpekuzi blog
Shahidi
katika kesi ya shambulio la kigaidi lililofanyika mwaka jana katika
Chuo Kikuu cha Garissa, Kenya ameiambia mahakama kuwa Mtanzania Rashidi
Mberesero anayetuhumiwa kushiriki, alikuwa akiswali katika msikiti ulio
karibu na chuo hicho kwa siku tatu mfululizo.
Kolombo
Adao ambaye ni imamu wa Msikiti wa Garissa alidai mbele ya Hakimu wa
Mahakama ya Mlimani, Daniel Ogembo kuwa Mberesero aliondoka katika
mazingira ya kutatanisha Aprili 2 mwaka jana huku akiacha begi lake
msikitini.
“Alikuwa
mwerevu mno na aliweza kuisoma Quran. Nilikutana naye mara ya kwanza
asubuhi ya Machi 30, 2015 wakati nafungua msikiti,” alieleza shahidi huyo.
Kwa
mujibu wa Adao, Mberesero alikuwa muumini wa kipekee kwani kila siku
alikuwa akifika msikitini saa 10:35 alfajiri, wakati mwingine kabla ya
adhana.
Shahidi
huyo alidai kwamba Aprili Mosi mwaka jana alipofungua msikiti asubuhi
alimkuta Mberesero akiwa ameshafika na alimpa kipaza sauti aweze kuwaita
waumini wanaotakiwa kuswali asubuhi siku hiyo.
“Nilikuwa naumwa kifua siku hiyo. Kwa hiyo nilimpa kipaza sauti atangaze kwa sababu alikuwa anaijua vyema Quran,” shahidi huyo alidai.
Kuhusu
sababu za Mberesero kuwapo Garissa, Adao aliiambia mahakama kuwa
aliambiwa na kijana huyo kuwa alikwenda kumsalimia mjomba wake lakini
alifukuzwa kwa kuwa ni Mwislamu.
“Alinieleza kuwa baba yake ni Mdigo wa Tanga na mama yake ni Mkamba wa Kenya,” alieleza Adao.
Kwa
maelezo ya shahidi huyo, siku ya tukio Mberesero ambaye alizoea kuvaa
kanzu alionekana amevaa mavazi ya kawaida na kofia kama mtu anayeficha
uso.
Mahakama
ilielezwa kuwa siku ya tukio aliingia msikitini na kuweka begi lake
kwenye kona ya msikiti lakini hakusali na baadaye aliondoka na
kuliacha.
No comments:
Post a Comment