Sunday, August 23, 2015

Rais Kikwete, Mkapa na Makongoro Nyerere Waishambulia UKAWA kwa zamu......Magufuli Aahidi Kuwashughulikia Mafisadi


Rais Jakaya Kikwete, Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa na Mtoto wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Makongoro Nyerere wameshambulia vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).

Wakizungumza kwa zamu katika Uwanja wa Jangwani jijini Dar es Salaam wakati wa kufungua kampeni za chama hicho wamesema, mgombea wa UKAWA hana sera za wapinzani.

Katika mkutano huo uliotawaliwa na vijembe kwa UKAWA Rais Kikwete bila kutaja jina amesema, katika umoja huo kuna mgombea anayesimama kama mgombea binafsi kwa kuwa, sera zake ni tofauti na chama anachosimama kugombea.

Alikwenda mbali na kuonesha kushangazwa kuwa, mmoja vyama viwili ambavyo sio msingi wa chadema ndio vimesimama katika ngazi ya urais na mgombea mwenza wake.

Rais Kikwete aliwalenga Mgombe Urais wa Chadema, Edward Lowassa aliyejiunga na chama hicho akitokea CCM pamoja na Juma Duni Haji aliyejiunga na Chadema akitokea Chama cha Wananchi (CUF).

“Wagombea sio wa Chadema. Mmoja ni CCM na mmoja ni CUF.., Pale kuna mgombea urais ambaye unaweza kusema kama mgombea binafsi maana ana sera zisizofanana na chama,” amesema Rais Kikwete na kuongeza “lakini wameyataka wenyewe.”

Hata hivyo Kikwete hakumwacha Waziri Mkuu Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Frederick Sumaye aliyejiunga na chama hichi siku moja iliyopita.

Kikwete amesema, pamoja na Sumaye kujieleza lakini hakumwelewa alichokuwa akikusudia “nimejaribu kusikiliza anasema nini lakini sikuelewa kabisa,” amesema.
.
Hata hivyo amesema, CCM haikubahatisha kumteua Dk John Magufuli kuwa mteule wa chama hicho katika urais na kwamba, “tumemweka kwa sifa zake, tunataka rais anayeipenda nchi na anayependa wananchi wa nchi hii.”

“Magufuli anayo sifa hiyo. Tumesema, hatutaki kuchukua mgombea mwenye makando kando mengi na tukatumia muda wetu mwingi kujitetea sisi na yeye kabla ya kuomba kura. Tunamtaka mgombea mwaminifu, mwadilifu. Safari hii Mungu kamchagua Magufuli.”

Kabla ya Rais Kikwete kuzungumza, alitanguliwa na Mkapa ambaye amesema, kuna vyama vinawadanganya Watanzania kuwa wanawatafutia ukombozi-wapumbavu.

“Kuna chama kimoja tu cha ukombozi hapa Tanzania, ni CCM iliyotokana nas ASP na TANU. Kuna vyama vinawadanganya Watanzania eti wanataka kuwakomboa wananchi-wapumbavu, nenda nchi zote za jirani uliza chama cha ukombizi Tanzania watakwambia CCM. Nina kila sababu ya kusema wapumbavu,” amesema.

Hata hivyo amesema, haitoshi kusema mtu anauchukia umasikini peke yake.

“Haitoshi kusema unauchukia umasiki, lazima useme unauchukiaje umasikini?” amesema Mkapa.

Lowassa katika hotuba zake mbele ya wananchi kwenye safari zake za kutafuta wadhamini alipokuwa CCM na hata baada ya kuhamia Chadema, amekuwa akisema anauchukia umasikini-haupendi.

Hata hivyo Mkapa amesema, timu ya CCM ni madhubuti kwa kuwa Magufuli anapenda kushirikiana na wenzake, yupo mstari wa mbele katika kutekeleza mambo yote ya umma na kwamba, wakati wote ni mfano wa tabia nzuri kwa vitendo vyake.

Makongoro ndio aliyefungua ukurasa wa mashambulizi kwa UKAWA kwa kumvaa Sumaye baada ya kujiengua CCM.

Makongoro amesema, anamshangaa Sumaye aliyejiunga na vyama vinavyounda UKAWA na kwamba, alipaswa kukubali matokeo ya kushidwa

Makongoro alianza kwa kibwagizo “kuna mmoja-au niache?- kuna yule kaka yangu mmoja nasikia afya yake sio kweli. Kuna huyu mwingine wa jana (Sumaye)?

“Sumaye tumpige kanzu au tumuache hivihivi, kwani angetulia tungeshughulika naye, kajileta mwenyewe sasa mimi nifanyeje, nimpige tobo?” amesema na kuongeza;

“Sumaye akiwa Waziri Mkuu na kaka yangu Kikwete (Rais Kikwete) waliingia kwenye tano bora, Sumaye alikuwemo, kura zake hazikutosha zikatosha za Kikwete, kwa kuwa aliingia tano bora akasema, chama kizuri.

“Miaka 10 baadaye tano bora hakuingia- Sumaye akatuambia mkimpa Lowassa kugombea urais hiki chama mimi nitahama, sasa huyo ni mkweli ama muongo. Hii ndio shida ya kusema uongo, kusema rahisi kuukumbuka tabu,” amesema Makongoro.

Katika mkutano huo, mgombea mwenza wa CCM, Samia Suluhu Hassan amesema, atasimamia na kuwawezesha akina mama.

Pia ameahidi kusimamia pesa Sh. Mil 50 zinazotolewa na serikali kwa ajili ya kupelekwa vijijini.

“Nitasimamia kuwawezesha akina mama, pesa za vijijini Sh. Mil 50 zitatoka kwa ajili ya vijijini nitazisimamia. Mimba za utotoni nitasimamia kuhakikisha zinaondoka, pia nitahakikisha maji yanapatikana na kusaida akina mama wote,” amesema.

Akizungumzia uzowefu alioupata amesema, amekuwa karibu na Makamu wa Rais wa sasa, Dk. Mohammed Gharibu Bilal hivyo hakuna wasiwasi katika nafasi hiyo.

“Nilikuwa kwenye mikono mizuri ya Dk. Bilal, najua kazi zilivyo nawahakikishia Ofisi ya Makamu wa Rais itasiamama vyema kutekeleza ilani ya uchaguzi pamoja na muungano,” amesema.

Dk. Magufuli amewaahidi watanzania kujikita katika kutetea maendeleo ya wananchi kwenye Nyanja zote.

Dk. Magufuli amesema utawala wake utajikita katika masuala ya kilimo, afya, uchumi na amani ya nchi.

“Watanzania natambua mnapenda kuona mabadiliko, nitasimama vizuri katika miradi ya uchumi. Watanzania nawahakikishia shida na matarajio yenu nayajua, nayafahamu na natambua ninao uwezo wa kuyashughulikia.

"Mnataka suala la rushwa, wizi serikalini vikomeshwe haraka. Kwa kuwa palipo na rushwa ufisadi hakuna maendeleo, nitasimamia hilo,”amesema.

Amesema, kama atachaguliwa “nitahakikisha naunda mahakama maalumu ya kushughulikia mafisadi na majizi yafungwe haraka.”

No comments:

Post a Comment