Saturday, August 22, 2015

Mkapa, Mwinyi kumnadi Dk. Magufuli Jangwani.


Marais wastaafu, Ali  Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa, wanatarajiwa kushiriki kwenye ufunguzi wa kampeni za kumnadi mgombea wa urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli Jumapili, jijini Dar es Salaam.

Pia uzinduzi huo unatarajiwa kupambwa na wasanii mbalimbali wa muziki wa kizazi kipya wakiongozwa na Nasiib Abdul (Diamond) na bendi mbalimbali ikiwamo ya Tanzania One Theatre (TOT).

Kadhalika, wamo marais wastaafu wa Zanzibar, mawaziri wakuu wastaafu, viongozi wakuu wastaafu wa CCM na viongozi wa serikali, makada kutoka mikoa mbalimbali nchini na wananchi wanatarajiwa kuhudhuria.

Habari za uhakika kutoka vyanzo vyetu ndani ya CCM zinaeleza kuwa baada ya kampeni hizo kuzinduliwa jijini Dar es Salaam, ziara ya kumnadi itaelekea mikoa ya kusini.

Mikoa hiyo ni Lindi, Mtwara na Ruvuma na kwamba ratiba hiyo itafuata hadi kumalizika nchi nzima.

Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye (pichani), alipoulizwa, alisema ratiba kamili itatolewa baadaye kwa vyombo vya habari.

Kuhusu wageni mbalimbali wa heshima ambao wanatarajiwa kuhudhuria uzinduzi huo alisema hafahamu na kwamba mgeni rasmi ni mgombea mwenyewe ni Dk. John Magufuli.

Nape akizungumzia ilani ya uchaguzi ya chama hicho, alisema inatarajiwa kuzinduliwa siku ya kuzindua kampeni.Mpekuzi jana ilishuhudia uwanja wa Jangwani ukifanyiwa usafi.

Magari ya ya kubeba mizigo yalionekana yakisomba taka na udogo uliokuwa ukichimbwa eneo hilo.

No comments:

Post a Comment