Thursday, May 7, 2015

Godbless Lema Atamba Kushinda tena Ubunge bila Kampeni.


Mbunge wa Arusha mjini kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Godbless Lema amesema kuwa atashinda tena ubunge kwa tiketi ya chama hicho, hata asipopiga kampeni.
 
Aidha amesema ni vyema wananchi wa Jiji la Arusha na maeneo mbalimbali nchini wakajitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura, ili waweze kupiga kura na kuchagua wagombea wanaotaka kuongoza.
 
Lema amesema hata asipopiga kampeni za kutetea kiti hicho yeye bado ni mbunge na uchaguzi huu ataendelea kushinda kwani wagombea wanaopitapita kutangaza nia na baadhi yao kugawa unga, bila mboga anawafananisha na bendera zinazoendelea kupepea bila kuwa na mafanikio yoyote.
 
Amesema ni vyema wananchi wanajitokeza kwa wingi kujiadikisha ili waweze kutumia haki yao siku ya uchaguzi na kuongeza idadi ya wabunge na madiwani wengi kupitia Chadema.
 
Lema amesema kwa jinsi anavyoona hadi sasa maandalizi ya uchaguzi mkuu yanasuasua, hivyo yawezekana daftari hilo likitangazwa kuhamia mkoani Arusha siku zinaweza kuwa chache hivyo ni vyema wananchi wakawa makini, wakisikia daftari linapita mkoa fulani wajitokeze kwa wingi kujiandikisha, ili waweze kuchagua wabunge wengi kutoka Ukawa.
 
Amesema anatarajia kufanya mkutano Ijumaa ya wiki hii, ataongelea mambo mbalimbali ikiwemo suala la uandikishwaji wa daftari la kupiga kura, sambamba na kujadili jinsi fedha ya Tanzania thamani yake inavyozidi kushuka.

No comments:

Post a Comment