Thursday, October 22, 2015

Mke wa Mtikila ataka iundwe Tume kuchunguza kifo cha mumewe


Mama Mtikila Ameongea Haya Mbele ya Waandishi wa Habari:


Ndugu Wana-Habari,

Kabla sijawaeleza kilichonilazimisha kuwaomba kuongea nanyinyi, kwanza niwarudishe nyuma kama miaka saba iliyopita, ndipo maisha ya Baba, Mchungaji, Mwenyekiti na mume wangu, Mchungaji Christopher Reuben Mtikila yalipoanzwa kuwindwa:-

MAUWAJI YA MHESHIMIWA CHACHA ZAKAYO WANGWE

Mara tu baada ya kifo cha mbunge huyo, mchungaji Mtikila alitoa ripoti maalumu juu ya mauaji yake ambayo ilimjengea uadui kati ya baadhi ya vyama vya siasa pamoja na wafanyabiashara wakubwa ambao hadi leo ni wapinzani wa serikali hapa nchini.--Mchungaji Mtikila hadi anafikwa na mauti aliendelea kupata upinzani wa aina hiyo hiyo kwa sababu mchungaji Mtikila aliendelea kudai haki ya marehemu Chacha Zakayo Wangwe.

MAUAJI YA BULIGI

Hii ilimwongezea uadui baada ya kusema/kuandika ukweli juu ya watutsi wa nchi jirani kuvamia nchi yetu kwa mtindo wa kujifanya wafugaji wasio hama. L.I.F. ilibaini uharamia huo kuwa hawakuwa wafugaji bali walikuwa askari wa Jeshi la Rwanda waliokuwa na mpango wa kutumika na Chama kimoja cha siasa hapa nchini ili kuleta mapigano yatakayo zaa mapinduzi. Jambo hili lilisababisha Rais wa Rwanda, Paulo Kagame kutamka hadharani kuwa angemkamata Mwenyekiti wa chama chetu cha DP--kwa lengo la kumuua na Serikali yetu inajua hilo. Mara baada ya ripoti hiyo kutolewa na Mchungaji Mtikila "operation Kimbunga" ilizaliwa na kuponya nchi yetu; lakini chuki na uadui uliendelea dhidi ya Mchungaji Mtikila.

MCHAKATO WA URAIS NDANI YA CCM

Ikumbukwe kuwa mara baada ya mchakato wa kutafuta mgombea urais kwa tiketi ya CCM kuanza DP ilitoa ripoti iliyowahusu wagombea sita wa CCM waliotumia mapesa mengi na kuanza kampeni kabla ya muda na kusisitiza kuwa Lowasa ni mtu asiefaa kuwa Rais wa nchi yetu. Na baada ya kuhama CCM, Mwenyekiti wetu aliendelea kutoa tahadhari hadharani jinsi Lowasa asivyofaa kuwa Rais wa nchi yetu hivyo likaendeleza uadui wake na Chama.

VITISHO--KUANZA

Mchungaji Mtikila alipata nafasi ya kuongea katika kipindi kinachorushwa na STAR TV cha asubuhi "TUONGEE" ndipo alipoanza kupata vitisho toka kwa watu mbali mbali wengine kupitia kwenye simu wengine uso kwa uso. Kipindi cha kwanza kilirushwa tarehe 25/9/2015 na kufuatwa na cha tarehe 27/9/2015. Alipotoka studio hiyo asubuhi ya tarehe 27/9/2015 ndipo watu waliodai wametumwa na Mhe. Edward Ngoyai Lowasa na Mhe Frederick Sumaye walimuomba wampe nusu bilioni na apewe maovu ya mgombea urais wa CCM ili afunike-alivyowamaliza wao.

Mchungaji Mtikila aliwapuuzia mbali wale wajumbe waliyotumwa kwani aliawaambia kuwa yeye siyo malaya wa kuuza utu wake kwa tende na haluwa. Yakumbukwe kuwa mahojiano kwenye hivyo vipindi viwili kwenye STAR TV hayakuwa yanatetea mtu au chama yalikuwa yanatetea Taifa letu lipate Rais anayefaa.

Kwa hiyo basi wale waliochukizwa na mahojiano hayo ni wale amabo hawakubaliani na mawaidha ya Mchungaji Mikila aliyokuwa anawatahadharisha watanzania juu ya Mh. Lowasa kuwa hatari kwa usalama wa taifa letu kama atakuwa Rais wa nchi yetu. Hao watu ndiyo waliopanga mpango mzima wa mauaji ya Mh. Mtikila ambaye ni mume wangu.

Wakati yuko Bunda mjini watu wasiofahamika walimfuatafuata na tarehe 26/9/2015 gari lake lilifukuzwa na gari usiku wakati alipokuwa anatoka Bunda kwenda Mwanza kufanya mahojiano ya tarehe 27/9/2015 na Star Tv.

MPANGO WA MAUAJI HALISI

Mchungaji Mtikila alitafutiwa gari na Victor James Manyahi ambayo ilikuwa na madereva wawili. Mchungaji madereva hakuwajua. Hata mimi madereva hao sikuwajua wala sikuwaona. Walikodiwa kutoka wapi sijui, wala sijui wanafanana vipi. Na wala sijui Victor Manyahi alikodi gari hilo kwa nani na makubaliano yepi sijui.

Kwa hivyo basi, kwenye gari aliyosafiri nayo Mchungaji Mtikila kulikuwamo madereva wawili na Mgaya Patrick (tunayemfahamu). Wakati wanakwenda gari lilipata ajali Makambako. Wakati wanarudi wakapata “ajali” Msolwa Mchungaji akapatwa na mauti peke yake. Ajali ilikuwa mbaya sana-IKAUWA MTU MMOJA AMBAYE NI MCHUNGAJI MTIKILA NA HAKUKUWA MAJELUHI HATA MMOJA.-Cha ajabu kwangu ni kuwa mtu ambaye alikuwa ni mlinzi wa kujitolea (body guard) Mgaya Patrick sijawahi kumuona usoni mwangu kabla na hata baada ya mazishi kuja kuniambia kilichotokea eneo la ajali. Pamoja na juhudi zangu zote za kumpigia simu mara kadhaa aje anijuze Mgaya Patrick hajatokea hadi sasa ndugu zangu wanahabari ninapoongea nanyi. Lakini si kwamba huyu mtu hayupo, yupo lakini sijaonana naye, kwa nini sijui. Je ndugu zangu wanahabari nimuweke Mgaya Patrick kwenye fungu gani?

Ndugu Wana-Habari, baada ya kuwaelezea yote hapo juu nakuja kwenye suala nililowaomba nikutane nanyi ili niongee mbele yenu kuwa sikubaliani na uchunguzi kuwa Mchungaji Christopher Reuben Mtikila amekufa kwa ajali. Sikubaliani na kazi ya Polisi kuwa wamefunga file lao kutokana na Post-mortem report kuwa mauti yaliotokana na ajali. Nafuta kabisa taarifa--iliyotoka katika gazeti la Nipashe chini ya kichwa cha habari kuwa “FAMILIA YAFUNGUKA KIFO CHA MTIKILA”-ilitolewa mapema mno. Kila mwanafamilia alikuwa hajawa tayari kutoa kauli yoyote. Kwa niaba ya Chama na familia ya Mchungaji Christopher Reuben Mtikila naomba tusaidiwe yafuatayo kusudi haki ya mpendwa wetu-ionekane--inatendeka:-

Kwa sababu mtandao umeanza kuficha ukweli ili kulinda wauaji; tunaomba Mheshimiwa Rais aingilie utata wa kifo cha Mheshimiwa Mchungaji Christopher Reuben Mtikila kwa kuunda tume ya uchunguzi isiyohusisha polisi.

Tunaiomba mamlaka ya mawasiliano yaani Tanzania Communications Regulatory Authority, TCRA itusaidie yafuatayo:-

(a)----Mtu aliyeweka picha kwanza alfajiri kuonyesha mauti ya Mhe Mchungaji Mtikila alikuwa wapi? Kwenye tukio? Au ni hao wauaji walikuwa wanatoa taarifa kwa waajiri wao kuwa wamekamilisha kazi!

(b)----Mtu aliyeweka picha ya Dr. Jean-Bosco Ngendahimana kwenye mtandao kuwa ndiye anahusika na mauti ya Mhe. Mch. Mtikila na kumusingizia kuwa amekamatwa na polisi akiwa anajiandaa kukimbia;

(c)-----Wote wanaoendelea kumhusisha Dr. Jean-Bosco Ngendahimana na mauaji ya Mhe. Mchungaji Mtikila, tuwafahamu ili watueleze vizuri.

Ukweli na haki ni vya Mungu hakuna anayeweza kuviua au kuvizuia. Tunategemea Mungu atawatumia watendaji wa Serikali/nchi yetu wenye nia njema, na makusudi yaliyonyooka kwa ajili ya nchi yetu ili Mhe. Mchungaji Mtikila apewe haki dhidi ya wauaji wake.

Asanteni,


Georgia C . Mtikila,

-KM DP/Msemaji-Familia

No comments:

Post a Comment