Monday, July 6, 2015

Makongoro Oging’ na Haruni Sanchawa
NIkweli dunia imekwisha! Ni vigumu kuamini mtoto mdogo ambaye anahitaji uangalizi na ulinzi kutoka kwa jamii anageuzwa mwanamke na kuingiliwa kwa nguvu hadi mauti. Huu ni unyama na ukatili wa hali ya juu.

Tukio hilo la kutisha lilitokea katikati ya wiki iliyopita, Tabata Msimbazi jijini Dar ambapo mtoto Ester Banzi ,5, (pichani) alikutwa na mauti baada ya kuingiliwa kimwili na mwanaume ambaye inadaiwa alimteka kwanza.
Akizungumza na Gazeti la Uwazi kwenye msiba huo, mama mdogo wa marehemu Ester aliyejitambulisha kwa jina la Watende Hamis huku akitokwa machozi mfululizo, alisema:

“Siku ya tukio, ilikuwa saa 5:30 asubuhi tukiwa nyumbani, dada (mama wa marehemu aitwaye Rebeka) alikuwa ameinjika sufuria ya ugali jikoni kwa ajili ya chakula cha mchana.
“Akamtuma Ester dukani akanunue unga. Alimpa shilingi 1,200. Si mara ya kwanza Ester kutumwa dukani kwa vile ni jirani tu.

“Tulimsubiri Ester arudi na unga lakini alichukua muda mrefu. Ikabidi tumfuate dukani, hatukumuona. Tuliwauliza watoto wenzake ambao anapenda kucheza nao, wakasema walimuona amebeba mfuko cha Rambo huku akiongozana na baba mmoja.


“Basi, tuliendelea kumtafuta bila mafanikio. Ikabidi tutoe taarifa kwa baba yake ambaye akaingiwa na wasiwasi, akaenda kutoa taarifa kwenye Kituo cha Polisi Tabata Shule.“Ndani ya masaa matatu baba yake akatupigia simu kwamba mwili wa Ester umeokotwa huku ukionekana alibakwa na kuharibiwa vibaya.”

Naye kijana anayeuza duka ambalo marehemu alitumwa kununua unga, bila kutaja jina lake alikiri Ester kufika dukani hapo na kupimiwa unga kisha akaondoka.

Baadhi ya wananchi majirani na maeneo hayo waliohojiwa na waandishi wetu kuhusiana na tukio hilo walisema kwamba wao walimuona mtoto huyo akifuatana na mwanamume mmoja, lakini hawakumtilia mashaka kutokana kwamba walifikiri ni ndugu yao.

Mtu mmoja ambaye mwili wa marehemu ulikutwa jirani na nyumba yake, naye alizungumzia tukio hilo:
“Sisi tulisikia sauti ya mtoto akiomba msaada. Tulipata hofu ikabidi tukaangalie eneo lile ndipo tulipouona mwili wa mtoto huyo. Tulipomchunguza tukagundua alibakwa kwani nguo yake ya ndani ilikuwa pembeni.

“Inaonekana huyo mtu hakuchukua muda mrefu kufanya kitendo hicho. Tulimpigia simu Mkuu wa Kituo cha Polisi Tabata Shule, Afande Kobelo akaja na timu yake. Hili tukio nahisi lina ushirikina ndani yake.”

Mmoja wa askari aliyefika katika eneo la tukio ambaye hakutaka kutaja jina lake kwa vile siyo msemaji mkuu wa jeshi hilo alisema mwili wa mtoto huyo ulionekana kuingiliwa kimwili, marehemu alivunjwa shingo na kutobolewa upande wa kushoto kichwani.Marehemu Ester alizikwa wiki iliyopita mkoani Morogoro. Mungu ailaze mahali pema peponi roho ya marehemu. Amina.

No comments:

Post a Comment