Nchimbi Afunguka baada ya CCM Kulikata Jina lake Kwenye Kinyang'anyiro cha Ubunge
Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Mbunge wa Songea Mjini, Dk. Emmanuel Nchimbi (pichani), amefunguka kuhusu mambo kadhaa na kueleza kuwa Watanzania wanapaswa kuelewa kuwa kutofautiana katika vyama vya siasa ni jambo la kawaida katika nchi yenye demokrasia.
Dk.
Nchimbi alisema hayo jana ikiwa ni siku moja baada ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM) wilaya ya Songea Mjini kuikataa fomu ya kuomba kuwania
ubunge aliyochukuliwa na wananchi kwa madai haikuwa imekidhi vigezo.
“Ninachowambia
Watanzania tuzoee kutofautiana, kutofautiana katika vyama vyetu ni
jambo la kawaida katika demokrasia, tunaweza kutofautiana katika
mapendekezo, lakini tukifika kwenye maamuzi tunakuwa kitu kimoja kuunga
maamuzi tuliyoafikiana na huo ndio utaratibu mzuri wa kujenga
demokrasia,” alisema.
Dk.
Nchimbi ambaye alikuwa akihojiwa na kituo cha Radio One jana asubuhi,
alisema demokrasia ya kutoelezana ukweli siyo demokrasia bali demokrasia
ya kweli ni ya uhuru wa fikra.
Alisema
mtu ambaye hapendi CCM iwe shwari ni mtu ambaye haitakii mema nchi na
kwamba hana mpango wa kuhama chama hicho kwa sababu amelelewa na CCM.
Aliongeza
kuwa taarifa za kwamba yeye na makada kadhaa wamehojiwa na chama
kuhusiana na kauli walizozitoa wakati wa vikao vya uteuzi wa mgombea
urais kuwa hawakuridhishwa na mchakato huo hazina ukweli.
”Mimi
nimekulia CCM na bado nitaendelea kuwa CCM kutokana na misingi ya
kifikra na kisera, sasa kama kuna mtu anayewaza kuwa naweza kuhama CCM
hiyo ni fikra ya kijinga sana,” alisema.
Kamati
ya Siasa ya CCM wilaya ya Songea Jumapili iliyopita ilikataa kupokea
fomu ya kugombea ubunge ya aliyojaziwa Dk. Nchimbi na baadhi ya wakazi
kwa madai kuwa haikukidhi vigezo.
Hata
hivyo, mwezi uliopita Dk. Nchimbi aliandaa mkutano wa wanachama wa CCM,
viongozi na wananchi na kuwashukuru kwa ushirikiano waliompatia katika
kipindi chake cha uongozi kisha kuwatangazia kwamba hatagombea tena
ubunge katika jimbo hilo mwaka huu.
Dk.
Nchimbi alikuwa akitajwa kuwa huenda atagombea katika Jimbo la Mbinga
Magharibi lililopo wilayani Nyasa ambalo lilikuwa likishikiliwa na
marehemu Kapten John Komba, aliyefariki dunia mapema mwaka huu.
No comments:
Post a Comment