Membe Arudisha Fomu Ya Urais......Akana Kuhusika Na Ufisadi Wa Mabilioni Ya Libya.
MAKADA maarufu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamerejesha fomu na kufafanua mambo kadhaa ambayo yamekuwa yanazungumzwa juu yao kama njia ya kujiweka sawa kabla ya uteuzi kufanywa na vikao vikuu vya chama hicho.
Mmoja wa waliorudisha fomu ni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ambaye
wakati akirudisha fomu za kuomba kuteuliwa na kusema kuwa wanaochukulia
suala la urais ni la kufa au kupona wana matatizo kwani anayejua Rais wa
Tanzania ajaye ni Mungu.
Alisema safari yake ya kutafuta wadhamini ilikuwa na misukosuko mingi
ikiwemo kutokea ajali tatu lakini hakuna ambaye alikuwa ameumia sana.
Akiwa ameongozana na mke wake, Tunu Pinda alisema mwana CCM mkomavu ni yule ambaye yuko tayari kukubali matokeo.
Alisema mpaka sasa ni wanachama wa CCM 42 waliojitokeza kugombea
lakini katika hatua ya kwanza ni majina matano tu yatakayoteuliwa na
kundi kubwa litaondolewa.
“Mimi sitegemei kwenye mchujo wa watu watano watokee watu wa
kunung’unika kwani kila mtu aliyefika kuchukua fomu alikuwa anafahamu
kuwa kutakuwa na mchujo kama tuko wengi wako watano kisha unakwenda
ngazi ya pili, hakuna sababu ya kunung’unika,” alisema.
Alisema baadaye kuna kwenda kwenye Mkutano Mkuu atabaki mmoja.
“Utanung’unikia nini? Kuna kushinda na kushindwa na kuna kupata na
kukosa na ukisema suala la Urais ni kufa au kupona basi una matatizo,
ifike mahali wana CCM wapate mtu ambaye wanadhani anaweza kusaidia
kuongoza,” alisema.
Pia alisema waliojitokeza mwaka huu kuchukua fomu ni wengi.
“Tuliojitokeza tusinuniane, kwa nini haniungi mimi mkono, na wewe usione
jambo hili ni nongwa na usijione mapenzi ya Mungu yako kwako tu,”
alisema.
Pia aliwataka viongozi wenzake washirikiane kumuunga mkono mgombea
mmoja atakayepeperusha bendera ya CCM. “Anayejua rais wa Tanzania
atakuwa nani ni Mungu peke yake,” alisema.
Mwakyembe arudisha fomu
Waziri wa Afrika Mashariki, Dk Harrison Mwakyembe jana alirudisha
fomu na kusema CCM itapata ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu
utakaofanyika Oktoba mwaka huu kutokana na kutekeleza ilani yake vizuri
na wananchi kuwa na imani kubwa na chama hicho.
Mwakyembe ambaye alirudisha fomu jana mchana alisema katika safari
yake ya kutafuta wadhamini mkoani ameweza kuwaona wanachama wengi wa CCM
ambao wanaonesha imani kubwa na chama chao.
Alisema kila alipokutana na wana CCM waliojitokeza kumdhamini kwa
tathmini aliyofanya tangu kuanza kwa siasa ya vyama vingi nchini CCM,
itashinda ushindi wa kimbunga kwani mtaji upo kutokana na kazi kubwa
iliyofanya serikali ya awamu ya nne katika utekelezaji wa ilani.
“Tumejipanga kuhakikisha wanaingia kwenye uchaguzi kifua mbele
kutokana na kutekeleza ilani,” alisema.
Pia alisema kwa upande wa pili
wana kazi ya kuhakikisha yote mazuri yaliyofanywa na CCM yanasemwa.
“Tuna kazi ya kuhakikisha kuwakumbusha wananchi barabara za lami na
mafanikio mengi yamepatikana na serikali ya awamu ya nne ya CCM,”
alisema.
Alisema kazi kubwa ni kuhakikisha umma unatambua CCM imefanya mambo
mengi kutokana na upotoshaji unaofanywa na wapinzani kuwa CCM haijafanya
lolote.
Pia alisema CCM kuwa na wagombea wengi waliojitokeza mwaka huu ni
dalili njema za CCM kutoa fursa za kupatikana mmoja ambaye kila moja
atamuunga mkono ili kuweza kukivusha chama.
Dk Mwakyembe alisema yuko tayari kumuunga mkono mgombea
atakayeteuliwa na chama. Awali alisema amezunguka katika mikoa 15 katika
kutafuta wadhamini.
Dk Mwele Malecela
Mwanachama mwingine wa CCM aliyerudisha fomu jana ni Dk Mwele
Malecela ambaye alisema pamoja na kazi kubwa iliyofanywa katika uongozi
wa awamu nne bado kuna watu wanaoishi kwenye umasikini uliokithiri.
Alitoa kauli hiyo wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari.
Alisema alifanikiwa kupata wadhamini katika mikoa 20 ikiwemo 17 ya
Tanzania bara na mitatu ya Zanzibar.
Alisema wananchi wameonekana kufarijika kuona wanafuatwa kwenye
maeneo ya kata walipo. Alisema ameweza kuzunguka mikoa tisa kwa siku nne
hali inayoonesha kuwa kazi kubwa imefanyika katika ujenzi wa barabara
za lami kuunganisha mikoa.
‘Pamoja na maendeleo na kazi kubwa ya awamu zote bado kuna umasikini
uliokithiri lazima kuliangalia suala hilo kama kiongozi na kulitafutia
ufumbuzi,” alisema.
Alisema aliguswa sana na wanawake waliojitokeza wakiwemo wazee ambao
walikuwa wakitaka kumuona ni mwanamke wa aina gani ambaye anataka
kugombea Urais.
“Wanawake wamefurahi sana kuona wanawake tunajitokeza hii ni fursa
nzuri ya kuwapa moyo akinamama kugombea nafasi mbalimbali za uongozi
katika nchi,” alisema.
Membe Ayakana Mabilioni ya Libya
Membe kwa upande wake wakati anarudisha fomu akijibu swali
aliloulizwa kuhusu madai ya kuwa anahusika na ufisadi wa fedha za Libya
na kama inavyosambazwa na wapinzani wake, alisema akigundulika kuwa
alikula hata dola moja yuko tayari kujiuzulu.
“Uvumi kuwa nahusika na mabilioni ya Libya hauna mashiko kabisa
baadhi ya wanasiasa wenzangu wanajua ukweli wote huu lakini kwa makusudi
wameamua kuniunganisha na kampuni hiyo na kuwaaminisha watu ni yangu au
nina hisa maneno hayo ni ya uongo,” alisema.
Alifafanua kuwa Libya ni moja kati ya nchi wafadhili wa Tanzania
ambapo, kama ilivyo wafadhili wengine imekuwa ikiipa Tanzania misaada na
mikopo yenye masharti nafuu.
Alisema katika utaratibu huo, Tanzania na Libya zilitia sahihi
mkataba wa kubadili madeni na kuyaingiza katika miradi ambao uliweka
utaratibu wa matumizi na urejeshaji wa fedha za deni la Libya.
Alisema kumbukumbu alizonazo zinabainisha kuwa kabla ya Serikali ya
Libya kuweka saini katika mkataba wa nyongeza iliyotaka fedha hizo
zikopeshwe kwa kampuni ya Meis, upembuzi yakinifu wa mradi husika
ulifanywa kupitia vyombo vyake, na wao wenyewe kujiridhisha juu ya ubora
wa mradi huo.
Sumaye na mahakama ya rushwa
Naye Waziri Mkuu mstaafu, Frederick
Sumaye ambaye naye alirejesha fomu alisema akichagulia kuwa Rais wa nchi
ataanzisha mahakama maalumu ya wala rushwa.
Mbali na rushwa pia vipaumbele vyake ni pamoja na ufisadi, uhujumu
uchumi na kwamba ataunda chombo cha uchunguzi katika masuala hayo.
Pia alisema wakati akiwa Waziri Mkuu wa Tanzania alifanya mambo
makubwa na atahakikisha anaunda serikali inayofahamu kutimiza wajibu
wake.
‘Uchumi ninaouzungumzia si wa takwimu ni wa hali halisi, nitaangalia
pia maeneo kama viwanda vikubwa na vidogo ili watu wengi waweze
kujiajiri na kulinda viwanda vya ndani,” alisema.
Alisema atahakikisha uzalishaji wa viwanda vya ndani unaongezeka na
kunakuwa na ongezeko la mauzo ya nje ya nchi. Pia alisema ataimarisha
huduma za jamii, ikiwemo elimu, afya upatikanaji wa maji na huduma
nyingine muhimu.
Alipohojiwa kama maeneo aliyokwenda kutafuta wadhamini aliombwa
rushwa, Sumaye alisema, tangu aanze kazi ya siasa hajawahi kutoa rushwa.
“Hata maeneo ambayo nimekwenda kutafuta wadhamini sijatoa fedha hata
zilizodaiwa kwa lugha laini nilikataa kwani nilitaka nidhaminiwe na wale
walio na imani na mimi,” alisema.
Alisema wakati akiwa Waziri Mkuu alipambana na wala rushwa ambapo
aliweza kuwafukuza kazi watu 3,360 huku wengine 400 walipelekwa
mahakamani.
Balozi Mahiga
Balozi Mahiga naye wakati anarejesha fomu alisema ameenda mikoa 15
kwa gari na akawashukuru wana CCM kumlaki na kwamba wamehamasika na
wanasubiri kwa hamu uchaguzi.
Alisema kama CCM ikimpitisha kuwa mgombea atahakikisha kuwa anajenga
maadili ya uongozi ili kuondokana na vitendo vya rushwa na ufisadi.
Alisema uongozi mzuri ni ule unaojengwa katika misingi ya maadili na
atapambana na rushwa ili kukomesha vitendo hivyo ambavyo vimekuwa
vikirudisha nyuma wananchi wengi.
“Nitahakikisha ninaimarisha misingi ya umoja na mshikamano katika
nchi ikiwa ni pamoja na kudumisha muungano wa Tanzania na Zanzibar,”
alisema.
Joseph Chaggama
Mwanachama mwingine wa CCM aliyerudisha fomu jana ni Joseph Chaggama
ambaye alisema amezunguka katika mikoa 17 wakati wa kutafuta wadhamini.
Alisema anaijua CCM vizuri na jinsi Serikali inavyoendeshwa.
Alisema yeye ni mmoja wa watu wasiofahamika na sababu ya kuchukua fomu ni nia ya dhati kutoka moyoni kuwa anaweza kuongoza nchi.
Pia alisema uwezekano wa yeye kuchaguliwa lazima kutokee muujiza.
Alisema yuko tayari kuwatumikia Watanzania ikiwa atapewa ridhaa ya kuwa
mgombea wa CCM na akashinda uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka
huu.
Pia alisema yuko tayari kumuunga mkono mgombea ambaye atateuliwa na chama.
Monica Mbega
Mbunge wa zamani wa Iringa Mjini, Monica Mbega naye
alirudisha fomu na kusema kuwa chama kiliweka utaratibu mzuri wakati
wakienda mkoani kupata wadhamini katika mikoa 15 ikiwemo mitatu ya
Zanzibar.
Alisema amekamilisha kazi yake kwa ukamilifu bila matatizo na kuwashukuru wanawake wengi waliojitokeza kumuunga mkono.
Alisema suala la rushwa linategemea jinsi mtu alivyokwenda wakati akitafuta wadhamini.
Amos akemea matumizi makubwa ya fedha
Mwingine aliyerudisha fomu
hizo jana ni Amosi Siyantemi ambaye ni mtumishi wa CCM wakati ambaye
alisema kuwa kwenye mchakato wa kutafuta wadhamini baadhi ya wagombea
wameonesha matumizi makubwa ya fedha.
“Ni jambo la kujiuliza fedha hizo wamepata wapi na ni kiasi gani ni lazima wachunguzwe na kuchukuliwa hatua,” alisema Siyantemi.
Pia
alisema rushwa ni ugonjwa mbaya unaoiangamiza jamii ni lazima
zichukuliwe hatua za haraka na makusudi ili kuweza kukomesha suala hilo
kabla nchi haijatumbukia kwenye shimo la machafuko.
Alisema CCM ya sasa si kama ile ya Mwalimu Nyerere. “Tunahitaji
kurejesha haraka heshima ya CCM machoni mwa Watanzania na kwenye macho
ya Jumuiya ya Kimataifa,” alisema.
Alisema akichaguliwa kuwa Rais atahakikisha kunakuwa na huduma bora
za matibabu sanjari na bima ya afya kwa kila Mtanzania, kufanya
mabadiliko makubwa kwenye mfumo wa elimu kwa kuchukua hatua mbalimbali
ikiwemo kupunguza idadi ya masomo.
Pia alisema atapiga marufuku mauzo na manunuzi yanayofanyika nchini
kwa malipo ya dola ambapo malipo ya dola yatafanyika kwa kibali maalumu.
Pia alisema atakuwa na jukumu la kuleta mageuzi makubwa katika sekta
ya sanaa, michezo na burudani yatakayolenga kuwanufaisha kiuchumi
wananchi.
No comments:
Post a Comment