Tuesday, June 9, 2015

Kina Sheikh Farid Wagoma Kuingia Mahakamani.


Katika halia isiyo ya kawaida, Kiongozi wa Jumuiya ya Uamsho ya Mihadhara ya Kiislamu (Jumiki) visiwani Zanzibar, Sheikh Ahmed Farid na wenzake wanaokabiliwa na kesi ya kula njama na kujihusisha ya ugaidi nchini waligoma kushuka kwenye basi la magereza ili kuingia mahakamani jana kutokana na hatma ya upelelezi wa kesi yao kutojulikana.

Washtakiwa hao walifikishwa kwenye viunga vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam saa 2:50 asubuhi kwa ajili kusikiliza kesi yao iliyopangwa kutajwa jana.

Kabla ya mgomo huo, washtakiwa hao wanaotoka visiwani Zanzibar, waliiomba mahakama kuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Jaji Mkuu na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar kuwatembelea mahabusu kwa ajili ya kusikiliza kero zao kuhusiana na kushitakiwa kwao katika mahakama za Tanzania Bara badala ya mahakama za kwao, Zanzibar.

Viunga vya mahakama hiyo vilifurika askari kanzu na wenye sare za Jeshi la Polisi pamoja na wa Jeshi la Magereza kwa ajili ya kuimarisha ulinzi.

Hata hivyo, baada ya kufikishwa mahakamani hapo washtakiwa wote 23 waligoma kushuka kwenda kusikiliza kesi yao kwenye ukumbi wa mahakama hiyo.

Saa 4:56 asubuhi, mahakama hiyo iliyoketi chini ya Hakimu Mkazi Renatus Rutatinisibwa, huku upande wa Jamhuri ukiongozwa na mawakili wa serikali, Peter Njike na George Barasa, wakisaidiana na wakili wa serikali mwandamizi, Tumaini Kweka.

Wakili Njike alidai kuwa washtakiwa wamegoma kushuka kwenye basi la Jeshi la Magereza tangu wafikishwe mahakamani hapo kutoka mahabusu.

Wakili wa utetezi, Abdallah Juma, alidai kuwa upande wao hauna taarifa kuhusiana na  washtakiwa kugoma kuingia mahakamani na kwamba, upande wa Jamhuri ndiyo una wajibu wa kujua chochote kuhusu washtakiwa waliopo mahabusu.
 
Wakili Kweka, alidai kuwa askari magereza wamefanya juhudi za kuwataka washuke kwenye basi ili kuingia mahakamani lakini imeshindikana.

Mheshimiwa, Mei 25 mwaka huu, mahakama yako ilitoa amri kwamba kesi hii itatajwa leo… Jamhuri tunaomba washtakiwa wahesabike kwamba hawajafika mahakamani. Pamoja na kwamba wapo katika viunga vya mahakama, tunaomba mahakama itoe amri wapangiwe tarehe nyingine na wafike mahakamani,” alidai Wakili Kweka wa upande wa Jamhuri.

Hakimu Rutatinisibwa alisema mahakama haiwezi kuwafuata washtakiwa nje ya ukumbi unaoendesha shughuli zake na kwamba, (mahakama) inaendesha kazi zake kwa mujibu wa sheria, hivyo inaahirisha kesi hiyo hadi Juni 18 mwaka huu itakapotajwa tena.

Mbali na Sheikh Farid, watuhumiwa wengine ni Noorid Swalehe, Ally Hamis Ally, Jamal,   Nassoro Hamad, Hassan Bakari, Ahtari Humoud, Mohamed Isihaka, Abdallah Hassan,  Hussein Mohamed,  Juma Sadala,  Said Kassim,  Hamis  Amour,  Abubakar Abdallah, Salum Ali, Salum Amour, Alawi Othuman, Rashid Ally, Amir Hamis, Kassim Salum na Said Shehe pamoja na wenzao.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka manne likiwamo la kula njama ya kuingiza watu nchini kushiriki katika vitendo vya ugaidi,, kusaidia na kuwezesha kufanyika vitendo hivyo.

Ilidaiwa kuwa kati ya Januari 2013 na Juni 2014, washtakiwa hao kwa pamoja walipanga njama ya  kutenda makosa hayo ya kula njama za kusaidia na kuwezesha kufanyika vitendo vya kigaidi.

Ilidaiwa kuwa  katika kipindi hicho na maeneo tofauti nchini,  Sheikh Farid na Sheikh Mselem Mselem waliwaingiza Sadick Absaloum na Farah Omary nchini ili kushiriki kutenda makosa ya ugaidi.

Shekh Farid anadaiwa kuwa katika kipindi hicho, akiwa anajua kuwa Sadick na Farah wametenda makosa ya kigaidi, aliwahifadhi.

Baaada ya kusomewa mashtaka hayo, washtakiwa hao hawakuruhusiwa kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo hadi Mahakama Kuu.

No comments:

Post a Comment