Thursday, May 7, 2015

Zitto Kabwe Afunguka Kuwa Alipofukuzwa CHADEMA Alitamani Kujiunga NCCR-Mageuzi......Kazungumzia Pia Anakotoa Pesa za Kufanya Mikutano


Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo Zitto Kabwe amefunguka na kusema kuwa alipofukuzwa Uanachama katika chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) alitamani kujiunga na Chama Cha NCCR-Mageuzi kwani ndicho chama ambacho kilikuwa  kinaendana na itikadi yake anayoifuata na kuiamini ambayo ni itikadi ya Ujamaa.
 
Zitto Kabwe alifunguka haya jana alipokuwa akichat Live kupitia ukurasa wa facebook wa EATV katika kipengele cha KIKAANGONI .

Zitto Kabwe alisema kuwa alishindwa kujiunga na Chama hicho cha NCCR-Mageuzi kutokana na kuwepo kwa matatizo hivyo aliona siyo vyema kujiunga nacho, ndiyo maana alifikiri kuwa na chama cha siasa ambacho kitakuwa na misingi na itikadi ambayo yeye anaiamini na kuisimamia. 
 
Katika hili moja ya shabiki alitaka kujua kwanini aliamua kujiunga na ACT Wazalendo na kuacha kujiunga na chama kilichokomaa kisiasa kama TLP,NCCR-Mageuzi,CUF, au CCM na majibu ya Zitto yalikuwa kama hivi.
 
"Nilifikiria hivyo pia lakini nikaona kuwa ni vema sasa kuwa na chama cha siasa ambacho kina itikadi ninayoifuata na kuiamini nayo ni itikadi ya Ujamaa.
 
"Chama cha NCCR-M mageuzi pekee ndio kinakaribia kuwa na itikadi hiyo lakini napo kulikuwa na matatizo ambayo kujiunga kwangu nao ingekuwa sio vema. Pili mimi ni mpiganaji. 
 
Wengine wananiita jeshi la mtu mmoja! Sio kweli lakini. Hivyo kwenda chama kichanga ni ujasiri wa hali ya juu. Mungu atasaidia hakitakuwa chama kichanga baada ya uchaguzi mkuu mwezi Oktoba 2015".
 
"Mimi sio mwanzilishi wa ACT Wazalendo isipokuwa waanzilishi walikuwa watu ninaoshabihiana nao kwenye itikadi kama Prof. Kitila Mkumbo na Ndugu Mwigamba" Aliongeza Zitto Kabwe.
 
Kiongozi huyo wa ACT Wazalendo ambaye kwa sasa amekuwa akiitwa majina mengi ya ajabu ajabu kama msaliti,Yuda, kibaraka wa CCM na mengine mengi alisema kuwa hilo ni suala la kawaida katika siasa maaana hayo ni maneno tu ambayo hata baadhi ya viongozi wakubwa katika vyama vya siasa walishaitwa majina hayo ila anasisitiza jambo kubwa na la muhimu ni kumpima kwa kazi zake ambazo amezifanya bungeni katika kipindi chote alipokuwa mbunge na jinsi alivyoweza kujenga uwajibikaji kwa baadhi ya viongozi.
 
"Hayo ni maneno ya kisiasa tu. Hata Marando aliwahi kuitwa Msaliti. CUF waliwahi kuitwa mashoga. NCCR na Mbatia waliwahi kuitwa pandikizi. 
 
"Ni maneno ya kisiasa tu ambayo hayaongezi ugali kwenye sinia. Muhimu ni kuni judge kwa kazi ambazo nimefanya Bungeni katika kipindi changu. Kazi ya kujenga uwajibikaji." 
 
Lakini mbali na kuonyesha kuwa kumekuwa na changamoto katika siasa za Tanzania hususani ndani ya vyama vya siasa Zitto Kabwe alizidi kusisitiza kuwa chama cha siasa ni itikadi hata hivyo umoja wa vyama vya siasa ni muhimu sana katika kujenga Demokrasia imara.
 
"Chama cha siasa ni itikadi. Hata hivyo umoja wa vyama ni muhimu sana katika kujenga demokrasia imara"
 
Uchaguzi Mkuu 2015
Kiongozi huyo wa ACT Wazalendo ameonyesha kuwa huenda kwa mwaka huu katika uchaguzi mkuu Tanzania ikaandika historia nyingine kwa Rais wa chama kimoja kukabidhi nchi kwa Rais wa chama kingine, hii inamaana kuwa huenda Rais Jakaya Kikwete akakabidhi nchi kwa Rais kutoka chama cha upinzani.
 
"Kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu Rais wa chama kimoja anaweza kukabidhi nchi kwa Rais kutoka chama kingine." 
 
Lakini hapo hapo kiongozi huyo ndipo alipoonyesha wazi kuwa kwa upande wake yeye atagombea nafasi ya ubunge kupitia chama chake cha ACT Wazalendo na kusema kuwa mpaka sasa hajajua ni jimbo gani anakwenda kugombea nafasi hiyo ya ubunge. 
 
"Nitagombea Ubunge mungu akipenda. Jimbo gani bado sijaamua" 
 
Kutokana na hili mashabiki walihitaji kujua siku akiweza kufanikiwa kushika nafasi ya Rais wa nchi hii ni jambo gani la kwanza kuanza kufanya .
 
"Ikitokea nimekuwa Rais wa Tanzania Kila Waziri ataandika kabisa barua ya kujiuzulu na inabakia kuweka tarehe tu ili akiboronga anawajibika bila hiyana. Uwajibikaji ni nguzo muhimu sana katika kuleta maendeleo nchini."
 
Lakini Zitto Kabwe aliweka sawa kuwa katika kipindi cha sasa ikitokea uchaguzi wa Oktoba hautofanyika au mwaka huu usipofanyika uchaguzi anaamini nchini itaingia katika machafuko. 
 
ACT Inatoa  Wapi Pesa za Ziara
Moja wa shabiki wa ukura wa facebook alihoji kuwa pesa zinazosaidia cha cha ACT Wazalendo kuweza kufanya ziara zake mikoani tena kwa speed kubwa na ni chama kichanga hizo pesa wanatoa wapi ukizingatia kuna vyama vya siasa vipo miaka mingi sana lakini havijaweza kufanya hata ziara ndani ya mji wa Dar es Salaam sababu vinakosa pesa za kufanya hivyo, kiongozi huyo wa ACT Wazalendo Zitto Kabwe alisema kuwa ni dhamira tu na yeye pesa za kufanya hivyo anachangiwa na wananchi wanaopenda harakati zake.
 
"Ni dhamira tu. Wapo watanziania wengi sana wanaoamini katika kazi za Zitto Kabwe hawawezi kukubali nishindwe kufanya siasa sababu ya fedha. Ninachangiwa hata na mama lishe."
 

Natamani  Kujiunga UKAWA
Katika hatua nyingine Zitto Kabwe ameweka wazi kuwa katika moja ya mipango yao ilikuwa ni kuunganisha nguvu kama ambavyo awali ametuleza kuwa ili kujenga demokrasia imara ni lazima vyama vya siasa viweze kuunganisha nguvu zao hivyo anadai alitamani waweze kuungana na UKAWA katika kuona ni jinsi gani wanaweza kufumua mfumo wa uongozi ulipo sasa wa chama tawala ila akadai kuwa UKAWA walikataa.
 
Kiongozi huyo wa ACT Wazalendo Zitto Kabwe alimaliza kwa kuwaambia mashabiki kuwa kuna matapeli wanatumia jina lake na kujifanya wanatoa mikopo hivyo yeye hausiki nao na wananchi wanapaswa kutambua hao watu ni matapeli na amesema mara nyingi huwa anatoa taarifa sehemu husika juu ya watu wao.
 
"Hao ni matapeli. Akaunti yangu ni hii na Zitto Z Kabwe pekee. Nyingine ni watu tu wanatengeneza na huwa tunazitolea taarifa."-Zitto  Kabwe

No comments:

Post a Comment