Tanzania Kuendelea Kupokea Wakimbizi wa Burundi
Mpekuzi blog
TANZANIA
imetangaza kuendelea kupokea wakimbizi wanaoingia nchini kutoka Burundi
kutokana na kuendelea kwa machafuko nchini humo huku waandamanaji
wakipambana na polisi kupinga hatua ya Rais Pierre Nkurunzinza kugombea
urais kwa muhula wa tatu.
Akizungumza
katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma kabla ya kuanza safari ya
kukagua kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu Wilayani Kasulu jana, Waziri wa
Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe alisema uamuzi huo unalenga kutoa nafasi
ya wakimbizi hao kupata mahitaji ya msingi.
Waziri
Chikawe alisema wakimbizi wana haki ya kulindwa na kuthaminiwa kama
raia wengine kwa hivyo uamuzi wa Serikali kutoa nafasi zaidi kwa
wakimbizi nchini una nia ya kutoa nafasi zaidi ili kupata mahitaji yao
ya msingi ikiwa ni pamoja na misaada mbalimbali ya binadamu kupitia
mashirika mbalimbali.
“Kama
nchi tumeona ni vema kuendelea kuwapokea, hivyo tumetoa nafasi ya
kuendelea kuwapokea wakimbizi hawa kutoka nchini Burundi mpaka hapo hali
ya usalama nchini mwao itakapoimarika,” alisema Chikawe.
Waziri
Chikawe pia aliyaomba mashirika mbalimbali ya kimataifa kusaidia
wakimbizi hao wanaoendelea kumiminika nchini kwa wingi kusaidiana na
serikali ili kuwapa huduma za malazi na chakula.
Mratibu Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP),
Alvaro Rodriguez alisema mpaka sasa hali ya siasa Burundi inatia shaka
kwa kuwa inaweza kusababisha ongezeko kubwa la wakimbizi Tanzania.
Alisema
Tanzania ni nchi ya mfano wa kuigwa kwa namna inavyoshughulikia
wakimbizi ikiwa ni pamoja na kuwapokea hiyvo umoja wa mataifa unaungana
na nia ya Serikali ya Tanzania kuwasaidia wakimbizi hao.
Alisema
kutokana na kuendelea kupokea idadi kubwa ya wakimbizi, kambi ya
Nyarugusu imeendelea kuelemewa na wakimbizi hivyo kuliomba shirika la
Umoja wa Mataifa kusaidia uwezekano wa kuongeza kambi nyingine kwa ajili
ya wakimbizi hao.
No comments:
Post a Comment