Wednesday, May 20, 2015

BENCHI la ufundi la Yanga chini ya Mdachi, Hans van Der Pluijm, limedaiwa kufanya maamuzi magumu ambayo kwa namna moja au nyingine, yatawashangaza wadau wengi wa klabu hiyo.

Imedaiwa kuwa kocha huyo ambaye ameiongoza Yanga msimu huu kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara, amependekeza wachezaji saba kuondolewa kutokana na mchango yao finyu msimu mzima, akiwemo mchezaji mkongwe wa klabu hiyo, Jerry Tegete na Danny Mrwanda aliyetua katika usajili wa dirisha dogo msimu uliopita akitokea Polisi Moro.

Habari za kuaminika kutoka Yanga zinasema kuwa mbali na Tegete na Mrwanda, nyota wengine ambao wamepitiwa na panga la kocha huyo mwenye msimamo mkali ni Nizar Khalfan, Rajab Zahir, Hussein Javu, Edward Charles na Hassan Dilunga.
Habari zinasema kuwa walio na mikataba watatolewa kwa mkopo, ambao ni Dilunga na Edward

“Kwa hali hiyo wachezaji hao hatutakuwanao tena msimu ujao kutokana na kocha kapendezeka waachwe waende wakatafute maisha sehemu nyingine ili nafasi zao tuweze kusajili wengine wenye uwezo na sifa za kuwa Yanga.

“Anataka msimu ujao kikosi chake kiwe chenye wachezaji wa ushindani ambao wataisaidia Yanga kufanya vizuri katika michuano ya ligi kuu na ile ya kimataifa, hivyo baada ya tathmini yake ya msimu uliomalizika, ameona nyota hao  hawatakuwa na msaada, ndiyo maana amewependekeza waondoke zao,” kilisema chanzo hicho cha habari.

Alipoulizwa juu ya jambo hilo, Katibu Mkuu wa Yanga, Dk Jonas Tiboroha, alisema kuwa si muda wa kuzungumzia suala hilo na kwamba muda ukifika wataweka wazi kila kitu.“Tuvumiliane katika hili, muda ukifika kila kitu kitakuwa wazi,” alisema Tiboroha.Alipotafutwa Tegete jana mchana alijibu kwa kifupi: “Mimi sijazipata hizo taarifa (za kutemwa).” Kisha akakata simu.

No comments:

Post a Comment