DU! Kazi kwelikweli! Habari ya mjini kwa sasa ni mtoto mzuri Bongo 
Movies, Wema Isaac Sepetu ‘Madam’ kuwania Ubunge wa Viti Maalum Mkoa wa 
Singida kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), lakini nyuma yake kuna 
habari zinazodai kuwa mrembo huyo ameingiwa na hofu ya kukatwa jina kama
 ilivyotokea kwa Mbunge wa Monduli, Edward Ngoyai Lowassa aliyekuwa 
mmoja wa watia nia ya kugombea urais, Amani lina mkanda kamili.
ALIVYOENGULIWA LOWASSA
Lowassa alikuwa miongoni mwa makada 33 kati ya 38 walioenguliwa na 
Kamati ya Maadili ambayo ilipitisha majina matano pekee katika kikao cha
 Kamati Kuu, Halmashauri Kuu na baadaye Mkutano Mkuu kupitisha Mbunge wa
 Chato, Dk. John Pombe Magufuli kuwa mgombea urais kwa Tiketi ya CCM.
TUJIUNGE NA CHANZO
Chanzo kilicho karibu na staa huyo kimepenyeza ‘ubuyu’ kuwa, Wema ambaye
 anashikilia Taji la Miss Tanzania 2006/07, ameingiwa na hofu hiyo baada
 ya kuona Lowassa ambaye ana sifa ya kukubalika kama alivyo yeye 
ameenguliwa na kikao cha Kamati ya Maadili ya CCM.
“Bibie (Wema) anajiamini, anakubalika kweli lakini kitendo cha Lowassa 
ambaye alikuwa anaonekana kukubalika kimemtia hofu na kuona kumbe 
kukubalika pekee si silaha ya ‘kuwini’ kupitishwa na chama,” kilisema 
chanzo hicho.
CHANZO CHAZIDI KUTIRIRIKA
Chanzo hicho kilizidi kwenda mbali zaidi kwa kudai hofu hiyo iliongezeka
 kwa Madam hususan baada ya kusambaa kwa kuwepo kwa watu wasiompenda 
kupandikiza chuki kwamba baadhi ya skendo zilizomgusa zinaweza 
kumpotezea sifa ya jina lake kupitishwa na Halmashauri Kuu ya chama 
chake.
“Si unajua tena Madam kwenye maisha yake ya sanaa amepitia skendo za 
hapa na pale, hiyo inaweza kuchangia kumtia hofu maana wabaya wake 
wanaweza kuitumia kama silaha hivyo amekuwa akitoa chozi na kumuomba 
Mungu amfanikishe,” kilisema chanzo hicho.
SKENDO INACHANGIA KUMPOTEZEA SIFA?
Duru mbalimbali za habari zinaonesha kwamba kitu kikubwa kinachoangaliwa
 kwa kiongozi ni suala la uwajibikiaji na si tabia binafsi au skendo.
Wapo viongozi ambao walikuwa na skendo lakini wameweza kupitishwa na 
wananchi wao na kuwatumikia vizuri kuliko hata wale walionekana wasafi.
“Si kweli kwamba skendo ndiyo kigezo kikuu cha kumpitisha mgombea, mbona
 watu kama akina Mike Sonko (alikuwa Mbunge wa Kenya), marehemu Amina 
Chifupa (alikuwa Mbunge Viti Maalum, Vladimir Vladimirovic Putin (rais 
wa urusi) na wengine wengi, walikuwa au walipata skendo lakini walifanya
 vizuri katika uongozi wao,” alisema mwanaharakati mkubwa wa siasa 
nchini aliyeomba hifadhi ya jina.
NAPE ANENA
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alipoulizwa kama kuna 
uwezekano wa kumuengua mgombea yeyote kutokana na skendo au chuki 
zinazoezwa na baadhi ya wanachama wa chama hicho, alisema si kweli bali 
wao wanafUata taratibu na kanuni walizojiwekea na si vinginevyo.
“Sisi tuna kanuni na taratibu za chama, hiyo ndiyo misingi yetu. 
Hatumuengui mtu kwa chuki binafsi wala kitu kingine chochote zaidi ya 
kufuata kanuni zetu,” alisema Nape.
WEMA ANASEMAJE?
Akizungumza na mwanahabari wetu hivi karibuni, Wema alikiri kupata hofu 
hiyo kwa muda lakini ameshajiamini kutokana na kumuomba Mungu ambaye 
amekuwa akimtanguliza katika kila jambo analolifanya.
“Kusema kweli mtu unapotaka kufanya jambo unapaswa kujiamini, hata mimi 
mwanzo nilikuwa nimejipa matumaini ya hali ya juu kwamba Lowassa 
atapita, lakini bahati mbaya akakatwa, naamini Mungu yupo, mimi naswali 
usiku na mchana, Mungu atanisimamia katika hili,” alisema Wema.