NA WAANDISHI WETU
MAKADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliotangaza nia ya kugombea urais, sasa ni wazi wanapigana vikumbo kila kona ya nchi.
Hatua hiyo inatokana na kila mtangaza nia kwa nyakati tofauti kutoa kauli nzito.
Wapo
 makada ambao kauli zao zinaonyesha wazi kuwa kuna mgongano ndani ya 
CCM, huku wengine wakitangaza nini watakifanya endapo watateuliwa 
kuongoza nchi.
MEMBE: SINA UNDUGU NA JK
WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, amesema hana undugu na Rais Jakaya Kikwete.
Membe
 ambaye pia ni Mbunge wa Mtama, alikanusha undugu wake na Rais Kikwete 
mjini Dodoma jana wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya 
kuchukua fomu ya kuomba kuwania urais kupitia CCM.
Akijibu maswali ya
 waandishi wa habari, alisema hana undugu na Rais Kikwete, ingawa baadhi
 ya nchi ambazo amekuwa anatembelea wamekuwa wakimfananisha naye.
Alisema baadhi ya sehemu hushindwa kumtofautisha kiasi cha kumpa hadhi ya urais ikiwamo kumwomba wapige naye picha.
“Mimi
 siyo ndugu wa damu wa Rais Kikwete, nimechukua sura, rangi na ufupi 
kutoka kwa mama yangu. Kwa bahati mbaya na Rais Kikwete pia kachukua 
sura kutoka kwa mama yake, bado mama zetu siyo ndugu.
“Hata hivyo, 
kungekuwa na aibu gani kiasi cha mimi kuficha kwamba Rais Kikwete siyo 
ndugu yangu, ningepata hasara gani kukubali ni ndugu yangu kwa sababu 
kama ni madaraka tayari nilishajipatia vyeo,” alisema.
Alisema wakati
 mwingine huwa anaenda katika kaburi la wazazi wake kuwaomba awasamehe 
wale wote ambao wanazusha maneno kuhusu undugu wake na Rais Kikwete.
“Wazazi wangu walishafariki dunia, wawaache wapumzike kwa amani na waniache niendelee na njia yangu,” alisema.
Katika hatua nyingine, Membe aliahidi kutoa ushirikiano kwa waandishi wa habari pindi akiingia madarakani.
Alisema ataangalia sheria zote zinazohusu vyombo vya habari.
Membe
 alikuwa akijibu swali jinsi atakavyohakikisha vyombo vya habari 
vinafanya kazi kwa uhuru kutokana na kauli yake kwamba endapo atapata 
nafasi ya kuongoza nchi, atavitaka kuhakikisha vinafichua rushwa.
“Ili
 waandishi wa habari wafanye kazi kwa uhuru, lazima waandaliwe mazingira
 ya kufanya kazi vizuri, tutaziangalia sheria zote zinazoendesha vyombo 
vya habari.
“Lengo ni kujenga mazingira mazuri ya kuwaweka waandishi 
wa habari kuwa na uhuru wa kuandika chochote bila kuogopa kufungwa au 
kunyanyaswa,” alisema Membe.
Alirejea kauli ya Rais Barack Obama wa 
Marekani walipokutana katika mazungumzo ambapo alisema ‘kabla ya 
kufikiria kuvishitaki vyombo vya habari kwa kumshambulia, lazima kwanza 
ashauriane na mwanasheria wake’.
Alisema hadi sasa Rais Obama hajawahi kushitaki chombo cha habari chochote kutokana na mwanasheria huyo kukataa.
“Rais
 Obama aliniambia nchi inapumua kupitia waandishi wa habari, nchi inatoa
 dukuduku lake kupitia vyombo vya habari na mimi nitapita huko,” 
alisema.
Akizungumzia baadhi ya vipaumbele vyake kama akifanikiwa kuwa rais, alisema atahakikisha nchi inakuwa na uchumi wa viwanda.
Alisema jambo hilo litawezekana kutokana na ugunduzi wa gesi asilia, hivyo nchi itakuwa na nishati ya kutosha.
“Nitahakikisha
 Serikali yangu inazingatia utawala bora, utawala wenye nidhamu, isiyo 
na ufisadi na inayopiga vita rushwa na harufu yake,” alisema.
LOWASA APATA MAPOKEZI MAKUBWA GEITA, AZOA WADHAMINI 3,000
WAZIRI
 Mkuu wa zamani, Edward Lowassa jana aliingia wilayani Geita na kupokewa
 na umati wa wananchi ambako alidhaminiwa na zaidi ya wana CCM 3,000.
Kaimu
 Katibu wa Wilaya ya Geita, Killian Balindo alisema waliotakiwa 
kumdhamini Lowassa katika wilaya hiyo ni wanachama 45, lakini 
waliojitokeza wamefikia zaidi ya 3,000.
Akizungumza na wananchi 
waliokusanyika mbele ya ofisi ya CCM Mkoa wa Geita, Lowassa alisema japo
 haruhusiwi kufanya kampeni ameahidi kushughulikia matatizo ya maji, 
wachimbaji wadogo na mawe yaliyoisha dhahabu (magwangala).
“Hayo ya 
bodaboda, mamantilie kushughulikia. Nikiingia ikulu ni kuweka tu kalamu 
nyekundu. Kazi yangu ikikamilika nitashughulikia magwangala,” alisema 
Lowassa.
Kuhusu wachimbaji wadogo, alisema atawapa kipaumbele kwa kuwamilikisha maeneo ya uchimbaji na mitaji.
“Nilipokuwa
 mbunge miaka ya 80, niliondoa shilingi bungeni kupinga wachimbaji 
wadogo kunyanyasika. Nitahakikisha kila mchimbaji anapata eneo lake. 
Serikali inajua maeneo yote yenye madini. Halafu tutawapa fedha ili 
wawekezaji wakubwa wakija waweze kushindana,” alisema Lowassa.
Msafara
 wa Lowassa ulikuwa na magari, pikipiki na baiskeli huku ikisindikizwa 
na helikopta ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita, Joseph Msukuma.
Awali
 Lowassa jana aliingia katika Jimbo la Chato linaloshikiliwa na Waziri 
wa Ujenzi, Dk. John Magufuli na kupata mapokezi makubwa ya wanachama 
waliojitokeza kumdhamini.
Dk. Magufuli ambaye pia amechukua fomu za kugombea urais bado hajafika jimboni humo kutafuta wadhamini.
Lowassa aliingia Chato saa 8:30 mchana na kuelekea kwenye ukumbi wa ofisi ya CCM wilaya walikokuwa wamekusanyika wana CCM.
Akizungumzia
 udhamini huo, mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM wilayani humo, 
Deusdedith Katwale, alisema wanachama waliojitokeza kumdhamini wamefikia
 430.
“Tunashukuru kwa kuipa kipaumbele Chato, hiyo ina maana sana siku zijazo,” alisema Katwale.
Naye Lowassa aliwashukuru wanachama hao na kurudia wito wake wa kuchagua rais aliyebobea katika chama.
“Tunakwenda
 kuchagua rais, tutafute mtu anayekijua chama. Angalieni historia yake 
na rekodi ya mambo aliyofanya,” alisema Lowassa.
AWAPONGEZA WANA CCM PEMBA
Awali
 akiwa kisiwani Pemba jana asubuhi, Lowassa amewasifu wanachama wa CCM 
kisiwani Pemba kwa kujiimarisha dhidi ya upinzani mkali wa Chama cha 
Wananchi (CUF).
Tangu kuanza kwa siasa za upinzani mwaka 1995, CCM imekuwa katika wakati mgumu visiwani Zanzibar, na hasa Pemba.
Akizungumza
 na wana CCM wilayani Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba alikokwenda kutafuta
 udhamini kwa ajili ya kupitishwa kugombea urais kupitia chama hicho, 
Lowassa alisema wana CCM kisiwani humo wanastahili pongezi.
Alisema 
alifika kisiwani humo mara ya mwisho mwaka 1984 na kwamba akifanikiwa 
kupata urais atafanya ziara ya muda mrefu kisiwani humo.
“Nilifika hapa mwaka 1984 na sijawahi kurudi tena. Lakini endapo nitafanikiwa safari yangu, nitakuja siku mbili tatu tuzungumze.
“Nawapongeza
 kwa jitihada zenu, licha ya upinzani mkali wa CUF bado mmeendelea 
kujiimarisha. Nitakuja Pemba siku mbili tatu nitakapofanikiwa ili 
tuzungumze,” alisema.
Lowassa pia alizungumza na wana CCM wa Wilaya 
ya Chakechake, Mkoa wa Kusini Pemba na kuwapongeza kwa jitihada zao za 
kukilinda chama chao licha ya upinzani mkali.
Lowassa alifanikiwa kupata udhamini wa wana CCM 90 katika wilaya za Wete na Micheweni Mkoa wa Kaskazini.
Akizungumzia
 hali ya chama hicho wilayani Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba, mmoja wa 
makada wa CCM, Juma Amir Juma alisema wanachokitegemea ni rehema za 
Mwenyezi Mungu.
“Hatusemi tutaendelea kushindwa, Mungu ni mkubwa ipo 
siku tutashinda. Lakini hali ni mbaya sana, kwani kama Mbunge wa CUF 
anapata kura zaidi ya 5,000 wa CCM anapata kura 500, wapi na wapi? 
Lakini hatukati tamaa,” alisema Juma.
Katibu wa CCM mkoa wa Kaskazini
 Pemba, Ali Haji Makame, alisema kuna wana CCM wengi walitamani 
kumdhamini Lowassa, lakini wameshindwa kutokana na idadi maalumu kuwekwa
 na kanuni za chama hicho ambayo ni wanachama 45 kwa kila wilaya.
Lowassa
 aliwasili Zanzibar juzi na kupokewa na umati mkubwa wa wanachama wa CCM
 walioandamana naye hadi katikati ya mji wa Unguja.
Kwa ujumla Lowassa amepata wadhamini 450 katika visiwa vya Unguja na Pemba.
NYALANDU ATANGAZA MAGEUZI YA KISERA
WAZIRI
 wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, amesema endapo atafanikiwa 
kuwa Rais wa Tanzania, atahakikisha anafanya mageuzi makubwa ya kisera 
kwa kuweka vipaumbele vya uchumi ili kuwanufaisha wananchi wa kipato cha
 chini.
Alisema mageuzi hayo yataendana na mabadiliko ya mifumo ya 
kiutawala kwa kutengeneza uwiano wa mgawanyo wa rasilimali sawa kwa 
wananchi wa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wale 
wa Zanzibar.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumaliza 
ziara ya kutafuta wadhamini mjini Unguja, Zanzibar jana, Nyalandu 
alisema haitoshi kusikia pato la taifa linakua na uchumi wa nchi 
unaimarika katika ngazi ya Serikali Kuu pekee, bila ya kuwanufaisha 
wananchi wa kipato cha chini.
Nyalandu, alieleza kwamba endapo 
atapata ridhaa ya wananchi na kumchagua kuwa rais, anatarajia kuleta 
mabadiliko makubwa ya kimaendeleo katika nyanja za kiuchumi, kijamii na 
kisiasa kwa kuzingatia utu na haki ili kujenga jamii moja ya Watanzania 
watakaonufaika na matunda ya nchi yao.
Alisema jambo la kwanza 
atakapopata nafasi ya urais, atahakikisha anaondosha dhana ya watunga 
sera ambao ni wabunge na wawakilishi kuhakikisha wanatunga sera imara 
zisizokuwa na chembe ya kulinda masilahi yao, bali ziwe na upana wa 
kulinda masilahi ya wananchi.
Nyalandu alisema ataweka mifumo imara 
ya kisheria inayodhibiti viongozi wa ngazi za juu ambao ni watumishi wa 
umma kufanya biashara na uwekezaji pindi wanapokuwa madarakani, bali mtu
 afanye kazi moja ya kuwatumikia wananchi ama kufanya biashara.
“Tanzania
 kwa awamu hii inahitaji kuwa na rais anayefahamu tafsiri halisi ya 
umasikini na anayechukia jinamizi la ubaguzi na utengano baina ya 
wananchi wa nchi moja na kuondosha nyufa zilizopo katika Muungano, nami 
nimejipima nikaona uwezo huo ninao na sababu za kuiongoza nchi kwa 
uadilifu pia ninazo hivyo wananchi nakuombeni mfanye maamuzi ya 
kunichagua ili niwatumikieni,” alisema.
LUHAGA MPINA ACHUKUA FOMU, AAHIDI KUONGEZA MAPATO YA SERIKALI
MBUNGE wa Kisesa, Luhaga Mpina, naye ameungana na makada wengine wa CCM kuchukua fomu za kuwania kuteuliwa kugombea urais.
Mpina
 alichukua fomu hiyo mjini Dodoma jana, huku akijinasibu kuimarisha 
ukusanyaji wa mapato ya ndani na kudhibiti mapato yanayokusanywa.
“Nitakuja
 na njia mbadala ya kuhakikisha mapato ya ziada yanapatikana ili kupata 
fedha kwa ajili ya huduma za jamii katika sekta mbalimbali kama vile 
elimu na afya.
“Kwa sasa watu hawalipi kodi, mikataba mibovu 
inatafuna taifa, mikataba ya gesi ina kasoro kubwa, makampuni makubwa ya
 madini yanakwepa kodi kwa kiwango kikubwa, haya mambo ninayafahamu na 
nitayasimamia,” alisema.
Mpina aliahidi kuongeza mapato ya Serikali mara tatu zaidi.
“Wale
 waliozoea kufuja mali za umma, kuiba na kufanya ubadhirifu, nitakuja na
 mbadala wa kumwajibisha mwenye jukumu la kuchukua hatua.
“Watanzania
 wanipe dhamana, wizi huu, utoroshaji wa fedha za umma utafika mwisho, 
kama kuna watendaji wanaona hawawezi kuacha basi siku wakisikia 
naapishwa wajiondoe kabisa mana watakiona cha mtema kuni,” alisema.
Mpina
 aliahidi kuboresha hospitali na shule nchini ili viongozi wakiwamo 
wabunge waache kuzinyanyapaa hospitali zao kwa kwenda kutibiwa nje ya 
nchi pamoja na kutowasomesha watoto wao katika shule za Serikali.
CHIFU WA RUNGWE AMPIGIA DEBE MAKONGORO
CHIFU
 wa Wilaya ya Rungwe, Prince Mwaihojo amesema Makongoro Nyerere ni 
kiongozi mzuri ambaye ameonekana kuwa na uwezo mkubwa wa kuwaunganisha 
watu.
Aliyasema hayo jana wilayani Rungwe, Mbeya wakati Makongoro – 
mtoto wa tano wa Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere,
 alipokwenda kutafuta wadhamini watakaomdhamini kwenye nafasi ya urais.
“Nchi
 ilivyo sasa imekosa kiunganishi, ukiangalia wagombea wote wanajinadi 
kwa kufuata sera za Baba wa Taifa na hiyo inatokana na chama kupoteza 
dhana nzima ya kuwa chama cha wafanyakazi na wakulima, na badala yake 
kugeuka na kuwa chama cha walanguzi,” alisema.
Alisema Makongoro 
anaweza kuifanya kazi ya kurudisha amani na upendo kwa asilimia 60 
kutokana na mtaji wa baba yake, huku asilimia 40 ni kutokana na uadilifu
 na uzoefu katika siasa.
Naye Makongoro ambaye ni Mbunge wa Afrika 
Mashariki, akizungumza na umati mkubwa wa wafuasi wa CCM, aliwataka 
wakazi wa Mkoa wa Mbeya kuhakikisha wanamuunga mkono na kumchagua kuwa 
rais wa Tanzania.
MANGULA : MATENDO YA WATANGAZA NIA YANAREKODIWA
MAKAMU
 Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Philip Mangula, amesema 
vitendo vyote vinavyofanywa na wagombea wa urais ndani ya chama hicho 
wakati huu wanapotafuta wadhamini vinaingia katika rekodi ya chama.
Mbali
 na hilo, aliwataka wanachama wa chama hicho kutambua mchakato wa 
kugombea au kuwapata wagombea kwa nafasi ya udiwani, ubunge na 
uwakilishi bado haujaanza.
Mangula, alitoa kauli hiyo mjini Dodoma 
jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mchakato 
unaoendelea sasa ndani ya CCM wa kumpata mwanachama atakayegombea urais 
wa Jamuhuri ya Muungano na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Alisema
 rekodi hizo zitatumika katika mchakato wa uteuzi wa wagombea hao ambapo
 majina matano ndiyo yatateuliwa kwa ajili ya kwenda kupigiwa kura 
katika kikao cha Halmashauri Kuu (NEC).
“Vikao vya uteuzi vitafanyika
 kwa kutumia kanuni za uteuzi wa wagombea wa CCM katika vyombo vya dola 
na kanuni za viongozi na maadili za chama chetu,” alisema.
Kanuni hizo pamoja na mambo mengine zinaeleza mambo ya kuzingatia kwa wagombea na pia zinaeleza sifa za mgombea wa urais.
“Kwa
 mujibu wa Kanuni ya Uteuzi kifungu cha 20(5) kutangaza nia kunaruhusiwa
 ila ni marufuku kwa mgombea au wakala wake kufanya vitendo 
vinavyoonekana ni kufanya kampeni kabla ya muda,” alisema.
Alisema 
kifungu za 20 cha Kanuni za Uteuzi, kinasema kwamba maadili na nidhamu 
ya chama katika kusimamia na kutekeleza shughuli za uteuzi wa wagombea 
wa CCM katika vyombo vya dola lazima vizingatiwe na wale wote 
wanaohusika.
Mangula alisema kanuni hiyo pia inapiga marufuku 
wagombea kutumia ukabila, dini, rushwa, rangi, hila na eneo analotoka 
katika shughuli ya uchaguzi.
“Ni mwiko pia kwa mgombea kufanya 
kampeni za kupakana matope na ya aina nyingine yoyote dhidi ya mgombea 
mwingine, ni mwiko kwa mgombea aliyekabidhiwa dhamana ya usimamizi, 
uchujaji na uteuzi kufanya vitendo vya ukiukwaji wa kanuni,” alisema 
Mangula.
Alisema kanuni hizo zinaeleza sifa 13 za mgombea wa urais 
ambazo vikao vya uteuzi vitazingatia sifa hizo wakati wa mchujo wa 
wagombea.
“Baadhi ya sifa hizo, ni pamoja na awe na elimu kuanzia 
chuo kikuu, awe na upeo wa kudumisha na kuendeleza muungano na asiwe 
mwenye hulka ya udikteta,” alisema.
Alizitaja sifa nyingine kwamba 
awe mtetezi wa wanyonge, asiwe na tamaa ya kujitafutia umaarufu, mpenda 
haki, asitumie nafasi yake kujilimbikia mali, awe na uwezo wa kuilinda 
katiba, sheria za nchi na utawala bora, atambulike na wananchi na awe na
 uwezo wa kusimamia majukumu ya utendaji na uwajibikaji.
Alisema wagombea wote watapimwa kwa sifa hizo katika vikao vya mchujo.
Kwa
 upande wa nafasi za udiwani, ubunge na uwakilishi, Mangula alisema 
mchakato wa kuwapata wagombea wa nafasi hizo ndani ya chama bado 
haujaanza.
“Hivyo napenda kuwaambia wenye nia ya kugombea nafasi hiyo wajiepushe na vitendo vitakavyoonekana ni kufanya kampeni.
Taarifa hizi zimeandaliwa na Pendo Fundisha (Mbeya), Debora Sanja (Dodoma), Is-haka Omar (Zanzibar) na Elias Msuya (Pemba)
CHANZO: MTANZANIA