Mpekuzi blog
WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa jana aliingia wilayani Geita na
 kupokewa na umati wa wananchi ambako alidhaminiwa na zaidi ya wana CCM 
3,000.
 
Kaimu Katibu wa Wilaya ya Geita, Killian Balindo alisema waliotakiwa 
kumdhamini Lowassa katika wilaya hiyo ni wanachama 45, lakini 
waliojitokeza wamefikia zaidi ya 3,000.
  
Akizungumza na wananchi waliokusanyika mbele ya ofisi ya CCM Mkoa wa 
Geita, Lowassa alisema japo haruhusiwi kufanya kampeni ameahidi 
kushughulikia matatizo ya maji, wachimbaji wadogo na mawe yaliyoisha 
dhahabu (magwangala).
  
“Hayo ya bodaboda, mamantilie kushughulikia. Nikiingia ikulu ni kuweka 
tu kalamu nyekundu. Kazi yangu ikikamilika nitashughulikia magwangala,” 
alisema Lowassa.
  
Kuhusu wachimbaji wadogo, alisema atawapa kipaumbele kwa kuwamilikisha maeneo ya uchimbaji na mitaji.
  
“Nilipokuwa mbunge miaka ya 80, niliondoa shilingi bungeni kupinga 
wachimbaji wadogo kunyanyasika. Nitahakikisha kila mchimbaji anapata 
eneo lake. Serikali inajua maeneo yote yenye madini. Halafu tutawapa 
fedha ili wawekezaji wakubwa wakija waweze kushindana,” alisema Lowassa.
  
Msafara wa Lowassa ulikuwa na magari, pikipiki na baiskeli huku 
ikisindikizwa na helikopta ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita, Joseph 
Msukuma.
  
Awali Lowassa jana aliingia katika Jimbo la Chato linaloshikiliwa na 
Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli na kupata mapokezi makubwa ya 
wanachama waliojitokeza kumdhamini.
  
Dk. Magufuli ambaye pia amechukua fomu za kugombea urais bado hajafika jimboni humo kutafuta wadhamini.
  
Lowassa aliingia Chato saa 8:30 mchana na kuelekea kwenye ukumbi wa ofisi ya CCM wilaya walikokuwa wamekusanyika wana CCM.
  
Akizungumzia udhamini huo, mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM wilayani 
humo, Deusdedith Katwale, alisema wanachama waliojitokeza kumdhamini 
wamefikia 430.
  
“Tunashukuru kwa kuipa kipaumbele Chato, hiyo ina maana sana siku zijazo,” alisema Katwale.
  
Naye Lowassa aliwashukuru wanachama hao na kurudia wito wake wa kuchagua rais aliyebobea katika chama.
  
“Tunakwenda kuchagua rais, tutafute mtu anayekijua chama. Angalieni 
historia yake na rekodi ya mambo aliyofanya,” alisema Lowassa.
  
Awapongeza  wana Pemba
Awali akiwa kisiwani Pemba jana asubuhi, Lowassa amewasifu wanachama 
wa CCM kisiwani Pemba kwa kujiimarisha dhidi ya upinzani mkali wa Chama 
cha Wananchi (CUF).
  
Tangu kuanza kwa siasa za upinzani mwaka 1995, CCM imekuwa katika wakati mgumu visiwani Zanzibar, na hasa Pemba.
  
Akizungumza na wana CCM wilayani Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba 
alikokwenda kutafuta udhamini kwa ajili ya kupitishwa kugombea urais 
kupitia chama hicho, Lowassa alisema wana CCM kisiwani humo wanastahili 
pongezi.
  
Alisema alifika kisiwani humo mara ya mwisho mwaka 1984 na kwamba 
akifanikiwa kupata urais atafanya ziara ya muda mrefu kisiwani humo.
  
“Nilifika hapa mwaka 1984 na sijawahi kurudi tena. Lakini endapo nitafanikiwa safari yangu, nitakuja siku mbili tatu tuzungumze.
  
“Nawapongeza kwa jitihada zenu, licha ya upinzani mkali wa CUF bado 
mmeendelea kujiimarisha. Nitakuja Pemba siku mbili tatu nitakapofanikiwa
 ili tuzungumze,” alisema.
  
Lowassa pia alizungumza na wana CCM wa Wilaya ya Chakechake, Mkoa wa 
Kusini Pemba na kuwapongeza kwa jitihada zao za kukilinda chama chao 
licha ya upinzani mkali.
Lowassa alifanikiwa kupata udhamini wa wana CCM 90 katika wilaya za Wete na Micheweni Mkoa wa Kaskazini.
  
Akizungumzia hali ya chama hicho wilayani Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba, 
mmoja wa makada wa CCM, Juma Amir Juma alisema wanachokitegemea ni 
rehema za Mwenyezi Mungu.
  
“Hatusemi tutaendelea kushindwa, Mungu ni mkubwa ipo siku tutashinda. 
Lakini hali ni mbaya sana, kwani kama Mbunge wa CUF anapata kura zaidi 
ya 5,000 wa CCM anapata kura 500, wapi na wapi? Lakini hatukati tamaa,” 
alisema Juma.
  
Katibu wa CCM mkoa wa Kaskazini Pemba, Ali Haji Makame, alisema kuna 
wana CCM wengi walitamani kumdhamini Lowassa, lakini wameshindwa 
kutokana na idadi maalumu kuwekwa na kanuni za chama hicho ambayo ni 
wanachama 45 kwa kila wilaya.
  
Lowassa aliwasili Zanzibar juzi na kupokewa na umati mkubwa wa wanachama
 wa CCM walioandamana naye hadi katikati ya mji wa Unguja.
  
Kwa ujumla Lowassa amepata wadhamini 450 katika visiwa vya Unguja na Pemba.