MAGUFULI: MAUAJI YA KIMBARI HAYAFAI KUJIRUDIA

Marais John Magufuli na Paul Kagame wakiwasha mwenye eneo la Gisozi
Rais wa Tanzania John Magufuli amesema mauaji ya kimbari sawa na yaliyotokea nchini Rwanda hayafai kuruhusiwa kutokea tena.
Akizungumza mara baada ya kutembelea
jumba la makumbusho mauaji ya Kimbari ya mwaka 1994, Rais Magufuli
amesema amesikitishwa sana na mauaji hayo.
"Haitatokea tena, hatuwezi kubadilisha
yaliyopita lakini tunaweza kubadilisha mambo ya sasa na yajayo, mauaji
haya hayapaswi kutokea tena," amesema Dkt Magufuli, kwa mujibuwa taarifa
kutoka ikulu.
Rwanda imekuwa ikiadhimisha kumbukumbu ya
miaka 22 ya tangu kutokea kwa mauaji ya kimbari yaliyosababisha vifo
vya watu takribani 800,000.
Rais Magufuli na mwenyeji wake Paul
Kagame waliwasha mwenge utakaowaka kwa kipindi cha siku 100 yaliyodumu
mauaji ya kimbari ya Rwanda katika eneo la makumbusho hayo Gisozi.
Mkuu wa kitengo cha Rwanda cha kupambana
na mauaji ya kimbari Dkt Jean Damascene Bizimana, akihutubu wakati wa
maadhimisho mafupi ya kukumbuka mauaji hayo, amezihimiza nchi za Afrika
Mashariki kubuni sheria za kufwatilia na kuwadhibiti watu wanaoeneza
itikadi za mauaji ya kimbari.
Tanzania na Rwanda zafungua ukurasa mpya
Amesema nchi za Burundi na Jamuhuri ya
Kidemokrasia ya Congo zilitoa hifadhi na kushirikiana na wapiganaji wa
kundi la FDLR wanaotuhumiwa kutekeleza mauaji hayo.
Amesema Rwanda imefurahishwa sana na
taifa la Ujerumani kwa kuwakamata na kuwahukumu vinara wa kundi hilo
wanaoishi nchini Ujerumani kutokana na mchango wao katika mauaji
yanayotekelezwa na kundi hilo nchini Congo.
Viongozi hao wa FDLR ni Ignace Murwanashyaka aliyehukumiwa miaka 13 jela na Straton Musoni aliyehukumiwa miaka 8 jela.
Mwandishi wa BBC aliyeko Rwanda Yves
Bucyana anasema kutakuwa na wiki nzima ya maombolezo kukumbuka waliouawa
wakati wa mauaji hayo.
Shughuli za michezo na burudani zimepigwa marufuku huku bendera zikipepea nusu mlingoti.
Dkt Magufuli amekuwa kwenye ziara rasmi
ya siku mbili nchini Rwanda, ziara yake ya kwanza nje ya nchi tangu
kuingia madarakani Novemba mwaka jana.
Ameondoka Kigali na kurejea Dar es Salaam.BBC
No comments:
Post a Comment