DPP Adhamiria Kumrudisha Shehe Ponda Issa Ponda Kizimbani... Akata Rufaa Mahakama Kuu Kupinga Kuachiwa Kwake
MKURUGENZI wa Mashitaka (DPP) ameamua kukata rufaa Mahakama Kuu dhidi ya kesi ya uchochezi inayomkabili mwanaharakati wa Kiislamu Shehe Ponda Issa Ponda.
Mwanasheria Mwandamizi katika ofisi ya DPP, Bernard Kongola
 amesema kuwa Serikali inapinga kuachiwa kwa Shehe Ponda ambaye 
alishitakiwa kwa makosa ya uchochezi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi 
Morogoro.
“Tayari tumeomba tupatiwe nakala ya hukumu pamoja na 
nyaraka za mwenendo wa shauri hilo ili upande wa mashitaka tuweze 
kuandaa rufaa yetu Mahakama Kuu,” alisema.
Kwa mujibu wa mwanasheria huyo, tangu waombe kupatiwa 
nakala ya hukumu hiyo katika mahakama hiyo ya hakimu mkazi, hakimu 
ambaye alikuwa anasikiliza kesi hiyo bado hajawapatia upande wa 
mashitaka hukumu ambayo imechapwa.
“Hatujui kuna tatizo gani, maana tunapoomba kupatiwa nakala
 ya hukumu, hakimu amekuwa anatuambia kwamba bado hawajamaliza kuichapa,
 kwa kweli hii inashangaza,” alisema.
Novemba 30 mwaka uliopita, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya 
Morogoro, Mary Moyo alimwachia huru Shehe Ponda kwa maelezo kuwa upande 
wa mashitaka ulishindwa kuthibitisha pasi shaka yoyote mashitaka dhidi 
ya mwanaharakati huyo wa Kiislamu.
Wakati kesi hiyo ilipokuwa inasikilizwa, upande wa 
mashitaka uliita mashahidi wanane kwa lengo la kuthibitisha makosa dhidi
 ya Shehe Ponda ambaye alikuwa anatetewa na Mawakili wa kujitegemea Juma
 Nassoro na Abubakar Salum.
Shehe Ponda alifikishwa katika mahakama hiyo Agosti 19, 
2013 akikabiliwa na mashitaka matatu likiwemo la kukaidi amri ya 
Mahakama ya Kisutu iliyomtaka awe mhubiri amani katika jamii likiwa ni 
sharti la kifungo cha mwaka mmoja nje baada ya kumtia hatiani katika 
kesi ya jinai.
Upande wa mashitaka ulidai kuwa Shehe Ponda alitenda kosa 
Agosti 10, 2013 katika eneo la Shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege iliyoko
 katika Manispaa ya Morogoro.
Ilidaiwa kuwa siku hiyo kiongozi huyo wa kidini alidaiwa 
kutoa maneno ya uchochezi ya kuhamasisha jamii kinyume na maelekezo ya 
mahakama.
Katika mkutano huo Shehe Ponda anadaiwa kusema maneno haya,
 “Ndugu Waislamu msikubali uundwaji wa kamati za ulinzi na usalama za 
misikiti, kwani kamati hizo zimeundwa na Bakwata ambao ni vibaraka wa 
CCM na Serikali na kama watajitokeza kwenu watu hao na kujitambulisha 
kwamba wao ni kamati za ulinzi na usalama za msikiti, fungeni milango na
 madirisha ya misikiti yenu na muwapige sana.”
Kauli hiyo inadaiwa kwenda kinyume cha amri ya Mahakama ya 
Hakimu Mkazi ya Kisutu, Dar es Salaam, iliyotolewa mahakamani hapo na 
Hakimu Victoria Nongwa, Mei 9, 2013 ambayo ilimtaka ndani ya mwaka mmoja
 kuhubiri amani na asifanye jambo lolote la uvunjifu wa amani na badala 
yake ahubiri suala la amani, ambayo ni kinyume cha Kifungu cha Sheria 
Namba 124 cha Mwaka 2002.
Shitaka la pili lililokuwa likimkabili Shehe Ponda ni 
uvunjifu wa sheria Kifungu cha 129 cha Makosa ya Jinai kuwa siku hiyo, 
alitoa maneno ya uchochezi yaliyohatarisha kuathiri imani za watu 
wengine.
Katika hati ya shitaka hilo, ilinukuu kauli ya Ponda kuwa 
“Serikali ilipeleka Jeshi Mtwara kushughulikia suala la vurugu 
iliyotokana na gesi kwa kuwaua, kuwabaka na kuwatesa wananchi kwa sababu
 asilimia 90 ya wakazi wake ni Waislamu. Lakini Serikali haikufanya 
hivyo kwa wananchi wa Loliondo walipokataa Mwarabu asipewe kipande cha 
ardhi ya uwindaji baada ya kudai ni mali yao kwa sababu asilimia 90 ya 
wakazi wake ni Wakristo.”
Shitaka la tatu anadaiwa kutenda kosa kinyume cha sheria 
kifungu cha 390 na 35 kwa kuchochea maneno dhidi ya wananchi wakati wa 
kongamano lililofanyika Agosti 10, 2013 Uwanja wa Shule ya Msingi 
Kiwanja cha Ndege.
 
  





































